COSTECH YATAKIWA KUBUNI MFUMO RAHISI KUFIKISHA MATOKEO YA TAFITI

Serikali imeiagiza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kubuni na kuimarisha njia rahisi za kufikisha matokeo ya tafiti kwa Wizara husika na taasisi nyingine zinazohusika, ili matokeo hayo yafanyiwe kazi na kusaidia kutatua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yalibainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa kila mwaka wa maendeleo ya utafiti chini ya Programu ya Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Profesa Mushi alisema matokeo ya tafiti ni muhimu kwa taifa kwa kuwa yataisaidia Serikali na Wizara husika kupata suluhisho la changamoto mbalimbali, ikiwemo uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Alisisitiza kuwa wajibu wa watafiti na wadau wa sekta ya sayansi haupaswi kuishia katika mikutano na machapisho pekee, bali wanapaswa kufuatilia kwa karibu kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.

“Hatupaswi kuishia kwenye huu mkutano pekee, bali tuwajibike kwa wananchi kwa kuwapatia matokeo ya tafiti na kuelekeza matumizi bora ya matokeo hayo,” alisema Profesa Mushi.

Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni janga la dunia lenye athari kubwa kwa mataifa yote, ikiwemo Tanzania, na kwamba yanatishia tija ya kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi. Pia alisema mabadiliko ya tabianchi huongeza gharama za kukabiliana na majanga na ukarabati wa miundombinu, hali inayopunguza rasilimali ambazo zingeweza kuwekeza katika sekta za elimu, afya na vipaumbele vingine vya maendeleo.

Kwa mujibu wake, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kunahitaji utafiti wa kina ili kuboresha sera na mikakati ya Serikali. Alisisitiza kuwa utafiti wa mabadiliko ya tabianchi usilenge tu kuongeza maarifa ya kitaaluma, bali uzingatie zaidi kutatua matatizo halisi yanayolikabili taifa.

Alibainisha kuwa Serikali inatambua umuhimu wa utafiti katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ndiyo maana ilianzisha Programu ya Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi inayoratibiwa na COSTECH.

Profesa Mushi alisema utekelezaji wa programu hiyo unahusisha Vyuo Vikuu na taasisi za utafiti 20 nchini, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali unaolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali.

Alisema hadi sasa programu hiyo imepatiwa jumla ya Sh bilioni 14.5, ambapo Sh bilioni 12.1 tayari zimewekezwa katika miradi 39 ya utafiti inayojikita kuchunguza na kutafuta suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika sekta za kilimo, maliasili, afya, nishati, maji pamoja na mifumo ya kijamii na kiuchumi.

Aliongeza kuwa matarajio ya Serikali kwa watafiti waliopata fedha hizo ni makubwa, na kwamba anatarajia miradi 34 kati ya hiyo kuwasilisha matokeo ya tafiti zao katika mkutano huo.

“Nitoe wito kwa watekelezaji wa miradi yote 39 kuhakikisha kila shilingi inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. COSTECH ihakikishe inasimamia vyema fedha za utafiti na kuratibu uwasilishaji wa matokeo kwa wadau wote,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwataka watafiti kuhakikisha tafiti zao zinaendana na vipaumbele vya kitaifa, kushirikisha wananchi, watendaji na watunga sera katika hatua zote za utafiti, badala ya kusubiri mwisho wa miradi na kuwasilisha matokeo kupitia machapisho pekee.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema kuwa hadi sasa programu hiyo imeshirikisha Taasisi 13, Vyuo Vikuu 12 na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), huku jumla ya watafiti 200 na wanafunzi 90 wakishiriki.

Dkt. Nungu aliwashukuru wafadhili wa programu hiyo, akiwataja kuwa ni SIDA na Serikali ya Norway, kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa programu ya utafiti wa mabadiliko ya tabianchi nchini.

Kwa upande wake mwakilishi wa SIDA Dkt. Johanna Variandek alisema wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha tafifi mbalimbali zinafanya vizuri.

Mwenyekiti wa Bodi ya Makamishna ya COSTECH Prof. John Kondoro alisema mkutano huo utakuwa na majawabu yenye ushahidi wa kisayansi ambayo yatasaidia kutatua changamoto mbalimbali zitokanazo na athari za mabadiliko ya tabia nchi.