Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitoa hundi ya Sh200 bilioni kuwezesha vijana na wanawake kiuchumi, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itachukua hatua kali kwa wale wanaofanya ubabaishaji na unyonyaji, kuwaumiza wananchi kupitia mikopo kausha damu.
Dk Mwigulu amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe kuwaelekeza wakuu wa mikoa, kuchukua hatua kwa watu wanaotumia shida za Watanzania kuwaweka kwenye minyororo ya unyonyaji.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Februari 5, 2026 jijini Dodoma, katika hafla ya utoaji wa hundi ya Sh200 bilioni kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya vijana ikiwa ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za uongozi wake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025.
Kuhusu utoaji wa fedha hizo, Dk Mwigulu amesisitiza uwazi wa masharti yanayotumika kutoa fedha hizo.
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Ikiwa ni sehemu ya kushukuru, amehimiza jamii kuwa na wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa fedha hizo, akisema Serikali inataka kuwaondolea adha ya mikopo yenye masharti makali.
Dk Mwigulu amesema bila kueleza uwazi masharti ya utoaji wa fedha hizo, wananchi watajenga dhana fedha wanazokopeshana mitaani zina masharti rahisi kuliko benki.
“Nimefuatilia hakuna benki ina masharti magumu kama yale ya kausha damu ambayo watu wanakimbilia na mbaya zaidi wanaokimbilia sio watu ambao unadhani ni kutoka vijijini hata watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na watumishi wa Serikali wamo kwenye kausha damu.
“Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa wale wanaofanya ukopeshaji usio rasmi unaoumiza watu, masharti yake hayajadhibitiwa,”amesema.
Akifafanisha mikopo ya benki na kausha damu, amesema hakuna unafuu wowote kwenye kausha damu bali unafuu upo kwenye taasisi rasmi za kibenki.
Hatari ya mikopo kausha damu, Dk Mwigulu amesema riba zake hutolewa na watu wasio rasmi akiahidi Serikali kuchukua hatua kali.
“Serikali itachukua hatua kali kwa wale wanaofanya ubabaishaji na unyonyaji kupitia mikopo kausha damu,”amesema.
Dk Mwigulu ametoa rai kwa taasisi za kifedha kuendelea kutoa elimu na kuanzisha dirisha la kulea watu wanaofanya nao kazi, kwa kuwa watu wanaogopa harakati zinazompata mtu aliyefilisika.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akipokea kutoka kwa Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Mbali na hayo, Dk Mwigulu amesema Watanzania wameumizwa sana katika mambo ya kuaminiana.
“Unaenda mnapeana mikopo masharti magumu, kwa sababu anajua huyu ni ndugu yangu na anashida anachukua mkopo baadaye anakuja kusombewa vitu vyake vya ndani,” amesema.
Katika kudhibiti hali hiyo, amesema Serikali itaendelea kuboresha masharti na kuweka upatikanaji wa mitaji kwa njia rasmi ili kuwaondoa Watanzania kukimbilia njia zisizo rasmi zinazowaongezea umasikini.
Dk Mwigulu amesema tayari Rais Samia ameelekeza kundi la vijana, wanawake na wenye ulemavu waliokuwa wakipokea mkopo kupitia halmashauri, kufikia Juni Serikali itaongeza asilimia tano ya mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
“Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya masoko, miundombinu inayohusisha maeneo ya kufanyia biashara,”amesema.
Katika msisitizo wake, Dk Mwigulu amesema uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ni mpango unaotekelezwa na Serikali na sekta binafsi kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kushiriki shughuli za kiuchumi kikamilifu.
Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka ambaye ndio mratibu wa programu hiyo, kuhakikisha fedha zinaingia benki ili ziwafikie walengwa.
“Twendeni tukazifikishe fedha hizi kwa walengwa kupitia programu zilizokusudiwa, tulibadilisha utaratibu wa kugawa fedha kupitia halmashauri ili kuepusha fedha kwenda kwenye vikundi hewa.
“Rais Samia hajakusudia fedha hizi ziende kwenye vikundi hewa kwa sababu vikundi hewa matokeo hayataonekana,” amesema.
Ametaka wizara zinazohusika na sera na mikakati yake kuhakikisha zinaakisi dhana ya uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi.
Mbali na hayo, Dk Mwigulu ametaka sera zinazokwamisha ubunifu, ujasiriamali au upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali, kufanyiwa mapito kwa kuwa malengo hayawezi kufikiwa kama kazi zikifanyika kwa mazoea.
“Tumekuwa wadhibiti zaidi ya wawezeshaji, sasa kwenye nchi ambayo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi, kila kitu inapaswa kufanyika kwa kasi, kila ofisi na taasisi tuwe wawezeshaji zaidi ya kuwa wadhibiti ili programu ziwezeshwe,” amesema.
Dk Mwigulu ameziagiza taasisi za fedha kutangaza kwa uwazi bidhaa za uwezeshaji za Serikali zikiwamo zinazotokana na fedha ambazo Serikali inatoa kupitia mabenki nchini.
Akizungumzia ahadi za Rais Samia, Dk Mwigulu amesema takribani ahadi zote alizotoa Rais zimetekelezwa kwa vitendo vinavyoonekana ikiwamo ajira 5,000 za watumishi wa sekta, ndani ya siku 100.
Ahadi nyingine, Dk Mwigulu amesema walimu 7,000 wa sayansi na hesabu tayari wameshaajiriwa na tayari Bima ya Afya kwa Wote imezinduliwa na kuanza kwa makundi maalumu.
Pia, jambo lingine lililotekelezwa amesema ni kupigwa marufuku uzuiaji wa miili katika hospitali.
Amesema utoaji wa hundi ya Sh200 bilioni unaonesha namna ambavyo Serikali ya awamu ya sita inatekeleza ahadi zake sio kwa maneno pekee bali kwa vitendo.
“Tukio hili linaweka msingi wa kuimarisha ushiriki wa vijana na wanawake katika uchumi wa Taifa na kuharakisha safari ya Tanzania kwenye uchumi jumuishi na endelevu.
Hii ni nyongeza ya fedha zilizoendelea kutoka kuhusu kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,”amesema.
Hatua zingine zilizofanyika ni kuwezesha vijana kushiriki shughuli za uzalishaji kupitia kujenga kesho iliyobora Building Better Tomorrow (BBT).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi amesema utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia ni kusaidia makundi ya vijana na wanawake kuchumi.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka, hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. kulia ni kutoka kwa Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar na kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) William Lukuvi. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Lukuvi amedokeza kuwa, Sh200 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa vijana zitawezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake waliojikita katika maeneo ya sanaa, kilimo, uvuvi, filamu, biashara, viwanda, usafirishaji na huduma za chakula.
“Fedha hizi zitawezesha uchocheaji kiuchumi hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji na vijijini ambako bado vijana na wanawake wana changamoto zaidi,” amesema.
Lukuvi amesema utoaji wa mitaji hiyo utazingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji na tija; na fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyo kusudiwa.
“Serikali itaimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kwa wanawake na vijana ili fedha hizo zikawezeshe makundi hayo,”amesema Lukuvi.