Mafaili ya Epstein ni jehanamu ya Trump na wenzake?

Matajiri wakubwa wa ulimwengu, wanasiasa wenye nguvu kubwa ya ushawishi na wanaoweza kutengeneza matokeo, maji hayashuki, chakula hakiteremki. Sababu ni hatima ya yaliyomo ndani ya Mafaili ya Epstein.

Rais wa Marekani, Donald Trump, ni mmoja wa watajwa kwenye maudhui ya Mafaili ya Epstein.
Katika kampeni za urais za mwaka 2024, Trump aliahidi kuwa angeyaacha wazi Mafaili ya Epstein kama angeshinda. Kumbe alikuwa akijikaanga kwa mafuta yake mwenyewe.

Rais wa Marekani, Donald Trump



Baada ya kushinda kiti, Trump alipuuzia ahadi yake ya Mafaili ya Epstein, akidai kuwa hoja tajwa ni uzushi wa chama pinzani cha Democratic, ikichochewa na mahasimu wake Joe Biden, Barack Obama na Hillary Clinton.

Mafaili ya Epstein ni nyaraka zenye kurasa milioni sita, picha mnato, video na barua pepe, vikibeba ushahidi wa matukio ya uhalifu wa kingono dhidi ya watoto, uliotekelezwa na mhalifu wa ngono, Jeffrey Epstein, na wenzake.

Epstein alifariki dunia Agosti 10, 2019, akiwa kwenye jela maalum ndani ya Gereza la Metropolitan Correction Center (MCC), New York, Marekani.

Ripoti ya kitabibu ilieleza kuwa alijiua. Mazingira ya kifo chake yalitengeneza wasiwasi mkubwa kwamba aliuawa kwa lengo la kuficha siri za wakubwa.

Epstein ni mzawa wa Brooklyn, New York, Marekani. Wazazi wake, Seymour George Epstein (baba) na Pauline “Paula” Stolofsky (mama), ni Wayahudi waliohamia Marekani. Epstein alikuwa kaka mkubwa katika uzao wa watoto watatu.

Mkusanyiko wa taarifa za Epstein unampambanua Mmarekani-Myahudi huyo kuwa tapeli wa kimataifa na mhalifu wa ngono. Aliwatumikisha watoto kingono, alifanya usafirishaji wa binadamu na aliwaunganisha watu na watoto kingono.

Jeffrey Epstein



Kwa miaka mingi, hasa baada ya kifo chake, kumekuwa na uvumi mkubwa kwamba Epstein alitunza ushahidi wa kila mteja wake aliyemuunganisha kushiriki ngono na watoto.
Wateja wake walikuwa watu wazito, matajiri wakubwa na wanasiasa mashuhuri.

Uvumi huo ndiyo uliojenga dhana katika jamii kwamba Epstein aliuawa mahabusu Agosti 2019 ili kuficha siri za watu wasioguswa (untouchables).
Tangu wakati huo, kumekuwa na shinikizo la Mafaili ya Epstein kuachwa wazi mbele ya macho na masikio ya umma.

Ripoti za maisha yake ya mwanzo zinamtaja Epstein kama mtu mwenye akili, aliyefanya vizuri kwenye somo la Hisabati na mwenye kipaji cha muziki.
Alijifunza na kuwa hodari wa kucheza piano. Muziki hakuupa nafasi, ila Hisabati ilimfikisha mbali, ingawa si kwa njia halali.

Alianza kusoma katika shule ya chipukizi ya Mark Twain, inayosimamiwa na Idara ya Elimu ya Jiji la New York (NYCDOE).
Kutokana na uwezo wake wa kunasa masomo haraka, Epstein alikuwa akilipwa na wanafunzi wenzake ili awafundishe kwa muda wa ziada.

Mwaka 1967, Epstein alijiunga na Kituo cha Sanaa cha Interlochen kwa ajili ya kujinoa zaidi kimuziki.
Mwaka 1969, alihitimu elimu ya juu katika Shule ya Lafayette, iliyopo Brooklyn, New York.
Mwaka 1971, alijiunga na Chuo cha Cooper Union, Manhattan, kusoma Hisabati, lakini alisoma kwa miezi michache tu.

Septemba 1971, Epstein alidahiliwa katika Taasisi ya Sayansi ya Hisabati ya Courant, Chuo Kikuu cha New York.
Juni 1974, aliacha chuo kabla ya kuhitimu shahada yake. Baada ya hapo alianza kazi ya ualimu.

Shule aliyojiunga nayo kama mwalimu ni Dalton, iliyopo Manhattan, New York.
Ni katika kipindi hiki cha ualimu ambapo alianza kuonesha tabia zisizofaa kwa watoto wa kike. Alipenda kujenga nao ukaribu na alihudhuria matukio ya sherehe zao, hasa zile zilizokuwa na pombe.

Dalton ni shule ambayo watoto wawili wa Alan Greenberg walikuwa wakisoma. Greenberg alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi kubwa ya kifedha ya Bear Stearns.
Mtoto wa kike wa Greenberg ndiye aliyemtambulisha Epstein kwa baba yake, na hapo Greenberg na Epstein wakawa marafiki.

Mwaka 1976, Epstein aliachishwa kazi Dalton. Moja kwa moja, Greenberg alimwajiri Bear Stearns kama mfanyakazi wa chini. Uwezo wake kazini ulimfanya apande ngazi hadi kuwa mshauri wa matajiri waliotumia benki hiyo.

Mwaka 1981, alipoondoka Bear Stearns, Epstein alianzisha kampuni yake ya ushauri wa masuala ya kifedha na uhalifu wa kifedha, Intercontinental Assets Group Inc. (IAG).
Ni kipindi hiki alipata utajiri wa haraka kwa njia nyingi za udanganyifu.

Kupitia IAG, Epstein aliweza kujenga ukaribu na matajiri pamoja na wanasiasa maarufu. Alijipambanua kama mshauri wa masuala ya kifedha wa Serikali ya Marekani na matajiri binafsi.

Aliinadi kampuni yake kuwa na uwezo wa kuokoa fedha zilizoibiwa kitapeli. Ana Obregón, nyota wa filamu mzawa wa Madrid, Hispania, ni mmoja wa wateja matajiri wa Epstein.
Mwaka 1982, Epstein alimsaidia baba yake Ana kuokoa mamilioni ya dola kutokana na hati fungani zake katika taasisi ya Drysdale Securities, ambayo ilifiliska mwaka huo huo.

Mara, Epstein akaanza kusafiri mara kwa mara kati ya Marekani, Ulaya na Mashariki ya Kati.
Katika kipindi hiki, alijitambulisha kama ofisa wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA). Inadaiwa pia kuwa alifanya kazi na Idara ya Intelijensia ya Uingereza na alikuwa akitumia hati ya kusafiria ya Australia.

Epstein alishirikiana pia na mhalifu mwingine wa kimataifa, Steven Hoffenberg, aliyekuwa anaendesha mtandao wa kitapeli uitwao Towers Financial Corporation (TFC).
Uhusiano wake na matajiri pamoja na wanasiasa wakubwa ulimfanya Epstein asiweze kuguswa na yeyote.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, Epstein alianzisha kampuni aliyoiita J. Epstein & Company, ambayo alisema ilisimamia mali za wateja wenye utajiri unaozidi dola bilioni moja.
Mwaka 1996, alibadili jina la kampuni hiyo na kuiita Financial Trust Company (FTC).

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, kati ya mwaka 1999 na 2008, FTC na kampuni nyingine ya Epstein, Southern Trust Company (STC), ziliingiza mapato ya dola milioni 800, mengi yakitokana na kazi za mabilionea Leslie Wexner na Leon Black.

Kisiwa cha Mtakatifu Thomas, ndani ya Visiwa vya Virgin, kina mengi kuhusu Epstein. Alikitumia kukwepa kodi na kuanzisha makazi ambako alikuwa akifanya hafla mbalimbali na kuwaalika watu maarufu, wengi wao matajiri wakubwa na wanasiasa.

Wasichana wadogo walisafirishwa hadi kisiwani na kutumikishwa kingono na Epstein mwenyewe, huku wageni wake wakikirimiwa masaji ya ngono. Kila kilichofanyika kisiwani humo kilirekodiwa.

Kasri lake la Palm Beach, Florida, nalo alilitumia kufanya hafla zenye nakshi za ngono na watoto wadogo wa kike. Epstein pia angeweza kucheza ngono na watoto hao mbele ya wageni wake.

Inadaiwa kuwa matajiri na wanasiasa waliokubali “ofa” za Epstein walirekodiwa kwa video na picha mnato bila wao kujua.
Makasri ya Epstein yalifungwa kamera za siri kuhakikisha kila kilichofanyika ndani kinarekodiwa.

Polisi walipopekua nyumba ya Palm Beach mwaka 2006, walibaini kamera mbili za siri. Kasri lingine la Epstein, lililopo New York, nalo lilibainika kuwa na kamera nyingi.

Nadharia ni kwamba watu wengi mashuhuri walirekodiwa na Epstein katika matukio machafu na watoto wa kike.
Video na picha mnato hizo alizitumia kuwatisha wateja wake—kwanza kujitajirisha, pili kuwalazimisha wanasiasa kumpa ulinzi wa vitendo vyake vya kihalifu.

Katika kufanikisha mtandao huo, kuanzia kutafuta watoto wa kike hadi kurekodi wateja, Epstein alishirikiana na mpenzi wake, Ghislaine Maxwell, raia wa Uingereza. Kwa sasa, Maxwell anatumikia kifungo cha miaka 20 katika Gereza la Bryan, Texas, baada ya kukutwa na hatia ya usafirishaji wa binadamu na kuwatumikisha watoto kingono.

Shinikizo la Mafaili ya Epstein linatokana na majina makubwa yanayoaminika kuwamo, akiwemo Trump, aliyewahi kuwa rafiki wa Epstein. Ikumbukwe, Epstein alifariki dunia wakati Trump akiwa madarakani katika muhula wake wa kwanza.

Watu wa karibu na Epstein wamekumbwa na kashfa na mashitaka. Bilionea Leon Black, mwaka 2021, alifikishwa mahakamani kwa kesi ya ubakaji. Mlalamikaji, Cheri Pierson, alisema Black alimbaka mwaka 2002 katika kasri la Epstein, New York.

Kesi nyingine dhidi ya Black ilifunguliwa Julai 25, 2025, ikidaiwa alimbaka binti wa miaka 16 mwenye utindio wa ubongo mwaka 2002, ndani ya jumba la Epstein, Manhattan.

Februari 19, 2022, mshirika wa Epstein, Jean-Luc Didier Henri Brunel, alikutwa amejiua katika Gereza la La Santé, Paris, Ufaransa, alipokuwa akikabiliwa na makosa ya ubakaji. Brunel alikuwa gwiji wa mitindo aliyekamatwa Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle akijaribu kutorokea Dakar, Senegal.

Novemba 19, 2025, Bunge la Marekani (Congress) lilipitisha sheria iitwayo Epstein Files Transparency Act, iliyomtaka Mwanasheria Mkuu kuweka hadharani nyaraka zote ndani ya siku 30 tangu kusainiwa.

Congress walichukua hatua hiyo baada ya kuona uongozi wa Trump ulikuwa ukipiga danadana. Januari 30, 2026, kurasa milioni tatu, picha 180,000, video 2,000 na barua pepe ziliachiwa. Ndani ya mafaili hayo, Trump alitajwa, pamoja na Elon Musk, Bill Gates, Richard Branson, Mwanamfalme Andrew Mountbatten-Windsor na Steve Bannon.

Waziri wa Fedha wa zamani wa Marekani, Larry Summers; Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak; na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ni miongoni mwa majina yaliyomo. Hata hivyo, kurasa milioni 3.5 bado hazijaachwa wazi.

Hofu kwa Trump na wengine ni je, watatajwa kuhusika na uhalifu wa kingono dhidi ya watoto? Vyovyote iwavyo, kwa sasa Trump na wenzake, kila wanaposikia habari za Mafaili ya Epstein, ni kama kusikia simulizi za jehanamu.