Tanga. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameitaka jamii kuendelea kusimamia maadili ya vijana kwa misingi ya dini, sambamba na kuhakikisha wanapata elimu bora, kama sehemu ya kutimiza wajibu kwa kizazi kijacho.
Hemed ametoa kauli hiyo usiku wa Februari 4, 2026, alipokuwa akihutubia viongozi wa kisiasa, Serikali, dini na maelfu ya waumini wa Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga, waliohudhuria kilele cha Maulid Jumuiya kilichofanyika wilayani Pangani.
Akizungumza katika hafla hiyo, amesema wazazi na walezi wana wajibu wa kuwalea vijana katika misingi ya maadili, heshima na ucha Mungu ili wawe raia wema na wenye mchango chanya kwa jamii.
“Tuhakikishe tunatimiza wajibu wetu kwa vijana wetu. Mambo ya heri ni ya kuyakimbilia leo ili kujenga kesho iliyo bora,” amesema Hemed.
Amewashukuru viongozi wa dini na wa kisiasa waliojitokeza kushiriki tukio hilo, akiwataka kuendeleza mshikamano, amani na upendo miongoni mwa jamii kwa kuzingatia maelekezo ya Qurani inayoramrisha matendo mema na kukataza mabaya.
Aidha, aliwaongoza waumini kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, akisema anaamini dua hizo zitapokelewa na Mwenyezi Mungu na kuleta baraka kwa taifa.
Katika hatua nyingine, Hemed alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman Abdallah, kwa kufanikisha maandalizi ya kilele cha Maulid Jumuiya, kilichowakutanisha waumini na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso, amepongeza jitihada za Serikali katika utekelezaji wa mradi wa barabara ya Tanga–Pangani–Saadani hadi Bagamoyo, akisema utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi.
“Barabara hii ni neema kubwa kwetu. Itafungua fursa za biashara, utalii na ajira kwa wananchi wa Pangani na maeneo ya jirani,” amesema Aweso.
Aweso pia ameeleza mafanikio katika sekta ya uvuvi kwa kupatikana kwa maboti na vifaa vya kisasa, pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Pangani hadi Korogwe, wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 175.
Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha usafiri wa boti za mwendokasi kati ya Pangani na Zanzibar ili kurahisisha usafiri na kukuza uchumi wa pande zote mbili.
“Sisi Pangani tuko karibu sana na Zanzibar. Kufunguliwa kwa usafiri wa haraka kutaimarisha uhusiano wa kiuchumi, kijamii na kiutalii,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman Abdallah, alisema kufanyika kwa tukio hilo wilayani Pangani ni heshima kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, akibainisha kuwa ni mara chache wilaya hiyo kupata fursa ya kutembelewa na viongozi wakuu wa kitaifa katika shughuli za kidini.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wote wa dini kwa kushiriki nasi. Hili ni jambo la kujivunia na la kumshukuru Mwenyezi Mungu,” amesema.