Namba za straika aliyekatwa Simba zashtua

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Simba, raia wa Cameroon, Leonel Ateba Mbida, ameendeleza kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Al Shorta kinachoshiriki Ligi Kuu ya Iraq, baada ya kufunga mabao 10 na kuasisti pia moja katika mechi zake 16, alizocheza.

Nyota huyo amejiunga na kikosi hicho cha Al Shorta, baada ya kuachana na Simba Agosti 24, 2025, ambako aliondoka katika timu hiyo ili kumpisha kiungo mshambuliaji, Neo Maema aliyesajiliwa kutokea Mamelodi Sundowns FC ya kwao Afrika Kusini.

Ateba aliyejiunga na Simba Agosti 15, 2024, akitokea USM Alger ya Algeria, katika kipindi cha mwaka wake mmoja akiwa na kikosi hicho cha Msimbazi, alihusika na mabao 17 ya Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, baada ya kufunga 13 na kuasisti manne.

Hata hivyo, katika Ligi Kuu ya Iraq hadi sasa, nyota huyo amefunga mabao 10, akishika nafasi ya tatu kwa kufunga mabao mengi, baada ya Kingsley Fidelis Kuku wa Al-Gharraf SC mwenye 11 na kinara, Sherzod Temirov wa Erbil SC aliyefunga 12.

Licha ya kufunga mabao mengi, ameiwezesha timu hiyo pia kuongoza katika Ligi Kuu ya Iraq, ambako inashika nafasi ya kwanza kwa pointi 35, baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza tatu, huku ikifunga mabao 29 na kuruhusu 11.

Mshambuliaji huyo, mbali na kuzichezea USM Alger ya Algeria na Simba ya Tanzania, ila alizichezea Coton Sport FC, PWD Bamenda na Dynamo Douala zote za kwao Cameroon.