Tabora. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, leo amewaongoza waombolezaji katika maziko ya aliyewahi kuwa mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Munde Tambwe.
Mbunge huyo mstaafu alifarikidunia usiku wa kuamkia Februari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatano, Februari 4, 2026, katika maziko hayo yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu eneo la Cheyo, Manispaa ya Tabora, Dk Nchimbi amesema Munde alikuwa kiongozi na mtendaji mahiri aliyekuwa mstari wa mbele kupambana na changamoto za wananchi wake.
Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi akizungumza na waombolezaji msibani nyumbani kwa Munde Tambwe
Amesema ni miongoni mwa viongozi wanaoweza kutajwa kwa kujivunia kutokana na uadilifu na mchango wake kwa Taifa na wananchi wa Tabora.
“Munde ni miongoni mwa viongozi ambao tunaweza kuwazungumzia kifua mbele kabisa bila woga, kwa maana ni rasilimali iliyotumika ipasavyo kabla ya kuondoka kwake,” amesema makamu huyo wa Rais.
Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi, akibainisha kuwa ndiyo misingi aliyokuwa akiishi marehemu Munde.
Amesema kwa kiongozi yeyote yule, kuwekeza kwenye jamii na kuishi vizuri na watu unaowaongoza, ni njia bora ya kutatua changamoto za wananchi pale uwezo unapokuwepo.
Aidha, amesema Rais Samia ametoa pole kwa wananchi wa Tabora na Watanzania kwa ujumla na amemtuma awahakikishie kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha majonzi. “Tumuombee mwenzetu ili safari yake iwe nyepesi aendako,” amesema Dk Nchimbi kwa niaba ya Rais Samia.
Waombolezaji wakiwa msibani nyumbani kwa Munde Tambwe
Akizungumza awali msibani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha alisema taifa limepoteza kiongozi mwadilifu, mwaminifu na aliyekuwa na uhusiano mzuri na wana Tabora. Amesema marehemu alikuwa akifuatialia kwa umakini mkubwa masuala yaliyokuwa yanahusu maendeleo ya mkoa huo.
“Tunaweza kusema tumepoteza mtu muhimu sana kwetu, kwa sababu Munde alikuwa miongoni mwa viongozi waliothamini sana mahusiano na wananchi na alikuwa mstari wa mbele katika mambo yanayogusa Tabora,” amesema Chacha.
Naye Mbunge wa Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga amesema Mkoa wa Tabora umepata pigo kubwa kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa bado anahitajika.
Amesema marehemu hakuwa tu kiongozi bali pia alikuwa dada mkubwa kwa wengi kutokana na tabia yake ya malezi na namna alivyokuwa akiishi na watu.
“Tunaweza kusema mengi kumzungumzia dada yetu Munde, lakini itoshe kusema tumuombee apumzike kwa amani na sisi tulio baki tuige mfano wa maisha yake ya kujitolea kwa jamii,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amewashukuru watu wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha msiba, akisema familia haina namna ya kuwalipa waliotenga muda wao kuhudhuria na kushiriki katika maziko hayo.
“Sisi hatuna cha kuwalipa zaidi ya kusema asanteni kwa kuwa karibu nasi. Ni ahadi yetu kuwa tutaendelea kushirikiana na wana Tabora na taifa kwa ujumla, kama alivyokuwa marehemu,” amesema Bashe.
Waumini wa dini ya kiislam wakiswalia jeneza la Munde Tambwe
Msiba huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wa chama, akiwemo Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Mary Chatanda na wabunge kutoka majimbo mbalimbali nchini na Mkoa wa Tabora, ambao pia walitoa salamu za rambirambi.
Mbali na kuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora kwa kipindi cha miaka 15 mfululizo, Munde alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, nyadhifa zilizokoma mwaka 2025 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.