TFS yateketeza shamba la bangi hifadhini

Geita. Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Geita, kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeteketeza shamba la bangi lenye ukubwa wa ekari 3.5 lililokuwa katikati ya shamba la mahindi ndani ya hifadhi ya msitu wa Shamba la Miti Rwamgasa.

Uteketezaji wa shamba hilo umefanyika leo Jumatano Februari 4, 2026, zao hilo haramu lililimwa ndani ya hifadhi yam situ wenye ukubwa wa ekari 28,160.

Akizungumza wakati wakiendelea na kazi hiyo,  Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Rwamgasa, Mhifadhi Mwandamizi Aloyce Paschal, amesema shamba hilo liligunduliwa walipokuwa wakifanya doria za kawaida ndani ya hifadhi.

Paschal amesema ilikuwa vigumu kulibaini kutokana na mbinu iliyotumiwa ya kupanda bangi katikati ya mistari ya mahindi.

“Mkulima alikuwa akipanda mstari wa mahindi na mstari unaofuata anapanda bangi, hivyo ukiangalia kwa mbali unaona mahindi tu, lakini ndani yake kuna bangi,” amesema Paschal.

Mhifadhi Mkuu Shamba la miti Rwamgasa, Mhifadhi Mwandamizi Aloyce Paschal akizungumza wakati wa uteketezaji wa shamba la bangi Leo Februari 04, 2026.

Ameongeza kuwa hadi sasa mtu mmoja amekamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusiana na tukio hilo na anahojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Lucy Beda aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amewataka wananchi kuacha mara moja kujihusisha na shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi za misitu.

“Tunaendelea kutoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi zetu. Sote tunafahamu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani mvua tunayoipata ni matokeo ya utunzaji wa mazingira,” amesema Beda.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Busolwa B uliopo jirani na hifadhi hiyo, Lucas Mkondo amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika kuonewa wanapozuiwa kuingia hifadhini, bila kufahamu kuwa baadhi yao wanajihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria.

Shamba la bangi lililoteketezwa Leo ndani ya shamba la miti, hifadhi ya msitu Rwamgasa Geita.

“Nimejionea leo kuwa pori hili lilikuwa linalimwa bangi kwa wingi. Nimefyeka sana hadi kunitoka jasho. Wapo wanaolalamika kuonewa kumbe wanajihusisha na mambo yaliyo kinyume cha sheria,” amesema Mkondo.

Aidha, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Busolwa B, Kazimili Malindi aliyemwakilisha Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, amesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara na vikao mbalimbali ili kuiepusha jamii na madhara yatokanayo na kilimo cha bangi.