Siri za kiafya kwenye nywele za kwapa

Mwanza. Watu wengi katika jamii za kisasa huona nywele za kwapa kama kitu kisichofaa au kisichopendeza, hasa kutokana na mitazamo ya urembo na usafi.

Hata hivyo, nywele hizi ambazo huanza kukua wakati wa balehe, ni sehemu muhimu ya mwili wa binadamu na zina kazi nyingi za kiafya, kibiolojia na hata kisaikolojia.

Makala hii itajadili kwa undani faida za nywele za kwapa na kwa nini zinapaswa kutunzwa badala ya kuondolewa kiholela.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa magonjwa ya binadamu wa Hospitali ya Lugeye mkoani Mwanza, Dk Daudi Amoni,  nywele za kwapa zina faida nyingi ikiwemo kupunguza msuguano, kufyonza jasho, kuzuia maambukizi pamoja na kulinda ngozi

Nywele za kwapa husaidia kupunguza msuguano kati ya ngozi ya kwapa na mikono. Wakati mtu anapotembea, kufanya mazoezi, au kufanya kazi za mikono, mikono mara nyingi hukandamiza ngozi ya kwapa.

Bila nywele, msuguano huu unaweza kusababisha muwasho, vidonda vidogo au kuchubuka. Nywele hutoa safu ndogo ya ulinzi inayopunguza mguso wa moja kwa moja kati ya ngozi na ngozi, hivyo kuzuia maumivu na kuwasha.

Nywele za kwapa hufanya kazi muhimu ya kunyonya na kusambaza jasho. Sehemu ya kwapa ina tezi maalum za jasho zinazoitwa apocrine glands ambazo hutoa jasho lenye mafuta na protini.

Nywele za kwapa husaidia kufyonza unyevu huu na kuusambaza, hivyo kusaidia mwili kupooza na kudhibiti joto.

Bila nywele hizi, jasho lingejaa moja kwa moja kwenye ngozi, na kusababisha hisia ya unyevunyevu na harufu kali. Kwa maneno mengine, nywele hizi huchangia katika utaratibu wa asili wa kudhibiti halijoto ya mwili.

Nywele hizi huchangia katika utoaji wa harufu ya asili ya mwili, ambayo kwa baadhi ya wanasayansi inahusiana na mvuto wa kijinsia na mawasiliano ya kimaumbile.

Tezi za apocrine zinazopatikana chini ya kwapa huzalisha kemikali ndogo zinazoitwa pheromones, ambazo zinaweza kuwa na jukumu katika kuvutia watu kimapenzi. Husaidia kuhifadhi na kusambaza harufu hizi, ambazo ni sehemu ya mawasiliano ya kiasili yasiyo ya maneno kati ya binadamu.

Picha na Mtandao



Aidha, nywele za kwapa hulinda ngozi dhidi ya vijidudu. Nywele hizi pamoja na mafuta ya ngozi (sebum) huunda kizuizi cha asili kinachozuia bakteria na vimelea wengine kupenya moja kwa moja kwenye ngozi laini ya kwapa.

Wakati mtu ananyoa au kung’oa nywele hizo, mara nyingi husababisha michubuko midogo inayoweza kutoa nafasi kwa bakteria kusababisha maambukizi kama vile folliculitis au boils. Hivyo, kuacha nywele za kwapa angalau kwa urefu fulani ni njia bora ya kujikinga dhidi ya maambukizi.

Pia, nywele za kwapa zina umuhimu wa kihisia na kisaikolojia. Ukuaji wake ni moja ya dalili za kubalehe, na kwa vijana, ni ishara ya ukuaji wa kimaumbile na mabadiliko ya homoni.

Hii husaidia katika kujenga utambulisho wa kijinsia na kujiamini. Kwa baadhi ya tamaduni, nywele hizi ni ishara ya utu uzima na nguvu za asili za mwili.

Kwa upande mwingine, watu wengi huchagua kuzinyoa kwa sababu za urembo au harufu. Hata hivyo, inashauriwa kutumia njia salama kama vile kukata kwa urefu mfupi badala ya kung’oa kabisa, ili kuepuka maambukizi na muwasho.

Usafi wa mara kwa mara pia ni muhimu ili kuzuia harufu inayoweza kujitokeza kutokana na mkusanyiko wa jasho.

Utafiti uliofanywa mwaka 2012 umebaini kuwa imani  kwamba kunyoa nywele za kwapa hupunguza harufu ya mwili kwa muda mrefu si kweli, kwani hatua hiyo hutoa nafuu ya muda mfupi pekee kabla harufu haijarudi katika hali yake ya kawaida.

Utafiti huo, uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Charles University na kuchapishwa mwaka 2012, uliendeshwa na watafiti Dagmar Kohoutova, Anna Rubesovana Jan Havlicek, ambao waliangalia tofauti za harufu ya mwili kwa wanaume baada ya kunyoa na baada ya nywele kuanza kukua tena.

Katika utafiti huo, wanaume walitoa sampuli za harufu katika kipindi tofauti, mara baada ya kunyoa, siku chache baadaye, na hadi wiki moja kisha wanawake waliombwa kupima harufu hizo kwa kuangalia uzito, kupendeza na kuvutia.

Matokeo yalionesha kuwa harufu ya kwapa mara tu baada ya kunyoa huonekana kupendeza lakini hali hiyo hutoweka ndani ya siku chache nywele zinapochomoza upya.

“Kunyoa hupunguza mabaki ya jasho na bakteria kwa muda mfupi, lakini si suluhisho la kudumu,” inaeleza sehemu ya utafiti huo.

Kwa mujibu wa wanasayansi hao, nywele zinaporudi, huanza tena kushika kemikali na jasho linalochangia harufu ya mwili, hivyo kurejesha hali ya awali.

Utafiti huo unaonesha kuwa kunyoa pekee si tiba ya harufu ya mwili, bali kinachotakiwa ni usafi wa mara kwa mara.

Nywele za kwapa si kero kama baadhi ya watu wanavyodhani. Zina faida nyingi kiafya kutoka kulinda ngozi, kupunguza msuguano, kudhibiti joto, hadi kusaidia katika mawasiliano ya kimaumbile. Badala ya kuzipuuza au kuondoa kabisa, ni busara kuzitunza kwa njia sahihi.

Mwili wa binadamu umetengenezwa kwa hekima kubwa, na kila sehemu, ikiwemo nywele za kwapa, ina jukumu maalum katika kuhakikisha afya na ustawi wa mwili kwa ujumla.

Athari za kunyoa mara kwa mara

Utafiti wa kimataifa unaoitwa ‘Athari za kunyoa katika tabaka la juu la ngozi ya kwapa, umeonesha kuwa kunyoa mara kwa mara kunaweza kuondoa sehemu ya tabaka la juu la ngozi na kusababisha kuwasha, ingawa hakubadilishi sana uimara wa kizuizi cha ngozi.

Utafiti huo ulifanywa mwaka 2003 na kuchapishwa katika jarida moja la kimataifa la sayansi ya vipodozi.

Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti, watafiti walichunguza namna unyoaji unavyoathiri tabaka la juu la ngozi ambalo hulinda mwili dhidi ya msuguano, vijidudu na chembe hatarishi.

Vipimo vilifanywa kabla na baada ya kunyoa ili kubaini mabadiliko katika uimara wa ngozi, unyeti, unyevunyevu na hali ya kukaza kwa ngozi.

Utafiti ulibaini kunyoa huondoa sehemu ya tabaka la juu la ngozi pamoja na nywele na kuacha ngozi ikiwa dhaifu kwa muda mfupi.

Watu wanaonyoa mara kwa mara waliathirika zaidi kwa kuchomachoma, kuwasha na msongamano wa ngozi. Viashiria vya uimara wa kizuizi cha ngozi havikubadilika kwa kiwango kikubwa, ikimaanisha ulinzi wa ngozi kwa ujumla unabaki thabiti licha ya msuguano.

Watafiti wanasema kuwa matokeo haya yanaonyesha umuhimu wa mbinu salama za kunyoa, hasa kwa maeneo nyeti kama kwapa, na matumizi ya bidhaa zinazolainisha na kutuliza ngozi.