BAADA ya kipindi kirefu cha sintofahamu na maswali mengi kutoka kwa mashabiki wa Yanga, hatimaye jina la Clement Mzize limeibuka kwenye msafara wa kikosi hicho kilichosafiri kwenda Morocco kwa ajili ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FAR Rabat.
Uwepo wake kwenye safari hiyo umeibua mijadala kutokana na ukweli kwamba mshambuliaji huyo bado hajacheza mechi yoyote ya ushindani tangu atoke kwenye majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Licha ya kutokuwa tayari kurejea moja kwa moja uwanjani, sababu kubwa ya Mzize kusafiri na timu kwa mujibu wa vyanzo vya Mwanaspoti ni kuendelea kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa jopo la madaktari wa Yanga.
Madaktari hao pia wamesafiri na kikosi, hali inayompa nafasi Mzize kuendelea na programu maalum za kurejea taratibu kwenye ushindani bila hatari ya kukumbana tena na majeraha.
Mbali na suala la afya, uwepo wa Mzize kwenye msafara huo unaweza kuongeza kitu, unajua kwanini? Ni mmoja wa wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kikosi hicho.
Hivyo uwepo wake unaweza kuwa chanzo cha hamasa kwa wachezaji wenzake wakati Yanga ikisaka matokeo kwenye mchezo huo.
Mzize amerejea kwenye kikosi baada ya kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane, akipambana na majeraha ya goti yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji. Kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake na timu, kwani Yanga ilimkosa mmoja wa washambuliaji wake muhimu zaidi.
Jeraha hilo lilitokea Septemba 27, 2025, kwenye mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Benguela ya Angola. Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, lakini ushindi huo uliambatana na janga hilo.
Hali ya Mzize ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kujiunga na majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambako alijitonesha tena jeraha hilo. Tukio hilo lilimlazimu kufanyiwa upasuaji na kuanza safari ndefu ya kurejea kwenye ubora wake wa awali.
Rejea ya Mzize kwenye msafara wa timu inakuja wakati Yanga ikiwa imeimarika zaidi baada ya kufanya maingizo kadhaa mapya katika dirisha la usajili la Januari 2026. Miongoni mwa usajili huo ni Laurindo Aurelio ‘Depu’, mshambuliaji ambaye tayari ameonyesha makali yake kwa kufunga mabao matatu na kutoa asisti moja kwenye mechi mbili Ligi Kuu Bara.
Mbali na Depu, Yanga pia ilimsajili kiungo mshambuliaji Allan Okello, ambaye ameongeza ubunifu na ushindani ndani ya kikosi. Ushindani huo unaifanya Yanga kuwa na machaguo mengi zaidi, jambo linalopunguza presha ya kumrudisha Mzize haraka uwanjani.
Msimu uliopita, Mzize alifunga mabao 14 katika Ligi na matano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akithibitisha thamani yake ndani na nje ya nchi.
Mbali na takwimu hizo, Mzize aliweka historia kubwa barani Afrika baada ya kutwaa tuzo ya Bao Bora la Mwaka Afrika katika tuzo za CAF zilizotolewa mwaka jana nchini Morocco.
Akizungumza wakati wa safari hiyo, kocha mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, aliweka wazi kuwa hawana mpango wa kumharakisha Mzize kurejea uwanjani.
Kocha huyo alieleza kuwa afya ya mchezaji ni kipaumbele kikubwa kuliko presha ya matokeo ya muda mfupi.
Kwa mujibu wa Goncalves, uwepo wa Mzize kwenye kikosi ni sehemu ya mpango wa kumrudisha taratibu bila kumuingiza moja kwa moja kwenye hatari ya majeraha mapya.
Katika mchezo dhidi ya AS FAR Rabat, Yanga itakuwa ikisaka ushindi au angalau sare ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Huu ni mchezo wa presha kwa pande zote mbili.
Kwa sasa, Yanga na FAR Rabat kila moja ina pointi tano katika msimamo wa Kundi B, juu yao kuna Al Ahly inayoongoza msimamo kwa pointi nane. Hali hiyo inaufanya mchezo wa Februari 7, 2026 kuwa wa uamuzi mkubwa kwa hatma ya kundi hilo.
Baada ya mchezo huo, Yanga itahitimisha hatua ya makundi kwa kucheza nyumbani dhidi ya JS Kabylie, ambayo kwa sasa inaburuza mkia ikiwa na pointi mbili tu. Mechi hiyo inatazamwa kuwa na nafasi nzuri kwa Yanga kukamilisha kazi mbele ya mashabiki wao.
Hata hivyo, kwa sasa hesabu za wengi zipo Morocco, ambako sio tu kuangalia matokeo ya uwanjani yatakavyokuwa, pia kwa hali ya Mzize akiwa sehemu ya msafara. Mashabiki wengine wanaona pengine nyota huyo anaweza kuanza kutumika katika mchezo huo japo kwa dakika chache.
