Daruwesh Saliboko avunja ukimya KMC

KIUNGO mshambuliaji wa KMC, Daruwesh Saliboko ametumia siku 86 ambazo ni sawa na miezi miwili na siku 25 kupachika bao lake la tatu na la ushindi kwa timu hiyo ikiichapa Mashujaa 1-0, huku mwenyewe akisema anafanya hivyo kwa wakati sahihi.

KMC juzi iliibuka na ushindi huo ukiwa ni wa pili kati ya mechi 13 ilizocheza za Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo imeambulia sare mbili na vipigo tisa, huku ikifunga mabao manne na kuruhusu 19, ikikusanya pointi nane na imeendelea kukaa mkiani mwa msimamo.

Saliboko hilo ni bao lake la tatu Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo mara ya mwisho kutupia ilikuwa Novemba 9, 2025 dhidi ya Yanga, KMC ikikubali kichapo cha mabao 4-1. Hivyo kuja kufunga tena Februari 3, 2026, ni sawa na siku 86 zimepita ndipo akaja kutikisa nyavu tena.

Ikumbukwe kuwa, nyota huyo ndiye kinara wa mabao kikosini hapo akiwa nayo matatu kati ya manne yaliyofungwa. Jingine limefungwa na Jammy Simba katika sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union.

Wakati KMC ina pointi 8, sita kati ya hizo zimetoka mguuni mwa Saliboko ambaye ameipa ushindi timu hiyo katika mechi mbili ikiwamo ya ufunguzi wa msimu walipoilaza Dodoma Jiji 1-0, akifunga bao pekee la mchezo Septemba 17, 2025. 

Akizungumza na Mwanaspoti, Saliboko amesema kuamini katika kupambania timu kwa kushirikiana na wenzake ndio siri ya hicho anachokifanya huku akisisitiza kuwa hakuna kukata tamaa hadi mwisho wa msimu wanaamini timu yao ina nafasi ya kutoka mkiani.

“Ni kweli inachukua muda mrefu hadi kupata nafasi ya kufunga, sijawahi kukata tamaa naamini katika juhudi na kuamini katika nyakati kwani nyakati sahihi hazijifichi, ndio kama kilichotokea, nimepata nafasi nimeitumia.

“Tunapitia nyakati ngumu kutokana na timu kushindwa kupata matokeo mazuri tukiburuza mkia, hilo halitufanyi tukaikatia tamaa timu, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunaondoka mkiani na msimu ujao tunacheza tena ligi,” amesema.

Saliboko amesema bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki na ushindi walioupata umerudisha morali kwa timu, hivyo wanaamini safari ya matumaini imeanza na  mechi zijazo wataendelea walipoishia.