Zamu ya Kibu Denis kusepa Simba, Waarabu wamwaga mpunga

Muda wowote kuanzia sasa, Simba itakamilisha makubaliano ya kumuuza mshambuliaji Kibu Denis kwenda Al Nasr ya Libya.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeithibitishia Mwananchi Digital kuwa mshambuliaji huyo anajiandaa kukamilisha mchakato wa kujiunga na miamba hiyo ya Libya.

“Kibu anaenda Libya. Klabu imeshafikia makubaliano ya kumuuza na kuna mambo machache tu yamesalia ili uhamisho huo ukamilike,” kimefichua chanzo hicho.

Winga wa Simba, Kibu Denis, akishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-0 kwenye mechi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs, Oktoba 19, 2025. Picha na Mtandao



Hii ni mara ya pili kwa Al Nasr kumhitaji Kibu kwani mara ya kwanza ilikuwa katika dirisha kubwa la usajili kabla ya kuanza kwa msimu huu ambapo nia yao haikufanikiwa.

Lakini awamu hii Al Nasr wameonekana kuja na nguvu mpya ambayo imewafanya wafanikiwe kumuachia Kibu ili kukwepa nyota huyo kuondoka bure baada ya msimu kumalizika.

Ifahamike kwamba mkataba wa Simba na Kibu Denis utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu hivyo klabu hiyo imeonekana haiko tayari kuziachia noti za Walibya hao kwa sasa.

Ndani ya Al Nasr, Kibu atakutana na nyota wawili aliocheza nao Simba hivi karibuni ambao ni kiungo Fabrice Ngoma na mshambuliaji Steven Mukwala.

Kibu kwa sasa yupo Angola na kikosi cha Simba ambacho Jumamosi kitakuwa na mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Luanda.

Winga wa Simba, Kibu Denis, akimpiga chenga aliekuwa beki wa Stellenbosch na sasa Mamelodi Sundowns, Fawaaz Basadien katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, Aprili 20, 2025. Picha na Mtandao



Al Nasr inaongoza msimamo wa kundi namba nne la Ligi Kuu ya Libya ikiwa na pointi 21 ilizokusanya baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zote saba ilizocheza.

Msimu huu Kibu Denis ameifungia Simba mabao mawili yote yakiwa ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao hayo aliyafunga katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.