Mkakati wa Katwila mechi 3 za uamuzi Championship

MECHI tatu za mwezi Februari huenda zikatoa picha na ramani ya safari ya Geita Gold kuelekea Ligi Kuu Bara kwani zinaweza kuharibu hesabu na kutibua mipango endapo haitachukua alama zote tisa.

Ndani ya mwezi huo, Geita Gold inayoongoza msimamo wa Ligi ya Championship ikikusanya pointi 40 katika mechi 16, itacheza ugenini Februari 7 kwenye Uwanja wa Filbert Bayi Complex mkoani Pwani, dhidi ya maafande wa Transit Camp walio katika nafasi ya nne kwa alama 33. Katika mchezo wa raundi ya kwanza, timu hizo zilimaliza kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Februari 14 itaikaribisha Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37, kwenye Uwanja wa Nyankumbu, ambapo mchezo wa awali Geita Gold ilipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini.

Katika mchezo wa tatu utakaochezwa Februari 20, Geita Gold itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi kuivaa Polisi Tanzania iliyoko nafasi ya sita ikiwa na alama 27, ambapo katika mchezo wa awali Geita ilishinda nyumbani mabao 2-0.

KATWI 01


Hivyo, kimahesabu mechi hizo ni muhimu kwa Geita Gold kwani inakutana na timu ambazo pia zinawania nafasi ya kwenda Ligi Kuu Bara, ambako kama itaharibu basi itatoa nafasi kwa wapinzani wake kumpita hususan Kagera Sugar iliyoko nafasi ya pili na pointi 39.

KATWI 03


Akizungumzia hesabu za kikosi chake katika michezo hiyo, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila amesema mikakati yao kwa sasa ni namna ya kupata matokeo mazuri ya kubeba alama tatu bila kujali wanacheza soka la kuvutia kiasi gani.

Alikiri kuwa baadhi ya mechi zinawapa tabu katika umiliki wa mchezo kwakuwa wanakutana na wapinzani wagumu, hivyo kilicho muhimu kwao ni kutumia nafasi chache zinazopatikana kufunga mabao na kuondoka na alama zote tatu.

KATWI 02


“Hii ni ligi na ligi ni marathoni lazima uangalie jinsi ya kukusanya pointi na magoli. Kuna mechi tunakutana na ugumu na tunasumbuka kwenye umiliki wa mpira, lakini huwa nawaambia wachezaji wangu wawe na utulivu,” amesema Katwila.

Ameongeza: “Lakini tukikamata mpira tujue jinsi gani ya kutafuta mabao. Sisi tunahitaji matokeo na matokeo ni kushinda mechi na siyo kucheza vizuri.”