Dodoma. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ametahadharisha kuwa bila kusimamia utu, Chama cha Mapinduzi (CCM) inaweza kuondoka madarakani hivyo akaonya wanachama ndani ya chama hicho wasione aibu kusimamia utu.
Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ametoa kauli hiyo bungeni leo Alhamisi Februari 5,2026 wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali uliowasilishwa mwanzoni mwa wiki na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Mbunge huyo, ameanza kutoa mchango wake kwa kukitakia mema chama cheke CCM ambacho leo kimetimiza miaka 49 tangu kilipoasisiwa.
CCM ni Muunganiko wa vyama viwili vya Tanganyika African Nation Union (TANU) Afro- Shiraz Party (ASP) ambavyo viliungana Februari 5, 1977 na kuzaa Chama cha Mapinduzi.
Amesema kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2025, kauli mbiu ilikuwa kazi na utu” “Suala la utu liende kwa wazi kwa machinga, wakulima, vyombo vya dola kila mahali iwe ni utu, tukimung’unya maneno CCM itaondoka jamani, tusione aibu Serikali macho kwa macho ithamini utu wa binadamu, na tusione aibu kuisimamia.”
Katika hatua nyingine, Nape amesema CCM kimefanya mambo mema akieleza hapa duniani, vimebakia vyama vichache huku akieleza chama hicho ni chama cha kibinadamu hivyo kinaweza kuwa na mabonde na milima.
“Lakini pamoja na hayo, katika moja ya misingi ambayo Mwalimu Nyerere alituachia ni kujikosoa, Mwalimu alituambia kujikosoa ndiyo msingi wa uimara wa chama nasi tumedumu hivyo na ndiyo maana tumeendelea kuwa imara,” amesema Nape.
Nape amesifu mpango namna ulivyoweka mikakati ya uwazi kwa upatikanaji wa viongozi wa umma, lakini mipango ya kusaini mikataba kwenye ajira zao kwamba utaongeza uwajibikaji.
Amesema kila mtu ni lazima apewe malengo ili asipotimiza aondoke na eneo lake awekwe mtu mwingine ingawa amesisitiza jambo hilo liende hadi kwa watumishi wa umma, wakurugenzi na watendaji wakuu.
Kwa mujibu wa Nape, kumekuwa na utamaduni watu wanabweteka hawafanyi kazi inavyotakiwa hadi wanastaafu lakini sasa itakuwa kila mwajiriwa kupewa mikataba ya malengo ili mtu akishindwa kufikia malengo kuwepo na kisingizio wala kumung’unya maneno bali awekwe pembeni.
Ameiomba Serikali inapoelekeza kwenye miradi mikubwa na kuja na miradi midogo ndani yake, wasiache kuweka mpango wa ujenzi wa reli ya kasi kutoka Dar es Salaam kwenda Kusini ili isaidie kulinda bandari zinazojengwa huko.
Akizungumzia mpango kubebwa na sekta binafsi, ameitaka Serikali kuwaandaa wale ambao watakuwa na mchango huo lakini akatahadharisha bila kuwaandaa sekta binafsi, hata walinzi watatoka nje ya nchi.