Utafiti Mpya Wabaini Pombe Haramu Kugharimu Tanzania Zaidi ya Shilingi Trilioni 1 na Kuhatarisha Afya za Wananchi

Pombe haramu zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wananchi, mapato ya Serikali na biashara halali nchini Tanzania. Utafiti mpya umebaini kuwa asilimia 61 ya pombe yote inayotumiwa nchini ni haramu, hali inayosababisha Serikali kupoteza takribani shilingi trilioni 1.026 kila mwaka kutokana na mapato ya kodi yasiyokusanywa.

Tafiti kama hiyo zilizofanywa na Euromonitor International nchini Kenya na Uganda mwaka 2025 zimeonesha mwenendo unaofanana, ambapo pombe haramu zilichangia asilimia 60 na 67 ya matumizi ya pombe katika nchi hizo, kama zilivyotajwa.

Kwa mujibu wa utafiti huu, pombe haramu zinafafanuliwa kama pombe ambazo hazikidhi kikamilifu matakwa ya kodi, udhibiti na sheria. Hii inajumuisha pombe ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki, hazina vibali muhimu vya afya, au zinazokiuka sheria na viwango vya uzalishaji, ikiwemo matumizi ya viambato visivyoidhinishwa.

Aidha, pombe haramu zinahusisha pia usambazaji kupitia vituo visivyo na leseni, ambavyo katika nchi zinazoendelea huchangia kwa kiwango kikubwa soko la pombe katika makundi mbalimbali.

Utafiti unaonesha kuwa pombe haramu zimeenea katika makundi yote, ikiwemo pombe kali, bia na divai. Pombe za kienyeji zisizo halali au za asili kama vile Mbege, Komoni, Wanzuki, Ulanzi, Dengerua, na nyinginezo, zinachangia sehemu kubwa ya matumizi ya pombe haramu. Ingawa pombe hizi zina nafasi ya kiutamaduni, matumizi yake kwa kiasi kikubwa yanachochewa na gharama nafuu.

Kwa mfano, gongo, ambayo imepigwa marufuku, inaweza kuwa hadi asilimia 80 nafuu zaidi ikilinganishwa na pombe kali halali. Pombe bandia na zile zinazoingizwa kwa njia za magendo nazo zinaendelea kuwa changamoto, hususan katika makundi ya pombe kali na bia.

Mbali na hasara za kiuchumi, pombe haramu zinaweka afya za walaji katika hatari kubwa. Uzalishaji usiozingatia viwango vya usalama pamoja na uwezekano wa matumizi ya kemikali hatarishi huongeza hatari za kiafya. Hatari hizi zimeendelea kuongezeka kadri soko la pombe haramu linavyokua kwa kasi zaidi kuliko soko la pombe halali.

Ni katika muktadha huo ambapo utafiti huu ulifanywa ili kutoa picha ya kina na ya wazi kuhusu ukubwa wa tatizo na mabadiliko yake ya muda mrefu. Utafiti umefanywa na Euromonitor International kwa niaba ya Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), na kwa kushirikiana na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL). Utafiti huo unalinganisha hali ya sasa na mwaka 2017, ambapo pombe haramu zilichangia asilimia 55 ya matumizi yote, na kuchambua vyanzo pamoja na mienendo ya biashara ya pombe haramu nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa kutolewa kwa matokeo ya utafiti huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dennis Londo, alisema kuwa takwimu hizo zinaonesha changamoto inayohitaji hatua za haraka na za pamoja.

“Kupotea kwa zaidi ya shilingi trilioni moja kila mwaka kutokana na pombe haramu kunapunguza uwezo wa Serikali kugharamia huduma muhimu za kijamii na kulinda afya za wananchi. Utafiti huu unatupa ushahidi muhimu wa kusaidia maamuzi ya sera na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau,” alisema Mheshimiwa Londo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, sehemu kubwa ya upotevu wa mapato inatokana na pombe za kienyeji zisizo halali, maarufu kama gongo, ambazo pekee zinachangia hasara ya takribani shilingi bilioni 709 kwa mwaka. Hasara nyingine zinatokana na pombe bandia, pombe zinazoingizwa kwa njia za magendo, pamoja na ukwepaji wa kodi, ambapo ushuru hulipwa kwa kiwango pungufu au kuepukwa kabisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda (CTI), Leodegar Tenga, alisema kuwa ukosefu wa takwimu za kuaminika kuhusu pombe haramu ulikuwa sababu kuu ya kuagiza kufanyika kwa utafiti huo, kutokana na biashara hiyo kufanyika kwa siri na nje ya mifumo rasmi.

“Bila kuwa na takwimu sahihi, inakuwa vigumu kubuni hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili. Utafiti huu umefanywa ili kuziba pengo la taarifa, kuonesha ukubwa halisi wa tatizo, na kusaidia Serikali pamoja na wadau wengine kuchukua hatua zinazozingatia ushahidi,” alisema Tenga.

Akielezea uhalali wa matokeo ya utafiti huo, mshauri wa Euromonitor International, Benjamin Rideout, alisema kuwa walitumia mbinu mseto za utafiti ili kuhakikisha matokeo yanaakisi uhalisia wa soko.

“Kwa kuwa pombe haramu haziingii kwenye mifumo rasmi, tulitembelea maeneo mbalimbali yanayouza pombe hizo, mahojiano na wadau pamoja na tafiti kwa walaji ili kujenga picha kamili na inayoweza kulinganishwa na soko kwa muda,” alisema Rideout.

Kwa upande wa sekta binafsi, Kampuni ya Bia ya Serengeti ilisema kuwa ushirikiano wake na CTI unatokana na wajibu wa kulinda walaji na kuunga mkono ushindani wa haki katika soko.

“Pombe haramu zinahatarisha maisha ya walaji, zinapunguza mapato ya Serikali na kudhoofisha biashara zinazofuata sheria. Ushiriki wetu katika utafiti huu ni mchango wa kuimarisha mjadala unaozingatia ushahidi na kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Obinna Anyalebechi.

Utafiti huo pia unaonesha kuwa licha ya walaji wengi kufahamu hatari za kiafya zinazohusiana na pombe haramu, sababu kama bei nafuu, upatikanaji wake wa kirahisi kupitia njia zisizo rasmi na kukubalika kwake katika jamii zinaendelea kuchochea matumizi yake.

Kutokana na hali hiyo, utafiti unapendekeza kuimarishwa kwa udhibiti wa ethanol, kuongezwa kwa juhudi za udhibiti mipakani na ndani ya nchi, kuimarishwa kwa elimu kwa walaji, pamoja na kupanua matumizi ya teknolojia kama mifumo ya uhakiki wa stempu za kodi ili kupunguza biashara ya pombe haramu nchini.