KIUNGO wa Simba, Neo Maema, amefichua kwamba, baada ya kumalizika msimu huu, ana machaguo mawili anayosikilizia ambayo ni kurudi Mamelodi Sundowns au kubaki klabuni hapo endapo itamnunua moja kwa moja kutokana na hivi sasa kucheza kwa mkopo.
Maema aliyetua Simba katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu akitokea Mamelodi Sundowns ya kwao Afrika Kusini, alitua sambamba na beki wa kati, Rushine De Reuck ambao wote wawili walipendekezwa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Fadlu Davids kabla ya kutimkia Raja Casablanca.
Akizungumza na kituo cha redio cha Sports Night Amplified cha Metro FM nchini Afrika Kusini, Maema amesema hatua ya kujiunga na Simba haikuwa rahisi kama wengi walivyofikiria.
“Sijazungumza moja kwa moja na klabu kuhusu timu nyingine yoyote, nilipata taarifa tu kutoka kwa wakala wangu kwamba kuna klabu inayovutiwa na mimi,” amesema Maema na kuongeza.
“Watu wengi hawajui, lakini kuja Tanzania kulikuwa kugumu kwa sababu ilinibidi nijadiliane na klabu. Wengi hawajui kuwa niko kwa mkopo na mkataba wangu utakapomalizika bado ninapaswa kurejea Sundowns kusikia watasema nini.”
Kiungo huyo aliongeza kuwa, hafahamu kwa nini taarifa ya kwenda kwa mkopo haikuwekwa wazi tangu mwanzo na kwa sasa hana uhakika kwamba Simba itamnunua moja kwa moja.
“Niko kwa mkopo na sijui kwa nini haikuelezwa wazi. Baada ya msimu huu nina chaguo mbili ama Simba watazingatia kipengele cha kuninunua au nitaachana nao, kwa sasa sina jibu la uhakika.”
Maema amecheza mechi 10 akiwa na Simba msimu huu, zikiwemo tano za Ligi ya Mabingwa Afrika ambako alifunga bao moja hatua ya makundi ugenini dhidi ya Stade Maliend wakati Simba ikifungwa 2-1.
Kwa ujumla, Maema alicheza dakika 19 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Simba ilipopoteza bao 1-0, kwenye ligi alicheza dakika 26 dhidi ya Fountain Gate, Namungo (dakika 45), JKT Tanzania (dakika 90), Azam (dakika 90), Mbeya City (dakika 31) na Mtibwa Sugar (dakika 74).
Kimataifa alicheza dakika 90 dhidi ya Petro Atletico, Mnyama akipoteza kwa bao 1-0 nyumbani, dhidi ya Stade Malien (dakika 64) na Esperance de Tunis (dakika 9).
Lengo la Mamelodi kumtoa Maema kwa mkopo, lilikuwa kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara na kuimarisha kiwango chake, ambapo tangu aondoke, klabu hiyo imesajili viungo wengine akiwemo Nuno Santos, Miguel Reisinho na Tsiki Ntsabeleng ambao wameonyesha kiwango bora na kuongeza ushindani katika nafasi yake.