Serikali kurejesha betri 474 za taa za barabarani Moshi

Moshi. Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, imeanza mpango wa kurejesha betri zaidi ya 474 za taa za barabarani zilizoharibiwa na kuibiwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Moshi kwa nyakati tofauti.

Wizi wa betri hizo umesababisha taa nyingi kushindwa kufanya kazi, hali inayohatarisha usalama wa wananchi wanaotumia barabara hizo nyakati za usiku, hususan katika maeneo ya Bonite, Bomambuzi, Shanti Town na maeneo mengine ya manispaa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 5, 2026, Meneja wa Tarura Wilaya ya Moshi, Godfrey Mbena, amesema Serikali imetenga bajeti ya Sh300 milioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kurejesha taa hizo.

Baadhi ya taa za barabarani ambazo zimeharibiwa katika Manispaa ya Moshi.



“Kuanzia bajeti ya mwaka 2026/27 tumetenga Sh300 milioni kwa ajili ya kufanya marekebisho ya taa za barabarani zilizoharibiwa, ikiwemo kununua betri mpya na kuboresha mifumo ya ulinzi,” amesema Mbena.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha taa za barabarani zinafanya kazi ipasavyo na kupunguza vitendo vya wizi vinavyoikosesha Serikali fedha nyingi.

Mbena amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya umma kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini vitendo vya wizi au uharibifu wa taa hizo.

Aidha, amesema Tarura itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama wilayani humo ili kudhibiti vitendo vya wizi wa miundombinu ya taa za barabarani, ambavyo vimekuwa vikijirudia mara kwa mara.

Baadhi ya taa za barabarani ambazo zimeharibiwa katika Manispaa ya Moshi.



Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi wamesema uharibifu wa miundombinu hiyo umekuwa kero isiyoisha, kwani taa hizo huwekwa na kuibiwa mara kwa mara.

Mkazi wa manispaa hiyo, Devota Shaka amesema kukosekana kwa taa za barabarani kumeongeza hofu kwa wananchi wanaotumia barabara hizo nyakati za usiku kutokana na kuongezeka kwa matukio ya uhalifu.

“Hizi taa zimekuwa zikiharibiwa na kuibiwa mara kwa mara. Serikali iangalie namna bora ya kuweka betri hizo ili kuzuia wezi kupata mwanya wa kuziiba,” amesema.

Naye Joshua Adam, mkazi wa Moshi, amesema maeneo yenye taa hizo yanapaswa kuwekewa ulinzi hasa nyakati za usiku, akieleza kuwa Serikali inapoteza fedha nyingi kwa kuzirejesha mara kwa mara.