Morogoro. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (Moruwasa), Sais Kyejo amesema licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kuboresha huduma, uchepushaji na wizi wa maji kwa baadhi ya wateja ni moja ya changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo kwa muda mrefu.
Kyejo ameyasema hayo leo Februari 4, 2026, wakati akitoa taarifa ya upatikanaji wa maji kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Morogoro iliyotembelea vyanzo, mtambo wa kusafisha na kusambaza maji katika Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kushuhudia hali ya upatikanaji wa maji katika kipindi cha miaka 49 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kyejo ametaja changamoto nyingine kuwa ni uvamizi wa vyanzo vya maji unaofanywa na watu wanaofanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uchimbaji wa madini.
Akieleza hatua zilizochukuliwa na mamlaka hiyo katika kukabiliana na changamoto hizo, Kyejo amesema ni pamoja na kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa jumuiya za watumiaji wa maji, lakini pia kushirikiana na wenyeviti wa Serikali za Mitaa, hasa katika kutoa taarifa za upotevu wa maji unaosababishwa na mivujo ama wizi unaofanywa na wateja wasiokuwa waaminifu.
Katika hatua nyingine, Kyejo ameeleza hali ya upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Morogoro kuwa kwa sasa kiasi cha maji kwenye vyanzo kimeanza kuridhisha baada ya mvua za hivi karibuni kuanza kunyesha.
“Kabla ya mvua hali ilikuwa hairidhishi. Mkoa wa Morogoro tumekuwa tukipata mvua katika msimu wa vuli zinazoanza Oktoba hadi Desemba, na masika huwa zinaanza Machi hadi Aprili. Sasa kwa mwaka jana hatukupata mvua za kutosha za vuli, badala yake zilinyesha mvua chini ya wastani na hivyo kusababisha kiasi cha maji kwenye mito mikubwa kupungua,” amesema Kyejo.
Amesema kwa mwaka huu mvua wanazotegemea ni za masika, hata hivyo kama mvua hizo zitanyesha chini ya wastani, basi upo uwezekano wa kuingia kwenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Kyejo ametaja mahitaji ya maji katika Manispaa ya Morogoro kwa siku kuwa ni lita za ujazo milioni 81.2, wakati upatikanaji wa maji kwa sasa katika chanzo cha Bwawa la Mindu na vyanzo vingine vidogo ni lita milioni 47 kwa siku.
Hata hivyo, Kyejo ametaja mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi katika Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine wanayoyahudumia kuwa ni pamoja na ukarabati wa mtandao wa mabomba chakavu kutoka kwenye kituo cha kusafisha hadi cha kusambaza maji.
Mkakati mwingine, Kyejo amesema, ni upanuzi wa mabomba ambapo mpaka sasa mabomba yaliyosambazwa ni kilometa 248.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Joseph Masunga ameitaka Moruwasa kuongeza juhudi katika kudhibiti wanaovamia vyanzo vya maji na kuchimba madini, akisema kuwa mbali na kuharibu vyanzo hivyo, pia ni hatari kwa afya za watumiaji wa maji.
“Hawa wanaochimba madini kwenye vyanzo vya maji ukiwauliza wanadai kuwa wanavibali vya uchimbaji. Sasa nataka kujua ni nani anatoa vibali hivi. Nilishatoa taarifa kwa mamlaka mbalimbali lakini mpaka sasa naona bado uchimbaji unaendelea,” amesema Mhandisi Masunga na kuongeza:
“Kamati tunawaagiza Moruwasa kushughulikia upotevu wa maji unaotokana na mivujo, maana kuna maeneo ni korofi kila siku mabomba yanapasuka, na wananchi wamekuwa wakiwalalamikia kuwa wanapotoa taarifa hamchukui hatua za haraka kwenda kuziba mivujo.”
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja amewataka Moruwasa na wadau wengine wa sekta ya maji kushirikiana kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na kuhifadhiwa.
Vilevile, ameiagiza Moruwasa kuhakikisha wanaondoa magugu maji yaliyopo kwenye chanzo cha maji cha Bwawa la Mindu, ambacho kinategemewa na wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa asilimia 75, ili bwawa hilo liweze kuwa salama.