Hizi hapa saratani 10 zinazoitafuna Dar

Dar es Salaam. Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) imezitaja aina 10 za saratani zinazosumbua katika Mkoa wa Dar es Salaam, huku saratani ya utumbo ikitajwa kuongoza kwa wanaume na kwa wanawake ni saratani ya mlango wa kizazi.

Takwimu hizo zimetajwa leo, Jumatano, Februari 4, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo, alipokuwa akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa katika maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani. Maadhimisho hayo yameandaliwa na GSM Foundation kwa kushirikiana na Radiotherapists Association of Tanzania (Raota), yaliyofanyika hospitalini hapo.

Takwimu za kanzi data ya saratani kwa Dar es Salaam kwa mwaka 2023, zinaonesha aina za saratani zinazoongoza kwa wanaume ni saratani ya utumbo asilimia 18.4, saratani ya koo la chakula asilimia 12, saratani ya ini asilimia 10.1, saratani ya tezi dume asilimia 10 pamoja na saratani ya mapafu kwa asilimia 8.

Kwa upande wa wanawake aina za saratani zinazoongoza ni ya mlango ya kizazi kwa asilimia 18.2, saratani ya utumbo asilimia 15.1, saratani ya matiti asilimia 12.6, saratani ya ini asilimia 11.8 na saratani ya koo asilimia 5.7.

Aina za saratani, dalili zake

Saratani ya utumbo, inaanzia kwenye utumbo mpana, sehemu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Tofauti na saratani nyingi, saratani ya utumbo mpana inaweza kuzuilika kwa kufanya vipimo vya uchunguzi mapema (screening) na pia hutibika kwa mafanikio makubwa inapogundulika mapema.

Njia za kuepuka ni pamoja na kula lishe bora, kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi, kuepuka uvutaji wa sigara, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kudhibiti uzito wa mwili pamoja na kutibu magonjwa ya utumbo mapema.

Saratani ya pili inayosumbua ni ya koo la chakula kwa asilimia 12. Saratani hii hushambulia koo linalopeleka chakula kutoka mdomoni kwenda tumboni.

Dalili zake ni pamoja na ugumu au maumivu wakati wa kumeza, kupungua uzito bila sababu, na wakati mwingine kutapika damu kwa baadhi ya wagonjwa.

Saratani hii husababishwa na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, kiungulia cha muda mrefu na lishe duni ya matunda na mboga.

Saratani ya tatu ni ya ini, ikiwa na asilimia 10.1, ambayo hushambulia ini, kiungo muhimu kinachosaidia kusafisha sumu mwilini na kumeng’enya chakula.

Dalili zake ni pamoja na maumivu upande wa juu wa tumbo (kulia), kuvimba tumbo, kupungua uzito bila sababu, unjano katika macho na ngozi, kuchoka sana, na kukosa hamu ya kula.

Saratani hii huweza kusababishwa na maambukizi ya muda mrefu ya homa ya ini (Hepatitis B na C), unywaji wa pombe kupita kiasi, ini lenye mafuta (fatty liver), sumu kama aflatoxin kwenye vyakula vilivyohifadhiwa vibaya, kisukari, na unene kupita kiasi.

Saratani ya nne ni tezi dume (prostate) asilimia 10. Huu ni ugonjwa unaoshambulia tezi ndogo ya kiume, tezi inayosaidia uzalishaji wa mbegu.

Dalili zake ni kupata shida au maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara (hasa usiku), au mkojo/manii kuwa na damu.

Sababu zake mara nyingi ni pamoja na umri mkubwa (hasa kuanzia miaka 50), historia ya saratani ya tezi dume kwenye familia, lishe yenye mafuta mengi, kutofanya mazoezi, na unene kupita kiasi.

Saratani ya tano ni ya mapafu, asilimia nane amabyo ushambuliaji wake ni pamoja na kikohozi cha muda mrefu kisichoisha, kikohozi chenye damu, maumivu ya kifua, kupumua kwa shida au kubanwa kifua, na kupungua uzito na uchovu usioelezeka.

Husababishwa na uvutaji wa sigara, moshi wa sigara kwa wasiovuta (secondhand smoke), vumbi, kemikali kazini, na uchafuzi wa hewa.

Kwa wanawake, aina zinazojitokeza zaidi ni saratani ya mlango wa kizazi, asilimia 18.2 ambayo hushambulia sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi (cervix), inayounganisha mfuko wa uzazi na uke.

Dalili zake ni kutokwa na damu isiyo ya kawaida, maumivu ya nyonga, kutokwa na uchafu wa ukeni wenye harufu mbaya, na maumivu wakati wa tendo la ndoa, huku sababu zikiwa ni pamoja na maambukizi ya virusi vya HPV, kinga dhaifu ya mwili, na kutofanya uchunguzi wa mara kwa mara. Inashauriwa watu kupata chanjo ya HPV, kufanya uchunguzi mapema, na kuepuka ngono zisizo salama.

Aina nyingine ni saratani ya utumbo, asilimia 15.1; saratani ya matiti, asilimia 12.6; saratani ya ini, asilimia 11.8 na saratani ya koo, asilimia 5.7.

Takwimu hizi zinaonesha saratani ya mlango wa kizazi bado inaongoza kwa mfululizo wa miaka 10 nchini, kwa takribani asilimia 23 hadi 24, kwa mujibu wa Taasisi ya Ocean Road.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, hadi mwaka 2024, kwa wastani katika wagonjwa 100 wa saratani, wanawake 25 wana saratani ya mlango wa kizazi.

Aina nyingine ni saratani ya matiti na koo, ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanawake 1,000, sita wana saratani ya koo.

Dk Diwani Msemo amesema saratani hizo zinaweza kuzuilika kwa kubadilisha mtindo wa maisha au kuzitambua mapema kupitia uchunguzi wa awali.

Amesema kuna chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti chini ya miaka 14, inayotolewa shule mbalimbali.

Mkurugennzi huyo amesema Watanzania wanapaswa kufanya uchunguzi mapema unaotolewa na taasisi hiyo, ambayo imefika mikoa yote na hadi sasa imechunguza watu 50,000 nchini kote.

“Juhudi mbalimbali zinaendelea za kupiga vita  saratani, ikiwemo matibabu kwa sehemu kubwa kuwa ya msamaha, mashine mbalimbali zinaletwa na Serikali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu,” amesema.

“Kwa jumla, takwimu zinaonesha saratani zinazoongoza ni mlango wa kizazi asilimia 23.5, matiti 10.1, tezi dume 8.4, koo 7.1, tumbo 5.1, na saratani nyingine 45.8. Hii inaonesha wanawake wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani ikilinganishwa na wanaume.”

Kinachofanywa na Serikali

Serikali imesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, ‘Ungana kwa upekee’ inalenga kuhakikisha tatizo la ugonjwa wa saratani linadhibitiwa kwa kuendelea kutoa elimu nchini, sambamba na kuhakikisha huduma za uchunguzi zinapatikana kote, kuimarisha mawasiliano na huduma bora kwa wateja kupitia Tehamana teknolojia ya kisasa.

Pia, Serikali inafadhili masomo ya ubingwa na bobezi, kuboresha miundombinu na vifaa tiba kwa Taasisi ya Ocean Road, Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za rufaa za kanda na mikoa, ili huduma za kibingwa na ubobezi zipatikane kwa gharama nafuu.

Katika kuhakikisha watu wanaepuka magonjwa hayo Serikali inashauri watu kujikinga kwa kuzingatia ulaji unaofaa kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga na matunda ya kutosha.

Kupunguza vyakula vyenye mafuta na chumvi nyingi, kuepuka vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi, kuacha tabia bwete, kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tano kwa wiki, kupunguza matumizi ya vilevi, kuepuka tumbaku na bidhaa zake, na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kupata matibabu mapema.

Kauli ya GSM, balozi wa saratani

Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu, amesema ushiriki wa taasisi hiyo ni sehemu ya dhamira ya muda mrefu katika kuboresha afya ya jamii kwa kukuza upatikanaji wa huduma bora, hususan kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

“Kwa mwaka wa tatu mfululizo, GSM Foundation imeamua kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani, ikitambua saratani na magonjwa yasiyoambukizwa kama changamoto kubwa kwa afya na ustawi wa Watanzania,” amesema.

Kwa upande wake, balozi wa saratani, Babuu wa Kitaa, amesema saratani inaweza kumpata mtu yeyote kwa wakati wowote, hivyo amekumbusha watu kuwa na utaratibu wa kupima.