Spika Zungu awakingia kifua Lugola na Shabiby, ataka uhuru na haki ya Bunge

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu amesema hadi sasa hajapokea barua ya wito kutoka taasisi yoyote wala kutoa kibali cha mbunge yeyote kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Zungu ametoa kauli hiyo bungeni leo Alhamisi Februari 5, 2026 akieleza uamuzi wake unatokana na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mengine kuwa wako baadhi ya wabunge wanatakiwa kuhojiwa.

Kauli ya Spika imekuja ikiwa imepita siku chache tangu iliporipotiwa wabunge Ahmed Shabiby (Gairo) na Kangi Lugola (Mwibara) kwamba wangeitwa na moja ya taasisi kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na michango yao.

Katika michango yao kwenye hotuba ya Rais wakati wa kuzindua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, wabunge hao kwa nyakati tofauti walitaja wizi kukithiri kwa watumishi ambao baadhi wamejificha kwenye kichaka cha uchawa.

Zungu amesema Bunge linaongozwa na Katiba na Kanuni zake, ambazo zinawalinda wabunge kutoa maoni yao kwa uhuru bila shinikizo, hofu, kuhojiwa, kushtakiwa au kikwazo chochote kinachoweza kuathiri uhuru wa mbunge katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.

“Uhuru huo wa wabunge umeainishwa na kulindwa chini ya Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayowapa wabunge kinga ya kisheria kwa maoni na michango wanayoitoa ndani ya Bunge,” amesema Zungu.

Spika amesema endapo itatokea mbunge amekiuka Kanuni za Bunge wakati wa mjadala au michango yake, mamlaka ya kuchukua hatua yapo ndani ya Bunge lenyewe kupitia kiti cha Spika, ikiwemo kufuta mchango husika.

Kwa mujibu wa Zungu, Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2025, hususan Kanuni ya 5, zinaelekeza wazi namna ya kushughulikia ukiukwaji wowote unaotokea ndani ya Bunge, bila kuingilia uhuru wa mbunge au kuvunja misingi ya kinga ya kibunge.

Amesisitiza Bunge litaendelea kulinda uhuru wa wabunge wa kuchangia masuala ya Kitaifa kwa uwazi na ujasiri, huku likihakikisha mjadala unafuata kanuni, heshima na misingi ya kikatiba.

Kabla ya kauli ya Spika leo, wabunge Mwita Waitara (Tarime Vijijini) na Festo Sanga (Makete) kwa nyakati tofauti walilaani kitendo cha kuitwa ili wahojiwe wabunge hao kwamba kingeingilia uhuru na hadhi ya kibunge.