Watu wasioweza kugharamia matibabu ya NCDs kutambuliwa

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiadhimisha siku 100 za uongozi, wananchi wanajiuliza kuwa, mpango wa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) nini mwelekeo wake?

Changamoto kubwa ya vifo vinavyosababishwa na kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya figo, saratani na magonjwa ya moyo bado inakabiliwa na upungufu wa fedha na uwazi.

Agosti 28, 2025 katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu za Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa chama hicho aliyekuwa mgombea urais Samia, alitaja mambo 10 atakayoyatekeleza ndani ya siku 100 za urais wake, iwapo atachaguliwa kuendelea kuongoza Tanzania, ikiwamo kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza.

Novemba 3, 2025, Samia aliapishwa kuwa Rais na Februari 11, 2026 atafikisha siku 100 madarakani.

Aliahidi Serikali itaanza kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo kwa magonjwa ya saratani, figo, moyo, sukari, mifupa na mishipa ya fahamu.

Februari 2, 2026 Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa alizindua rasmi mashine ya PET Scan inayotumika katika uchunguzi wa Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kuwepo kwa mashine hiyo kutapunguza gharama za matibabu kwa wananchi kwenda nje ya nchi hususan India.



“Haya ndiyo magonjwa yenye gharama kubwa ambayo wananchi wasio na uwezo wamekuwa wakishindwa kumudu gharama zake na Serikali itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000 ndani ya siku 100, wakiwamo wauguzi na wakunga,” aliahidi Samia.

Hivi sasa ni muhimu kufahamu mwelekeo kama nchi ni kiasi gani cha fedha kimetengwa, kinaenda wapi na je, wananchi wanaona matokeo yake?

Akizungumza Februari 2, 2026 katika kikao kazi cha wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa alisema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa kushughulikia magonjwa hayo sambamba na kuhakikisha wagonjwa wasio na uwezo wanapata huduma za afya bila kikwazo fedha pale wanapozihitaji.

“Huu ni ujumbe wa ukombozi wa kisasa. Taifa linalowekeza kwenye ubingwa na ubobezi, linaamua kwamba maisha ya raia wake hayataamuliwa na bahati au umbali. Na Taifa linalosema wagonjwa wasio na uwezo wapate huduma bila kikwazo cha fedha, linatoa tamko la maadili,” alisema Mchengerwa.

“Tiba ya ubingwa si anasa, ni hadhi ya Taifa. Kumkinga asiye na uwezo si hisani bali ni wajibu wa dola yenye utu.”

Akifafanua zaidi hatua hizo, Mkurugenzi wa Sera, Tafiti na Ubunifu kutoka Wizara ya Afya, Dk Tumainiel Macha amesema ndani ya siku 100 Serikali imeandaa mwongozo wa kutambua wasio na uwezo kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu, Ofisi ya Waziri Mkuu, wenye Ulemavu, Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Amesema baada ya hapo, mwongozo utatuma vyombo husika kufanya uhakiki, kisha watalipiwa na Serikali bima ya kitita cha msingi Sh150,000.

“Miongoni mwao watakaougua magonjwa yasiyoambukiza, sheria imetengeneza mfuko maalumu wa kugharamia wasio na uwezo katika tiba za ubingwa na ubingwa bobezi.

“Kwa sasa mfumo umetenga bilioni 41 kuwasajili wasio na uwezo kuwagharamia, asilimia 14 ya fedha zinazoingia pale lazima ziingie kugharamia wasio na uwezo, bilioni 6.7 zimeshatengwa pale kugharamia watakaohitaji upasuaji wa moyo, dialysis, nyonga na hiyo ni nje ya bajeti ya Serikali,” amesema.

Dk Macha amesema ili mgonjwa aweze kupata matibabu anatakiwa kufuata mfumo wa rufaa, kwa kuanza na zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya, rufaa mkoa, kanda mpaka hospitali ya Taifa.

“Hazina wameshatoa bilioni 6.7 iko mkononi, lakini kwenye bajeti yetu ya Serikali kuna bilioni 9 itaendelea kusaidia wasio na uwezo, Serikali imedhamiria katika hili, hakuna mgonjwa ambaye ameachwa asiye na uwezo,” amesema.

Alipoulizwa nafasi ya wale ambao hawatakuwa katika makundi ya msamaha wa matibabu, Dk Macha amesema sera ya afya inamtaka mwananchi yeyote apewe huduma za matibabu awe ana hela au hana.

“Leo mgonjwa akitakiwa kufanyiwa matibaba ya nyonga milioni 18 ukafika MOI una uwezo wa kuchangia milioni 9 au 5 sera ya afya inaitaka Serikali ile sehemu iliyobakia ilipie na hata kwa mtu mwenye bima, ikiwa kiwango cha matibabu kinavuka ile bima yake, Serikali inatakiwa kumchangia huyu mgonjwa,” amefafanua akisema msamaha huo hutolewa kisera.

Februari 2, 2026 Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa alizindua rasmi mashine ya PET Scan inayotumika katika uchunguzi wa Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kuwepo kwa mashine hiyo kutapunguza gharama za matibabu kwa wananchi kwenda nje ya nchi hususan India.



Dk Macha amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kugharamia magonjwa yasiyoambukiza kwa kuweka mashine mbalimbali za dialysis katika kila hospitali ya mkoa, kuanzisha matibabu ya saratani katika hospitali zote za kanda na kufunga mashine za mionzi na kutoa elimu kwa umma.

Amesema mashine za CT- Scan zimefungwa katika hospitali za rufaa ili kurahisisha ugunduzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kusomesha wataalamu wa ubingwa na ubingwa bobezi kupitia Samia Fund.

Hatua hiyo imeungwa mkono na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kikisema ni hatua kubwa kwa nchi kuanza kusaidia wananchi walioshindwa kumudu gharama za matibabu.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko ametoa pongezi akiita ni utashi wa Serikali iliyopo madarakani, hasa ujio wa mpango wa bima ya afya kwa wote ambao unakwenda kubadilisha mfumo wan chi.

“Bado hatujashuhudia kwa macho utoaji wa huduma kwa mwananchi hata mmoja, tutafurahi kuona utekelezaji wa vitendo zaidi ya matamko, tunaomba utekelezaji uongezeke ili matarajio na maono ya Rais iwe ndoto iliyotimia,” amesema.

Kufuatia hatua hiyo, wananchi mbalimbali wametoa maoni yao, huku wakionesha kuwa na matumaini makubwa katika hatma yao kiafya.

Wanandoa bibi na bwana, Samweli James wakazi wa Mawelewele, Iringa, wamethibitisha kuwa wamejiandikisha katika ofisi za kata kwa ajili ya mchakato wa msamaha wa matibabu. Kwa upande wa wazee, wanasubiri majibu ya maombi yao.

Ivan Njako (37) mkazi wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Kata ya Luhota, amesema anasubiri kwa hamu kuanza kwa mchakato wa msamaha wa gharama za matibabu, kwani yeye ni miongoni mwa wanufaika wanaotarajiwa, hupata huduma ya dialysis mara mbili kwa wiki tangu mwezi wa sita mwaka jana.

“Hospitali wamesema kwa sasa ninaweza kupatiwa msamaha wa dawa pamoja na huduma ya kumuona daktari, lakini huduma ya dialysis bado naendelea kujigharamia mwenyewe kwa msaada wa ndugu na watu mbalimbali,” amesema Ivan.

Yondo Mlula (50) mkazi wa Kitayawa, Iringa vijijini amesema katika kijiji chao, mchakato unaoendelea kwa sasa unahusu msamaha wa matibabu na vipimo kwa wagonjwa wenye umri wa miaka 15 na chini, pamoja na wazee wa miaka 60 na kuendelea.

 Aidha, wametangaziwa kuwa usajili wa kaya maskini utaanza hivi karibuni.