Shinyanga. Katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) imebaini kwamba changamoto kubwa inayokabili mfumo huo ni udahili hafifu pamoja na ucheleweshwaji wa matokeo.
Hayo yamebainishwa leo Februari 5, 2026 na Meneja wa Utahini na Utunuku wa Nactvet, Dk Obeid Mahenya, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Nactvet, wakati wa mafunzo maalumu kwa maofisa udahili na maofisa mitihani kutoka katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini Tanzania katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha ufanisi wa mifumo ya udahili na mitihani katika vyuo pamoja na kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji.
Dk Mahenya amesema mafunzo yanayotolewa kwa maofisa udahili yataimarisha ufanisi wa mifumo ya udahili na mitihani katika vyuo.
“Kuwepo kwa changamoto za udahili hafifu unaonekana katika kanzidata ya baraza pamoja na ucheleweshaji wa upakiaji wa matokeo ya mitihani, mfano, Januari 20, 2026 kuna chuo kilisajili wanafunzi wanne pekee katika mfumo wa baraza kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
“Hali hiyo haiakisi idadi halisi ya wanafunzi waliopo vyuoni, Nactvet ililazimika kuongeza muda wa usajili wa wanafunzi hadi Januari 31, 2026 ili kutoa fursa kwa vyuo vyote kusajili wanafunzi katika kanzidata ya Baraza,” amesema Dk Mahenya.
Pia, ameongeza kuwa: “Vyuo vingi vimekuwa vikichelewa au kushindwa kupakia matokeo ya mitihani kwa wakati kulingana na kalenda ya kitaaluma ya baraza, jambo linaloleta athari kwa wanafunzi na wadau wengine, changamoto hizi zinasababisha wanafunzi kukosa mikopo ya elimu, kuchelewesha kuendelea na masomo, utoaji wa vyeti pamoja na kukosa fursa za ajira.”
Dk Mahenya amesisitiza kuwa vyuo vyote vinapaswa kuwasilisha matokeo ya mitihani kupitia kanda husika kabla ya Februari 15, 2026.
Naye Meneja wa Nactvet Kanda ya Kati, Ramadhani Samainda, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Udahili, Mitihani na Utunuku wa Nactvet, Dk Marcelina Baitilwake ameeleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia changamoto za uelewa mdogo wa mifumo ya udahili na mitihani.
“Kufuatia changamoto za uelewa mdogo wa mifumo ya udahili na mitihani, kutokuzingatia taratibu na ucheleweshaji wa uthibitishaji wa matokeo, baraza limeamua kutoa mafunzi kwa maofisa udahili na mitihani ili kuondoa athari kwa wanafunzi katika kuendelea na masomo, kupata vyeti na fursa za ajira,” amesema Samainda.
Ameeleza kuwa: “Washiriki wanapatiwa mafunzo kuhusu miongozo ya udahili na mitihani, matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki, ulipaji wa ada za uhakiki wa ubora na upatikanaji wa namba za uthibitisho wa tuzo, kwa lengo la kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa vyuoni,” ameeleza Samainda.
Nactvet ni taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge, Sura ya 129, ina dhamana ya kusimamia na kuhakikisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa nchini ili kuzalisha wahitimu wenye umahiri unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.