Hospitali ya Mkapa yaandaliwa ubingwa matibabu ya saratani

Dodoma. Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA) Kanda Afrika, wameagiza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kuwa tayari katika utoaji wa huduma za magonjwa ya saratani kwa wagonjwa wengine nje ya Tanzania.

Hii imetokana na kukubalika kwa miundombinu yake na mazingira yaliyoandaliwa kwa ajili ya utoaji wa huduma hiyo, ndani ya jengo linalojengwa ambalo linatarajia kuzinduliwa Septemba mwaka huu.

Mkurugenzi wa Shrika la Kimataifa la Nguvu za Atomu Kanda ya Afika Gashaw Wolde, amesema katika ukaguzi wake leo Jumanne Februari 3, 2026 licha ya kuwa jengo hilo halijakamilika lakini anaona maandalizi yake yanaashirikia mipango mikubwa kwa siku za usoni.

Wiki mbili zilizopita Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi, Madalitso Baloyi, alitangaza kuwa wananchi wa Malawi sasa wanaweza kupata matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini Tanzania hasa katika Hospitali ya Mkapa baada ya wataalamu wao kujiridhisha kuwa pangewafaa.

“Mawazo mazuri, ubunifu mzuri, asanteni sana Tanzania, nataka kusema hapa msifanye maandalizi ya kutibu Watanzania pekee, bali iwe ni hub ya kupokea wagonjwa kutoka mataifa majirani cha msingi tuwekeze kwenye rasilimali watu,” amesema Wolde.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk Henry Humba amesema ndani ya eneo lao wamejenga jengo lenye thamani ya Sh30.2 bilioni ambalo ni la kisasa na kwamba linatarajia kukamilika Agosti na ifikapo Septemba 2026 wataanza kutoa huduma ya kutibu saratani.

Dk Humbo amesema Shirika la Nguvu za Atomu Afrika, wamekuwa na ushirikiano nao tangu mwanzo wa kubuni mradi huo na tayari wameshasaidia kwa kiasi kikubwa hata kusomesha madaktari na kuwajengea uwezo watoa huduma.

“Pamoja na hayo lakini tunahitaji fedha za haraka Sh12 bilioni kwa ajili ya kununulia vifaa ambavyo vitafungwa ndani ya jengo hilo ili tuweze kutoa huduma za kisasa zaidi, lakini tupo tayari kupokea wageni kutoka nje kama alivyotuasa,” amesema Humba.

Mkurugenzi Mkuu wa Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Najat Mohammed amesema maandalizi ya ujenzi na kuanza kutoa huduma za saratani na mionzi inakwenda vizuri na kwamba mwaka huu wataanza huduma hiyo ili kuwapunguzia mzigo wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Kwa sasa hospitali zinazotoa huduma kutibu saratani ni Taasisi ya Saratani Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Bugando (Mwanza), KCMC (Kilimanjaro) na sasa maandalizi ya kutoa huduma hiyo yapo Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya rufaa ya Mbeya.