Mmiliki Mbeya Kwanza apiga mkwara

MMILIKI wa Mbeya Kwanza, Yusuph Kitumbo, amesema hana mpango wowote wa kuiuza timu hiyo kwa sasa kama inavyodaiwa, baada ya hivi karibuni kuibuka taarifa za Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuanza kufanya mazungumzo ya kina ya kutaka kuinunua.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kitumbo, amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote na zimeandaliwa makusudi na watu wenye nia ovu juu yao, kwa lengo la kutaka kurudisha chini morali ya kikosi hicho kutokana na mwenendo mzuri iliyonayo kwa msimu huu.

“Tunajua kuna watu wanatumika kwa ajili ya kutuvuruga, ila niwaambie ukweli sisi hatutatetereka hata kidogo kwa sababu tumejipanga vya kutosha, malengo yetu ni kurejea Ligi Kuu Bara na wala sio vinginevyo,” amesema Kitumbo.

Katika hatua nyingine, Kitumbo amesema ametumia uwekezaji mkubwa katika kikosi hicho kuanzia benchi la ufundi, wachezaji bora na wenye majina makubwa, hivyo, suala la kuiuza halipo na mashabiki wa timu hiyo waendelee kuisapoti ifanye vizuri.

Kitumbo ameinunua Mbeya Kwanza kutoka kwa aliyekuwa mmiliki wa timu hiyo, Shiraz Batchu, huku akiihamishia mjini Tabora, baada ya msimu uliopita kuweka kambi na kutumia Uwanja wa Ilulu Lindi, katika mechi za nyumbani za Ligi ya Championship.

Katika Ligi ya Championship msimu huu, Mbeya Kwanza iko nafasi ya tatu na pointi 37, baada ya kushinda mechi 12, ikitoka sare mmoja na kupoteza tatu, nyuma ya Kagera Sugar iliyo ya pili kwa pointi 39 na vinara, Geita Gold yenye pointi 40.

Mbeya Kwanza inayotumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kwa sasa katika mechi za nyumbani msimu huu za Championship, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani baada ya kikosi hicho kukusanya jumla ya pointi 25 tu kibindoni.

Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza katika nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.mesema Sabiyanka.