Pombe haramu zinavyoitafuna Tanzania | Mwananchi

Dar es Salaam. Utafiti mpya uliofanywa umebaini kuwa asilimia 61 ya pombe yote inayotumiwa nchini ni haramu, hali inayosababisha Serikali kupoteza takribani Sh1.026 trilioni kila mwaka kutokana na mapato ya kodi yasiyokusanywa.

Utafiti huo umefanywa na Euromonitor International kwa niaba ya Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kwa kushirikiana na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ukilinganisha hali ya sasa na mwaka 2017, na pombe haramu zilichangia asilimia 55 ya matumizi yote, na kuchambua vyanzo pamoja na mienendo ya biashara ya pombe haramu nchini Tanzania.

Tafiti kama hizi, zilizofanywa na Euromonitor International nchini Kenya na Uganda mwaka 2025, zimeonesha mwenendo unaofanana, ambapo pombe haramu zilichangia asilimia 60 na 67 ya matumizi ya pombe katika nchi hizo mtawalia.

Kwa mujibu wa utafiti huo, pombe haramu zinafafanuliwa kama pombe ambazo hazikidhi kikamilifu matakwa ya kodi, udhibiti, na sheria.

Hii inajumuisha pombe ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki, hazina vibali muhimu vya afya, au zinazokiuka sheria na viwango vya uzalishaji, ikiwemo matumizi ya viambato visivyoidhinishwa.

Pombe haramu zinahusisha pia usambazaji kupitia vituo visivyo na leseni, ambavyo katika nchi zinazoendelea huchangia kwa kiwango kikubwa soko la pombe katika makundi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kutolewa kwa matokeo ya utafiti huo, leo Februari 5, 2026, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema kuwa takwimu hizo zinaonesha changamoto inayohitaji hatua za haraka na za pamoja.

“Kupotea kwa zaidi ya Sh1 trilioni kila mwaka kutokana na pombe haramu kunapunguza uwezo wa Serikali kugharamia huduma muhimu za kijamii na kulinda afya za wananchi. Utafiti huu unatupa ushahidi muhimu wa kusaidia maamuzi ya sera na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau,” amesema Londo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, sehemu kubwa ya upotevu wa mapato inatokana na pombe za kienyeji zisizo halali, maarufu kama gongo, ambazo pekee zinachangia hasara ya takribani Sh709 bilioni kwa mwaka.

Hasara nyingine zinatokana na pombe bandia, pombe zinazoingizwa kwa njia za magendo, pamoja na ukwepaji wa kodi, ambapo ushuru hulipwa kwa kiwango pungufu au kuepukwa kabisa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda (CTI), Leodegar Tenga, amesema ukosefu wa takwimu za kuaminika kuhusu pombe haramu ulikuwa sababu kuu ya kuagiza kufanyika kwa utafiti huo, kutokana na biashara hiyo kufanyika kwa siri na nje ya mifumo rasmi.

“Bila kuwa na takwimu sahihi, inakuwa vigumu kubuni hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili. Utafiti huu umefanywa ili kuziba pengo la taarifa, kuonesha ukubwa halisi wa tatizo, na kusaidia Serikali pamoja na wadau wengine kuchukua hatua zinazozingatia ushahidi,” amesema Tenga.

Akielezea uhalali wa matokeo ya utafiti huo, mshauri wa Euromonitor International, Benjamin Rideout, amesema walitumia mbinu mseto za utafiti ili kuhakikisha matokeo yanaakisi uhalisia wa soko.

“Kwa kuwa pombe haramu haziingii kwenye mifumo rasmi, tulitembelea maeneo mbalimbali yanayouza pombe hizo, kufanya mahojiano na wadau, pamoja na tafiti kwa walaji, ili kujenga picha kamili na inayoweza kulinganishwa na soko kwa muda,” amesema Rideout.

Katika hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Obinna Anyalebechi, amesema kuwa ushirikiano wake na CTI unatokana na wajibu wa kulinda walaji na kuunga mkono ushindani wa haki katika soko.

“Pombe haramu zinahatarisha maisha ya walaji, zinapunguza mapato ya Serikali, na kudhoofisha biashara zinazofuata sheria. Ushiriki wetu katika utafiti huu ni mchango wa kuimarisha mjadala unaozingatia ushahidi na kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu,” amesema.

Utafiti huo pia unaonesha kuwa, licha ya walaji wengi kufahamu hatari za kiafya zinazohusiana na pombe haramu, sababu kama bei nafuu, upatikanaji wake wa kirahisi kupitia njia zisizo rasmi, na kukubalika kwake katika jamii, zinaendelea kuchochea matumizi yake.

Kutokana na hali hiyo, utafiti unapendekeza kuimarishwa kwa udhibiti wa ethanol, kuongezwa kwa juhudi za udhibiti mipakani na ndani ya nchi, kuimarishwa kwa elimu kwa walaji, pamoja na kupanua matumizi ya teknolojia kama mifumo ya uhakiki wa stempu za kodi, ili kupunguza biashara ya pombe haramu nchini.

Kwa mfano, gongo, ambayo imepigwa marufuku, inaweza kuwa hadi asilimia 80 nafuu zaidi ikilinganishwa na pombe kali halali.

Pombe bandia na zile zinazoingizwa kwa njia za magendo nazo zinaendelea kuwa changamoto, hususan katika makundi ya pombe kali na bia.

TRA inavyopambana na pombe haramu

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, akizungumza na Mwananchi leo, Februari 5, 2026, amesema ili kukabiliana na pombe haramu na bandia, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kupunguza na hatimaye kutokomeza pombe hizo.

Amesema TRA imetekeleza mfumo wa Stempu za Kielektroniki za Kodi zinazowekwa kwenye vinywaji vyote vinavyotozwa ushuru wa forodha, vinavyozalishwa ndani ya nchi na vile vinavyoagizwa kutoka nje.

“Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuuza au kuonesha bidhaa zinazotozwa ushuru bila kuwa na stempu halisi za kodi. Ikiwa mlipakodi ataingiza bidhaa za magendo, hawezi kupata stempu halisi za kodi na mara nyingi hulazimika kutumia stempu bandia,” amesema.

Amesema endapo mtu atapatikana, atakabiliwa na adhabu za kisheria, ikiwemo kifungo cha gerezani.

“Pia TRA imetekeleza matumizi ya Programu ya Hakiki Stempu, ambayo ni programu ya bure inayopatikana kwenye majukwaa yote ya simu za mkononi, ikiwemo Android na iPhone (iOS).

“Programu hii hutumiwa zaidi na wazalishaji, waagizaji na watumiaji wa mwisho kuhakiki uhalisi wa bidhaa na stempu za kodi kabla ya kuingiza bidhaa hizo kwenye maeneo ya biashara au kabla ya matumizi. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 35 ya Kanuni za Stempu za Kielektroniki za Kodi za mwaka 2018,” amesema.

Mbali na hayo, amesema TRA imeanza kutumia Akili Unde na LLM (Large Language Model) kupitia Suluhisho la Ujasusi wa Soko la Kidijitali (Digital Market Intelligence Solution) kuchakata data ya mwanzo hadi mwisho na kubaini mienendo na vitendo vinavyotia shaka katika bidhaa zinazotozwa ushuru.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Kayombo, imeboresha utekelezaji wa shughuli za ukaguzi zinazolengwa na kuwawezesha wakaguzi kuchukua hatua za haraka na za kinga dhidi ya uwepo wa stempu bandia ndani na nje ya nchi.

“TRA inaendelea kutoa elimu kwa walaji na wafanyabiashara wa bidhaa zote zinazohitaji stempu za kielektroniki za kodi, kwa kuhakikisha wanapakua na kutumia programu rasmi ya uhakiki wa stempu ili kuhakiki vinywaji vyao kabla ya matumizi,” amesema.