CCM kutoa elimu kwa wanachama wake kujiimarisha

Bunda. Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuanza kutoa elimu kwa wanachama wake nchi nzima ili wajue wajibu wao katika kukiimarisha chama hicho, kifanye vizuri na kuendelea kushika dola.

Elimu hiyo itatolewa kupitia idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ambapo kabla idara hiyo haijaanza kutoa mafunzo hayo, kwanza itawezeshwa ili kuyafahamu majukumu yake matatu kuliko ilivyo sasa ambapo imeelezwa kuwa majukumu ya mafunzo na itikadi bado hayajatekelezwa vema na idara hiyo.

Kauli hiyo imetolewa mjini Bunda leo Alhamisi Februari 5, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira kwenye harambee ya ujenzi wa jengo la ofisi ya CCM Wilaya ya Bunda.

Wasira amesema chama hicho kinajivunia kuwa na wachama zaidi ya milioni 13 lakini wanachama hao bado hawajui majukumu na wajibu wao katika kuimarisha chama chao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira akisalimiana na baadhi ya viongozi wa CCM mkoani Mara baada ya kuwasili wilayani Bunda kwaajili ya kuongoza harambee ya ujenzi wa jengo la ofisi ha CCM wilayani Bunda. Picha na Beldina Nyakeke



“Kuna wale wanachama wa vilabu vya Simba na Yanga, wanajua sana majukumu yao, wao wanajua kuwa vilabu vyao vinatakiwa kufunga magoli na ikitokea wamefungwa basi wanachachamaa na hata kumfukuza kocha na benchi lote la ufundi, lakini hali ni tofauti na huku kwa wanachama wetu,” amesema.

Amesema licha ya chama hicho kuwa na idara hiyo ya Uenezi, Itikadi na Mafunzo, bado idara hiyo haijafanya kazi vizuri hasa kwenye mafunzo, hali ambayo kwa namna moja ama nyingine imesababisha wanachama kutokujua wajibu wao katika ujenzi na uimarishaji wa chama chao.

Wasira amesema chama hicho kimeamua kuweka nguvu kubwa kwenye mafunzo ili kuwa na wanachama wanaojivunia chama chao na kutimiza wajibu wao ipasavyo kuanzia ngazi ya chini.

Akizungumza kuhusu harambee hiyo, Wasira amewaomba wanachama na wapenzi pamoja na wadau wa chama hicho kuunga mkono chama hicho ili kupata Sh700 milioni zinazohitajika ili kukamilisha ujenzi huo.

Ujenzi huo wa ofisi ya CCM unafanyika kutokana na chama hicho kutokuwa na ofisi kwa sasa katika Wilaya ya Bunda baada ya ofisi yao ya awali kuchomwa moto wakati wa vurugu za uchaguzi Oktoba mwaka jana.

Amesema uratibu wa michango utafanywa na ofisi yake ambayo tayari imefungua namba maalumu ya akaunti kwaajili ya kupokea michango mbalimbali na kuahidi kuwa fedha zote zitakazopatikana zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira akisalimiana na baadhi ya viongozi wa CCM mkoani Mara baada ya kuwasili wilayani Bunda kwaajili ya kuongoza harambee ya ujenzi wa jengo la ofisi ha CCM wilayani Bunda. Picha na Beldina Nyakeke



Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bunda, Abraham Mayaya amesema watendaji na uongozi wa chama hicho, walipata wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao kutokana na kutokuwa na ofisi hali ambayo kwa namna moja ama nyingine ilisababisha kusuasua kwa utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya chama.

Amesema jukumu ambalo lilishindwa kutekelezeka kwa ufanisi ni pamoja na la kusikiliza na kutatua kero za wananchi huku akieleza kuwa miongoni mwa majukumu ya chama hicho ni pamoja kusikiliza na kutatua kero za wananchi kupitia Serikali ya CCM.

“Sisi tunaamini bila kuwasikiliza na kuwatatulia kero zao hawa wananchi basi sisi ni kazi bure, jukumu hili kwa muda huu ambao hatukuwa na ofisi lilikuwa gumu kutekelezeka kwani tulikuwa hatuna sehemu maalumu ya kufanyia kazi kwa sababu tulikuwa tunafanya kazi kwa kuhangaika sana,” amesema.

Amesema jengo hilo linalotarajiwa kugharimu Sh700 milioni pamoja na kuwa na ofisi za chama, pia, litakuwa na ukumbi  wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 300 kwa wakati mmoja, ofisi zote za jumuiya ya chama, kumbi ndogondogo, uzio na vitu vingine.