Changamoto hii pia inaonekana Zanzibar, ambapo wataalamu wa afya wameendelea kubainisha uwepo wa kiwango kikubwa cha wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha juhudi za kinga, uchunguzi wa mapema na elimu ya afya kwa jamii.
Ni katika muktadha huo ambapo Vodacom Tanzania Foundation inaendelea na mpango wake wa muda mrefu wa kambi za afya bila malipo, mpango ambao umetekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika mikoa saba na wilaya 16 nchini Tanzania. Mwaka huu, mpango huu umeanza Zanzibar kwa mara ya kwanza, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Foundation ya kupanua upatikanaji wa huduma za afya za kinga kwa jamii mbalimbali.
Kambi ya afya inayofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 6 Februari, inalenga uchunguzi wa mapema na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kupitia huduma za upimaji wa afya, ushauri wa kitaalamu pamoja na elimu ya afya. Umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuboresha afya ya jamii ulidhihirishwa wakati wa ufunguzi rasmi wa kambi hiyo uliofanyika Jumatano, Februari 4, 2026, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Msafiri Marijani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Marijani alisisitiza mchango wa mipango ya kinga katika kupunguza athari za muda mrefu za magonjwa yasiyoambukiza.
“Shinikizo la damu na kisukari vinaendelea kuwaathiri wananchi wengi Zanzibar, mara nyingi bila dalili za awali. Mipango inayohamasisha uchunguzi wa mapema, uelewa na hatua za kinga ni muhimu katika kusaidia jamii kudhibiti magonjwa haya na kuzuia madhara makubwa kiafya,” alisema.
Akithibitisha dhamira ya Vodacom Tanzania Foundation, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, alisema kambi hizi za afya zimebuniwa ili kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.
“Kwa upande wetu, mpango huu unalenga kuimarisha huduma, upatikanaji na athari chanya kwa jamii. Kwa kupeleka huduma za afya za kinga moja kwa moja kwa wananchi, tunawawezesha kuchukua hatua mapema kuhusu afya zao. Kuanzia Zanzibar mwaka huu ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa mpango huu,” alisema Sandra.
Aliongeza kuwa Vodacom Tanzania Foundation itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya na wadau mbalimbali ili kupanua mpango huo katika maeneo mengine, ikijenga juu ya uzoefu na mafanikio ya miaka iliyopita.
Mpango huu ni sehemu ya mchango mpana wa Vodacom Tanzania Foundation katika kuunga mkono Lengo la Maendeleo Endelevu namba 3 (SDG 3): Afya Njema na Ustawi, unaolenga kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote.
Vodacom Tanzania Foundation inawahimiza wakazi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kambi hii ya afya, ikisisitiza kuwa uchunguzi wa mapema, uelewa na kinga ni nguzo muhimu katika kujenga familia zenye afya njema na jamii imara.
Mkurugenzi Idara ya Tiba ya Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani (wapili kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kambi ya Huduma za Afya na Vodacom Tanzania Foundation.Ikilenga kutoa huduma bure za upimaji wa afya, ushauri na elimu juu ya magonjwa yasiyo ambukiza kama shinikizo la damu na kisukari.
Kambi hii ya huduma za Afya inatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine hivi karibuni.
Tukio hili limefanyika Visiwani Zanzibar na kushuhudiwa na Kaimu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Julieth Magandi ( Kushoto), Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation Sandra Oswald (wapili kulia)..jpeg)

.jpeg)