Tarime. Diwani wa Kata ya Ketara (CCM) katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, Philipo Gikaro (60), amefariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari akiwa anaendesha pikipiki katika barabara ya Tarime–Nyamwaga, eneo la Kibumaye wilayani Tarime.
Diwani huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, jana Jumatano Februari 3, 2026.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 4, 2026, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Ghati, amesema marehemu alipata ajali hiyo majira ya saa 11 jioni akiwa njiani kurejea nyumbani kwake akitokea kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha halmashauri hiyo.
“Jana tulikuwa naye kwenye kikao cha kupitisha bajeti ya halmashauri na baada ya kikao ndipo alipata ajali hiyo. Alikuwa karibu kabisa kufika nyumbani kwake, kwa kuwa eneo alilopata ajali ni karibu na makazi yake,” amesema Ghati.
Amesema diwani huyo aligongwa na gari wakati akiendesha pikipiki, hali iliyosababisha kuvunjika mguu na mkono wa kulia.
Baada ya ajali hiyo, alipelekwa Hospitali ya Mji wa Tarime kwa ajili ya matibabu ya awali kabla ya kupewa rufaa kwenda hospitali ya mkoa kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Ghati amesema eneo alilopata ajali limekuwa likisababisha ajali mara kwa mara kutokana na kuwepo kwa korongo na bonde linalojaza maji wakati wa mvua, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.
“Pale kuna bonde na korongo, hivyo huwa ni vigumu kwa magari kupishana yenyewe kwa yenyewe au kupishana na pikipiki, jambo ambalo husababisha ajali,” amesema.
Ameongeza kuwa maziko yatafanyika Jumapili Februari 8, 2026, huku mwili wake tayari ukiwa umesafirishwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa Tarime.
Ghati amesema kifo cha diwani huyo ni pigo kubwa kwa halmashauri kutokana na umahiri, bidii na utendaji kazi wake ulioweza kuleta matokeo chanya kwa Kata ya Ketara ndani ya kipindi kifupi tangu achaguliwe.
Ameeleza kuwa mara baada ya kuchaguliwa, diwani huyo alibainisha changamoto mbalimbali za wakazi wa kata hiyo na kuanza kuzitafutia ufumbuzi, akianzia na ubovu wa barabara pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme.
“Aliwasilisha kero za barabara na umeme kwa Mkuu wa Mkoa mwishoni mwa Desemba mwaka jana alipofanya ziara katika kata hiyo. Mkuu wa Mkoa aliagiza Tarura na Tanesco kushughulikia changamoto hizo mara moja. Hivi sasa barabara zinaendelea kukwanguliwa na mafundi wa Tanesco wako eneo la kazi; yote haya ni kutokana na jitihada zake,” amesema.
Amesema changamoto nyingine aliyokuwa akiendelea kuifanyia kazi ni suala la Mlima Nkongore uliopo katika kata hiyo, ambapo alijitahidi kuhakikisha mlima huo unarejeshwa kwa wananchi ili utumike kwa shughuli za kilimo.
Mlima Nkongore, wenye ukubwa wa zaidi ya ekari 200, ulichukuliwa na Serikali mwaka 2020 baada ya kukithiri kwa kilimo cha bangi na kukabidhiwa Jeshi la Magereza kama sehemu ya mapambano dhidi ya kilimo hicho haramu wilayani Tarime.
Ghati amesema baada ya kuchaguliwa, diwani huyo aliahidi kushughulikia suala hilo ili mlima urejeshwe kwa wananchi kwa masharti ya kuhakikisha unatumika kwa kilimo chenye tija na matumizi sahihi.
“Kuna timu tayari imeundwa na Mkuu wa Mkoa kufanya tathmini ya maombi ya kurejeshwa kwa mlima huo kwa wananchi. Hii pia imetokana na juhudi za diwani huyu kuhakikisha rasilimali hiyo inawanufaisha wananchi,” ameongeza.
Amesema huu ulikuwa ni muhula wa kwanza kwa marehemu kuchaguliwa kuwa diwani wa Kata ya Ketara, baada ya kugombea mara mbili bila mafanikio.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa diwani, Gikaro alikuwa kada mtiifu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliwahi kuhudumu kama dereva wa wilaya kabla ya kustaafu.
