Miaka 49 iliyopita, siku kama ya leo, kilizaliwa chama kipya; Chama cha Mapinduzi (CCM). Ulikuwa uamuzi baada ya tafakuri ya kina, kujiuliza na kujijibu, kisha vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) vilivunjwa na kuzaliwa CCM.
Februari 5, 1977 ilikuwa Jumamosi. Wenyeviti wawili, Mwalimu Julius Nyerere (TANU) na Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi (ASP), waliachana na vyama vyao.
Mwalimu Nyerere akawa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Jumbe Makamu Mwenyekiti wa kwanza. Pius Msekwa, Katibu Mtendaji wa kwanza.
Cheo cha Katibu Mtendaji kilifutwa na kuwa Katibu Mkuu. Ni mabadiliko ndani ya miaka 49.
Umesalia mwaka mmoja chama kitimize nusu karne. Siku 17,897 ndiyo umri wa CCM, kama utataka kuiweka hesabu yako kwa tarakimu za mawio na machweo.
Miaka 49 ya CCM unaweza kuigawa katika makundi mawili kisiasa.
Miaka 15 (1977–1992), chama hicho kikiongoza dola na kufanya uchaguzi bila ushindani. Miaka 34 (1992–2026), chama kikipambana na vyama vingine kushinda dola.
Hesabu hiyo inaonesha kuwa CCM kimeishi ndani ya mfumo wa vyama vingi kwa muda mrefu kuliko kilivyokuwa peke yake.
Chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu mara tatu kilipokuwa peke yake na mara saba kikichuana na vyama vingine.
Ni siku 17,897 za machozi, jasho, damu na tabasamu. Ushindi wa jasho katika vipindi vya mchuano mkali. Nyakati za damu kumwagika, misiba iliyotengeneza machozi, vilevile tabasamu, maana dola bado wanayo na nchi inapiga hatua. Tanzania ya mwaka 2026 imepiga hatua kubwa kimaendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 1977.
Hatusahau hadithi ilipoanza
TANU ilipigania uhuru wa Tanganyika na kuupata Desemba 9, 1961; ASP ikaongoza Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964. Kisha, TANU na ASP kwa pamoja vikaongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Aprili 26, 1964 hadi Februari 5, 1977, CCM ilipozaliwa.
Kutoka Februari 5, 1977 hadi Februari 5, 2026 ni miaka 49 (umri wa CCM). TANU na ASP vimewahi kuwa vyama vya upinzani kabla ya uhuru.
Ni upinzani wa nyakati za ukoloni. CCM tangu kuzaliwa kwake hakijawahi kuonja ladha ya kuwa chama cha upinzani.
Hiyo ndiyo ladha kubwa ya kisiasa ambayo CCM hawajawahi kuonja. Hata wazazi wake, ASP na TANU, hawakuwahi kuonja ladha ya kuwa chama cha upinzani dhidi ya chama tawala ndani ya mipaka ya nchi huru.
CCM kilizaliwa kipindi Tanzania, Kenya na Uganda zikiunda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kisha jumuiya hiyo ilivunjika na kurejea tena wakati CCM ikiongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na sasa Afrika Mashariki ni jumuiya ya nchi nane: Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Somalia.
CCM ikiwa madarakani, nchi ilipigana Vita ya Kagera dhidi ya Uganda. Damu ilimwagika. Ikafiwa na Waziri Mkuu Edward Sokoine mwaka 1984. Makamu wa Rais, Dk Omar Ali Juma, mwaka 2001. Na taifa likaondokewa na rais aliyekuwa madarakani, Dk John Magufuli, mwaka jana. Ni nyakati za machozi.
CCM wakaridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa, wakaingia kwenye siasa za ushindani ndani na nje. Machafuko ya kisiasa Januari 26 na 27, 2001 yalifanya nchi izalishe wakimbizi kwenda Kenya mpaka Somalia. Damu ilimwagika. Kisha mwafaka wa CCM na CUF mwaka 2001 ukarejesha tabasamu la kitaifa.
Uchaguzi Mkuu wa 2025, nchi ilikumbwa na majaribu mazito. Watu waliingia barabarani; baadhi walipoteza maisha na wengine wameachwa na ulemavu wa viungo.
CCM imeweza kuvuka mtihani huo mgumu, lakini hali ya nchi haijakaa sawa.
Kulikuwa na jaribio la mapinduzi mwaka 1983 lililolenga kumwondoa Mwalimu Nyerere madarakani; CCM ilivuka.
Miaka 49 ni siku 17,897 za ushindi dhidi ya majaribu mengi.
Uchaguzi Mkuu wa 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020 umewezesha CCM kujionea ladha tofauti ya upinzani.
Joto la mwaka 1995 lilikuwa kali walipomkabili Augustino Lyatonga Mrema (NCCR-Mageuzi), vilevile upinzani mwepesi dhidi ya Profesa Ibrahim Lipumba mwaka 2000 na 2005 (CUF).
Upinzani mkali dhidi ya Dk Willibrod Slaa (2010) akiwa CHADEMA na Edward Lowassa (2015) chini ya CHADEMA na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Vilevile kuna uchaguzi wenye tafsiri ngumu wa mwaka 2020. Mwaka 1995 na 2015, CCM walishinda baada ya kuvuja jasho jingi.
Mwaka 2022, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alijiuzulu, kisha chama kikaendesha mchakato wa kumpata spika mpya, Dk Tulia Ackson.
Ni tafsiri kuwa ndani ya miaka 49, kimekuwa chama chenye kukabiliana na vishindo pamoja na hekaheka za kisiasa na kuvuka salama.
Chama kimefiwa na wenyeviti wastaafu: Mwalimu Julius Nyerere (Mwenyekiti wa kwanza), Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti wa pili) na Benjamin Mkapa (Mwenyekiti wa tatu). Pia kimefiwa na rais aliyekuwa madarakani aliyetokana na chama hicho, Dk John Magufuli.
Hivyo, CCM iliyoonja ladha nyingi za kisiasa imeendelea kufuta machozi na kusonga mbele.
Hata kabla ya CCM kuzaliwa, enzi za TANU na ASP, aliuawa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Amani Karume.
Mwaka 1984, Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumbe, alilazimishwa kujiuzulu nyadhifa zake zote.
Mwaka 2021, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, alifariki dunia.
Ikumbukwe pia Seif, akiwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alifukuzwa uanachama wa CCM kisha akafungwa.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Februari 2008 alilazimika kujiuzulu kwa kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa dharura kati ya TANESCO na Kampuni ya Richmond.
Kwa uamuzi huo, Baraza la Mawaziri likavunjwa.
Kipindi CCM wakiwa madarakani kimeshuhudia serikali ikivunjika mara kwa mara.
Kushiriki migogoro ya kisiasa nchi za nje, hususan ndani ya Bara la Afrika, na kusaidia utatuzi, imekuwa sehemu ya utaratibu wa CCM.
Karibu ladha zote za kisiasa CCM wameshaonja. Bado ladha moja ambayo ni ngumu mno; ni wao kuwa chama cha upinzani ili wengine washike dola.
Je, inawezekana hivi karibuni au itabidi kusubiri sana?
Kwa Afrika, CCM ndiyo chama kinachoendelea kuongoza dola hata baada ya kupita miongo minne na kenda madarakani, na sasa umebaki mwaka mmoja miongo mitano kamili ikamilike.
Kuendelea kuongoza dola kunategemea uimara wake. Ikiwa CCM watamudu kuwafanya wapinzani wao kuwa dhaifu, basi nafasi ya kubaki kwenye usukani wa uongozi kwa miaka mingi ijayo ni kubwa. Wakilegea, watakuwa wapinzani.
Wakati huohuo, CCM wanakabiliwa na mtihani mgumu wa kulinda wanachama wao ili wasigeuke wapinzani.
Alipata kusema Mwalimu Nyerere kuwa upinzani imara utatoka ndani ya CCM.
Mwaka 1995, CCM walipata wakati mgumu kumdhibiti aliyekuwa mwanachama wao, Mrema; vilevile mwaka 2015, Lowassa, ambaye alifikia wadhifa wa Waziri Mkuu lakini alihamia CHADEMA na kuitikisa CCM.