Sababu kukithiri kero ya foleni External Dar

Dar es Salaam. Wananchi na madereva wanaotumia barabara eneo la External jijini Dar es Salaam wamelalamika kuhusu foleni sugu inayosababisha ucheleweshaji wa majukumu, usumbufu na hasara za kiuchumi.

Hali hii imekuwa ikijitokeza karibu kila siku, hususan nyakati za jioni huku magari yakikosa kupita kwa wakati kutokana na msongamano mkubwa.

Sababu za foleni hiyo ni nyingi, kati ya vichocheo vikubwa ni kusimama ovyo kwa magari katika sehemu zisizo rasmi, daladala kupakia na kushusha abiria nje ya vituo pamoja na kuharibika kwa malori.

Utitiri wa bodaboda na bajaji ambazo zimekuwa kero kwa kutofuata sheria za usalama barabarani.

Mbali na hivyo, usimamizi hafifu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani umetajwa, ambapo baadhi ya magari husimama katikati ya barabara au kwenye vituo kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168, ni kosa kwa gari lolote kusimama au kuegesha katika eneo lisilo rasmi, hususani kwenye kivuko cha waenda kwa miguu au katikati ya barabara, hali ambayo imekuwa chanzo kikuu cha foleni katika eneo la External.

Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo wanasema foleni pia huongezeka pale ambapo magari yanayotoka Ubungo Maziwa hutumia upande wa pili wa barabara ili kuepuka foleni upande wao, jambo linalopunguza ufanisi wa barabara.

Mfanyabiashara wa eneo hilo, Shedrack Mrope, amesema kutokana na wembamba wa barabara, yapo magari yanayosimama kununua mahitaji bila kujali kuwa yanakuwa chanzo cha foleni.

“Eneo letu ni dogo na linatumiwa na magari mengi. Unakuta dereva katoka huko, kaona kitu anahitaji, anasimamisha gari, anaingia dukani na kusahau kuwa njia yetu ni ndogo na anakuwa chanzo cha foleni,” amesema Mrope.

Pia amesema tabia ya daladala kupakia na kushusha abiria katika barabara hiyo imekuwa changamoto nyingine kwa sababu hakuna vituo maalumu.

“Magari yanapaki tu pembeni bila kujali kama ni kituo au la, wengine wanashusha na kupakia abiria katikati ya barabara. Hii inasababisha msongamano mkubwa,” amesema.

Madereva wa daladala nao hawajasalimika kulaumiwa, ambapo wanadaiwa kuegesha magari yao kwenye kivuko cha waenda kwa miguu, licha ya uwepo wa kituo cha daladala kilichopo karibu na taa za kuongozea magari.

Dereva wa daladala ya Mbezi hadi Mbagala, Jamal Jumbe, amesema hali hiyo inatokana na ushindani wa abiria, huku kila dereva akitaka kuwahi kuwachukua kabla ya mwenzake.

“Ukweli ni kwamba kituo kipo, lakini daladala zikisimama zote pale, wengine wanaona wanapoteza abiria. Ndiyo maana utaona gari linasimama hata kwenye kivuko,” amesema Jumbe.

Amesema si hilo tu, hata biashara ya bajaj imekuwa ikichangia kwa kusimama katika vituo na kuita abiria, hali inayosababisha kukosa sehemu sahihi ya kuegesha.

Mbali na hilo, Mrope amesema usimamishwaji wa magari na Jeshi la Polisi umechangia foleni kwani wapo polisi wa usalama barabarani wanaosimamisha malori katikati ya barabara au kuruhusu magari kusimama vituoni kwa muda mrefu.

Wananchi pia wamelalamikia usalama wa waenda kwa miguu, wakidai kuvukia barabara imekuwa hatari kutokana na daladala kuegesha juu ya vivuko, hali inayowalazimisha watu kuvuka katikati ya magari.

“Unapofika kwenye kivuko unakuta daladala zimesimama juu yake, sasa unalazimika kuvuka barabara bila ulinzi, ni hatari,” amesema Mwapewa Ally, mkazi wa Buguruni.

Akizungumza na Mwananchi Januari 31, 2026, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kuhusu eneo la External, amesema eneo hilo ni miongoni mwa barabara za kimkakati za kiuchumi zinazotegemewa kwa usafirishaji wa mizigo kutoka na kuelekea bandarini.

Amesema serikali inaendelea kuchukua jitihada kuhakikisha barabara hiyo inapunguza msongamano wa magari, hususani katika maeneo korofi kama External. Kukamilika kwa bandari kavu ya Kwala kunatarajiwa kupunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa.

“Ni mkakati wa kisayansi wa serikali unaolenga kupunguza changamoto ya foleni katika mkoa wa Dar es Salaam na kurahisisha shughuli za usafiri ili kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Muliro.

Amesema Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani linaendelea na jitihada za kudhibiti foleni katika maeneo yote yenye changamoto ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi na kuwahi majukumu yao ya kila siku.

“Tutasimamia na kudhibiti foleni ili iwe rahisi kwa watu kwenda na kutoka katika maeneo mbalimbali yenye changamoto hiyo ambayo imekuwa kero ya muda mrefu,” amesema.

Muliro amemuagiza Kamanda wa Usalama Barabarani mkoani humo kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinasimamiwa kikamilifu ili mkoa wa Dar es Salaam uwe salama.