…………
Na Sixmund Begashe, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewataka viongozi na wataalam wa wizara na Taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, kuzingatia uzalendo na manufaa ya nchi kabla ya kusaini mikataba ya uwekezaji katika sekta za uhifadhi na utalii ili kuwawezesha Watanzania kunufaika na Maliasili za Taifa.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo katika kikao chake na wataalam kutoka Mamlaka ya usimamizi ya wanyamapori nchini (TAWA) jijini Dodoma wakati akijengewa uelewa wa kanuni na sheria mbalimbali kuhusu uwekezaji katika sekta ya utalii na uhifadhi.
Mhe. Dkt. Kijaji amesema katika utendaji wake atasimamia maslahi mapana ya wananchi kwa maendeleo ya Taifa na kwamba hakutakuwa na upenyo wa maslahi binafsi katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za Taifa.
Mhe. Waziri ameelekeza maeneo yote yaliyopewa wawekezaji yasimamiwe ipasavyo na kuendelezwa kwa wakati kwa mujibu wa sheria ili kuyafikia matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuacha tabasamu kwa Watanzania kwa kuwanufaisha na rasilimali zao.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji, amekutana na wasimamizi wa Fedha za Maendeleo ya Utalii Tanzania (TDL), kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja wa uendeshwaji wake.
Kikao hicho kimeudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu Bw. Nkoba Mabula, na Menejimenti ya Wizara hiyo.



