UDP CHAPINGA VIKALI KUVUNJWA MABARAZA YA ARDHI⁹

……..

CHATO

SIKU Chache baada ya Jaji mkuu wa Tanzania, George Masaju, kupendekeza kuvunjwa kwa mabaraza ya ardhi na nyumba, mabaraza ya Kata pamoja na Kamati za maadili za mahakimu ambazo zipo chini ya wakuu wa wilaya na mikoa, Chama Cha United Democratic Party (UDP) kimepinga vikali mapendekezo hayo.

Kinasema kuvunjwa kwa mabaraza hayo kutasababisha kucheleweshwa kwa haki za wananchi hasa waliopo gerezani kutokana na mrundikano wa kesi mahakamani.

Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu wa UDP wilaya ya Chato, Amos Lukinda, amesema Chama hicho hakikubaliani na mapendekezo yaliyotolewa na Jaji mkuu mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeshiriki katika mkutano wa mahakimu uliofanyika Januari 13, 2026.

Katika mkutano huo Jaji mkuu aliiomba serikali kuridhia kuvunjwa kwa mabaraza ya ardhi na nyumba, mabaraza ya Kata pamoja na kamati za maadili ya mahakimu zinazosimamiwa na wakuu wa wilaya na mikoa kwa madai ni wanasiasa.

Kutokana na hali hiyo, Chama Cha UDP kimeishauri serikali kutazama nini lililokuwa kusudio la kuanzishwa kwa mabaraza hayo katika jamii badala ya kupokea ushauri wa Jaji mkuu na kuutekeleza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu huyo, kuyafuta mabaraza ya ardhi na nyumba kutarejesha msongamano wa kesi katika mahakama za mwanzo na wilaya jambo ambalo awali lilikuwa likilalamikiwa sana na wananchi kutokana na baadhi ya kesi zao kuchukua muda mrefu pasipo kumalizika.

Aidha kutokana na mahakimu kuelemewa na wingi wa mashauri mahakamani, sheria iliamua kuwapa nafasi ya kumaliza shauri kwa kipindi cha miaka miwili, jambo ambalo bado ni changamoto katika upatikanaji wa haki kwa haraka.

Kadhalika, UDP kimeitaka serikali kutambua kuwa uwepo wa mabaraza ya kata ni urithi wa taifa kutoka kwa waasisi waliopokea ushauri kutoka kwa majaji na wanasheria kabla ya kuanzishwa mwaka 1985.

“Mabaraza hayo walikusudia kusuruhisha masula ya ndoa na ardhi kabla ya kufikishwa mahakamani na kwa uchache kesi zilizoshindwa kupata usuruhishi ndizo pekee zilipelekwa mahakamani na kutoa mwanya wa kesi zingine kuendelea kusikilizwa haraka” amesema Lukinda

Vile vile katika tamko hilo, UDP kimependekeza kuendelea kuwepo kwa Kamati ya maadili ya mahakimu inayosimamiwa na wakuu wa wilaya na mikoa ili kutoa mwanya kwa wananchi kufikisha maoni yao kwa viongozi hao badala ya mahakimu wenyewe.

“Aidha kuhusu wazo la Mheshimiwa Jaji eti kamati za maadili kwa mahakimu zivunjwe na badala yake wao mahakama ndiyo wajichunguze kwa makosa yao ni wazo lisilo kubalika, hakiwezi kuwa chombo kinacholalamikiwa ndicho tena kijichunguze chenyewe” amesema Lukinda.

Hata hivyo UDP kimeiomba serikali kupokea ushauri wa Jaji mkuu wenye nia ya kuboresha na siyo kuvunja mabaraza hayo ambayo yamekuwa kimbilio na unafuu wa wananchi wanyonge, na iwapo kuna changamoto zifanyiwe kazi kuliko kuvunja kwa madai hata mahakama za kawaida changamoto bado zipo.

                       Mwisho.