Upatikanaji chenji za Sh100, Sh200 kunavyowatesa wafanyabiashara

Huko mtaani kumekuwa na malalamiko kuhusu upatikanaji wa sarafu za Sh100 na Sh200, hali inayowafanya wafanyabiashara kupata tabu katika kurudisha chenji kwa wateja wao.

Hilo linalalamikiwa zaidi na makondakta katika usafiri wa daladala na hivyo katika safari ambazo wanapaswa kuwarudishia abiria wao Sh100 huwawia vigumu kuzipata na kuwaomba kama wanazo wawape na zikikosekana huwaomba radhi japo wengine huwa wagumu kuelewa.

Issa Seleman, kondakta wa daladala za Mbezi amesema kutokana na kuadimika kwa sarafu hizo, hata bei ya kununua chenji yake imepanda kwani awali kwenye Sh1000 walikuwa wanapata Sh800 lakini sasa hivi ukitoa Sh1000 wanapewa Sh600.

“Hali hii inatuathiri hata katika hesabu za kuwapelekea matajiri wetu, ukienda kuchenji Sh1,000 aliyoitoa abiria mmoja, wewe ukapewa Sh600, kwa hesabu za haraka huyo mtu utakuwa umemlipisha nauli Sh200, wakati mwingine ni bora mtu akupe Sh500 kama hana Sh600 na hilo wala tajiri halimuhusu,” anasema Seleman.

 Aziz Chongolo anasema kutokana na sarafu hizo kuwa adimu imewalazimu kuwa wanatoza nauli ya Sh500 badala ya kutoza Sh600 iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini(Latra) ili kuondoa kero ya kutafuta chenji.

Jambo hilo pia linadhihirishwa na abiria wa Chanika kwenda Zingiziwa, Zuwena Ramadhan anayesema katika nauli ya Sh600 waliyokuwa wanatozwa siku za nyuma ilikuwa ukikosa Sh100 ni ugomvi lakini sasa makondakta ndiyo wanaokata Sh500.

Patrick Lymo kondakta wa daladala za Gongo la Mboto-Kivukoni anasema kwa sababu nauli ni Sh700, anachofanya ni kuwaomba abiria wanaotoa Sh1,000 kuambatanisha na Sh200 ili amrudishie Sh500.

Moshi Kilonzo dereva wa daladala anayefanya safari zake Tabata Segerea kwenda Mnazi Mmoja amesema sasa hivi wanategemea kupata chenji kwa wafanyabisahara ndogondogo, ambao hao kutokana na vitu wanavyouza ni rahisi kuzipata.

“Hivyo ninapopita maeneo ya pale soko la Buguruni, kuna watu wananijua kabisa kuwa huwa nahitaji chenji hizo, hivyo huniletea katika Sh1000 napata Sh800,” amesema Kilonzo.

Neema Gabriel aliyekuwa akifanya biashara ya kuuza chenji anasema sasa hivi ameacha kwani hazipatikani.

Angel Leornad anayefanya kazi katika moja ya maduka makubwa Posta anasema wamekuwa wakiwapa bidhaa wateja wao inayolingana na thamani ya chenji ikiwemo pipi au biskuti ndogondogo.

John Kimaro mfanyabiashara wa duka la vitu vya rejareja maeneo ya Vingunguti alisema inapobaki chenji ya Sh200 au Sh100 humpa mteja kiberiti au pipi mbili za Sh50 ilimradi tu mteja asije akaona kamchukulia hela yake bure.

 Akizungumzia suala hilo, Meneja Idara ya Sarafu, Ilulu Said Ilulu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) anasema sio kweli kuwa sarafu hizo zimeadimika kwani zipo nyingi.

“Huenda tu kuna watu wanatumia ujanja zionekane ni adimu mtaani ili waweze kufanya biashara yao ya kuuza chenji, jambo ambalo haliruhusiwi kwani huduma hii ukienda benki inatolewa bure,” anasema Ilulu.

Akifafanua kwanini hazionekani mtaani, anasema hali hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo watu wanaopaswa kwenda kuzichukua benki huenda hawafanyi hivyo.

“Nao siyo wengine ni benki ambao hao ndio wenye dhamana ya kwenda kuwasambazia watu. Hii ndio maana kwenye benki zetu kuna dirisha kwa ajili ya kuhudumia watu wanaotaka chenji. Jambo la Pili huenda imechangiwa na kushuka kwa thamani ya sarafu zenyewe, ambapo kwa sasa vitu vingi haviuzwi kwa hela hiyo,” anasema.

Anasema hali hiyo huweza kufanya sarafu kuanza kupotea kwenye mzunguko wa fedha huku akiweka wazi kuwa zikipotea huwa haziruidi benki bali hupotea mtaani na ni jambo ambalo lipo duniani kote.

“Hili tumeliona kwenye hela ya senti tano, Sh5, Sh10 na Sh20, kwani hizi sio kwamba haziruhusiwi kutumika bali ni thamani yake imeshuka katika kununulia vitu ndio maana huzioni huko mtaani kwenye mzunguko wa fedha,” anasema.

Sababu nyingine ni kuongezeka huduma za malipo kwa njia ya kidigitali ambapo siku hizi watu wengi hawalipi kwa pesa taslimu, hivyo fedha hizi kuzipata inakuwa shida nazo.

“Kama unakumbuka kuna wakati katika usafiri wa mabasi ya mwendokasi wananchi walipaza sauti kuhusu kupatiwa chenji, hivyo BOT tulilazimika kutoa huduma maalum kwa Kampuni ya Udart inayotoa huduma hizo lakini tangu wameanza kukata kwa kadi kelele hizo hazipo tena,” anasema Ilulu.

Mbali na Udart, Meneja huyu anasema pia walikuwa waliwapa huduma hiyo Shirika la reli Tanzania (TRC) chenji kwa treni zao zinazotoa huduma katikati ya jiji, daraja la Kigamboni na kwa baadhi ya maduka makubwa.

Alipoulizwa juu ya mashine za kuchezea bahati nasibu maarufu kwa jina la ‘dubwi’ kuwa moja ya kichocheo cha kupotea kwa sarafu hizo Ilulu anasema katika kipindi cha miezi mitano iliyopita hili suala lilikuwa ni kweli, kwani mashine moja ilikuwa na uwezo wa kumeza sarafu 200,000.

“Tulikuja kushtuka zaidi ya Sh8 bilioni zilikuwa katika mashine hizo zilizopo maeneo mbalimbali nchini ambazo zinaelezwa kuwa zipo zaidi ya 40,000, fedha ambazo ni nyingi katika masuala ya mzunguko wa fedha ni nyingi,” anasema.

Hata hivyo anasema baada ya serikali kubadili sheria na kufanya Aprili 2025 kuwa mwisho wa mashine hizo kutumia sarafu na badala yake zinatakiwa ziwe na tokeni zao zitakazokuwa na thamani ya sarafu hizo ilisaidia kupunguza hali hii.

 Kutokana na uhaba huu wa sarafu za Sh100 na Sh200, Ilulu anabainisha kuwapo kwa mikakati ya kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kusogeza huduma hizo kupitia mawakala kwani benki ndizo zinafanya kazi na wakala hao.

“Tuna imani hata huduma hiyo ya chenji tukijipanga vizuri wataweza kuitoa na huduma hii naomba nisisitize ni bure ukitoa Sh1,000 unapewa hizo sarafu zenye thamani hiyohiyo kwa kuwa sheria ya sarafu inabadilishwa na sarafu na sio kununua,” anasema.

Lakini hata kabla hatujafika hivyo, pia nashauri hao madereva na makondakta wanaweza kupitia vyama vyao kumtuma mmoja wao benki kuwachukulia chenji hizo au kupitia vyama vya wafanyabiashara sokoni pia nao wanaweza kufanya hivyo.

Anafafanua kuwa katika box la Sh50 wana kimfuko kinachotoa chenji za hivyo za thamani ya Sh300,000 wakati kwenye Sh100 kuna chenji za zenye thamani ya Sh500,000, na kwenye Sh200 kuna chenji za thamani ya Sh1 milioni moja huku kwa Sh500 kuna chenji za thamani ya Sh2.5 milioni.

“Huduma hizo wanaweza kuzipata katika matawi yetu tuliyofungua maeneo mbalimbali ambapo ni benki za kibiashara nchini na utapata box lake likiwa limefungwa kutoka kiwandani,” anasema Ilulu.