Sh28.3 bilioni kufikisha umeme vitongoji 173 Songwe

Songwe. Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imetenga jumla ya Sh28.3 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 173 mkoani Songwe, ambavyo hadi sasa havijafikiwa na huduma ya umeme.

Mradi huo umeanza rasmi kutekelezwa kuanzia Januari 31, 2026 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu hadi ifikapo Januari 30, 2029.
Katika kipindi hicho, utekelezaji wa miradi ya awamu mbalimbali utafanyika kwa lengo la kufikisha umeme katika maeneo yote yaliyotengwa ndani ya muda uliopangwa.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo leo Jumatano Januari 4, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omary Makame amesema unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wananchi waishio vijijini; zaidi ya wananchi 6,000 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja.

Makame amesema tayari vijiji vyote 307 vya mkoa huo vimefikiwa na huduma ya umeme huku vitongoji 1,073 navyo vimefikiwa na umeme kati ya vitongoji 1,489 vilivyopo mkoani humo.

Makame amesema kupitia mradi huo, vitongoji hivyo vitaunganishwa na umeme kwa awamu kulingana na mpango wa utekelezaji uliowekwa na Serikali.

“Utekelezaji wa mradi huu utawezesha wananchi kupata huduma muhimu za kijamii na kiuchumi ikiwemo kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali, biashara ndogondogo, viwanda vidogo, pamoja na kuboresha huduma za elimu na afya katika maeneo husika,” amesema Makame.

Amesema mradi huo utatoa fursa za ajira kwa wananchi katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu ya umeme huku serikali ikieleza kuwa umeme huo unapaswa kutumika kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi na si kwa matumizi ya kawaida pekee.

“Kupitia mradi huu, gharama za kuunganishiwa umeme kwa wananchi wa vijijini zitatolewa kwa gharama ya Sh27,000, hatua itakayowawezesha wananchi wengi zaidi kumudu gharama za kuunganishwa na huduma ya umeme,” amefafanua Makame.

Amewahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na wataalamu watakaotekeleza mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, kwa manufaa ya maendeleo endelevu ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza jana Februari 3, 2027 baada ya kuwapokea makandarasi kutoka Kampuni ya Jai Tech watakaotekeleza mradi huo wilayani Ileje, Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi alisema mkandarasi huyo atasambaza umeme katika vitongoji 48 vya kata mbalimbali wilayani Ileje ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme.

Mgomi amesema mradi huo unatarajiwa kuleta neema na ahueni kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje, hususan waishio katika vitongoji ambavyo havikuwa na huduma hiyo, hali itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Niwahimize wakandarasi mliopewa kazi hii wilayani Ileje kutekeleza kwa weledi, umakini na ufanisi, sambamba na kuhakikisha mnakamilisha kazi mapema ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo kwa wakati,” amesema Mgomi.