Shinyanga. Taka za kielektroniki zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu na mazingira nchini, huku uelewa wa jamii kuhusu madhara yake ukiwa bado mdogo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa taka hizi zina kemikali hatarishi zinazoweza kusababisha saratani, matatizo ya mfumo wa neva na uharibifu wa mazingira.
Taka za kielektroniki ni vifaa vilivyokwisha kutumika au kuharibika kama simu, kompyuta, runinga na redio. Vifaa hivyo hubeba madini hatarishi yakiwamo zebaki, kadminamu na kromu, ambayo yakitupwa ovyo huingia kwenye udongo, maji na hewa, hivyo kuhatarisha afya ya binadamu na viumbe hai.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, mwaka 2020 dunia ilizalisha tani milioni 50 za taka za kielektroniki. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazochangia ongezeko hilo.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), Dk Ally Simba, anasema ripoti ya Taifa ya Taka za Kielektroniki ya Tanzania Bara ya mwaka 2019 (NBS), inaonyesha kuwa mwaka 2007 nchi ilizalisha tani 12,500, kiasi ambacho kiliongezeka hadi tani 35,800 mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, ongezeko hilo linachochewa na matumizi makubwa ya bidhaa za kielektroniki, hususan simu za mkononi, kompyuta, runinga na redio.
Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) inakadiria kuwa taka hizi zina thamani ya dola bilioni 62 (takribani Sh trilioni 142.4), lakini ni asilimia 20 pekee ndizo hurejeshwa rasmi kwa ajili ya kuchakatwa.
Uelewa mdogo, hatari kubwa
Utafiti wa Mwananchi umebaini kuwa jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya taka za kielektroniki.
Ofisa afya na mazingira Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu, anasema taka hizi ni hatari kwa ustawi wa viumbe hai na zinaweza kusababisha madhara ya muda mfupi na mrefu endapo hazitadhibitiwa ipasavyo.
“Jamii ipo hatarini kwa kukosa elimu sahihi ya ukusanyaji, utunzaji na uteketezaji wa taka hizi,” anasema.
Anaongeza kuwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ni watoto, wafanyakazi wa maeneo ya taka, wakazi wa karibu na vizimba vya taka, mafundi wa vifaa chakavu na wajawazito.
“Fundi anaweza kuwa na vifaa vingi vilivyoharibika. Anachukua kifaa kimoja kumsaidia mteja na vingine kubaki hapo. Kundi hili liko hatarini zaidi kuathiriwa na kemikali,” anasema.
Makungu anashauri Serikali na wadau kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na uteketezaji, kuhamasisha utenganishaji wa taka za kielektroniki na taka nyingine, pamoja na kutoa elimu endelevu kwa jamii.
Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzania Environment Initiative (TEI), Bakari Juma, anasema Manispaa ya Kahama imekumbwa na changamoto ya utupwaji ovyo wa taka za kielektroniki, hususan kwenye Bwawa la Nyihogo.
“Wavuvi wanaendelea na shughuli zao huku taka zikitupwa kwenye maji na maeneo yasiyo rasmi,” anasema.
Hata hivyo, anasema elimu kwa jamii imeanza kuzaa matunda, huku baadhi ya vijana wakijitokeza kukusanya taka hizo na kuzipeleka viwandani kwa ajili ya kuchakatwa upya.
Hatua hiyo anasema imesaidia kupunguza utupwaji holela uliokuwa umegeuza bwawa kuwa dampo.
Madhara ya kiafya na kimazingira
Mkemia kutoka Shinyanga, Method Kagaye, anaeleza kuwa taka za kielektroniki zina madini hatarishi kama zebaki, risasi, kadminamu, kromu na arseniki.
Madini haya yanaweza kusababisha madhara makubwa yakiwamo matatizo ya mfumo wa neva, figo, damu, macho, mifupa, udumavu kwa watoto, matatizo ya uzazi na hata kusahau.
Kwa mazingira, madhara ni pamoja na uchafuzi wa udongo na maji, kuathiri viumbe wa majini na kupotea kwa bioanuwai.
Kagaye anaonya kuwa sumu hizi huingia mwilini kupitia chakula, hewa au kwa kugusana nazo moja kwa moja.
“Mtu akivuta au kugusana na sumu hizi anapaswa kuwahi kituo cha afya. Ikiingia machoni, aoshwe kwa maji safi mengi kwa dakika 15 hadi 20,” anashauri.
Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kahama, Emmanuel Chiwinda, anasema kwa kiasi kikubwa taka hizi hukusanywa na vijana wanaoziona kama fursa ya kiuchumi.
Licha ya kukosekana kwa sheria ndogo maalumu, manispaa inaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya kaya kupitia vyombo vya habari na mikutano ya jamii.
“Tunawahamasisha wananchi kuvaa kinga wanaposhughulika na taka hizi na kujitokeza kwenye mikutano ya elimu, kwa kuwa taarifa zinazotolewa ni kwa manufaa yao,” anasema.
Kadri matumizi ya vifaa vya kielektroniki yanavyozidi kuongezeka, ndivyo hatari ya taka zake inavyoendelea kukua.
Bila mikakati madhubuti ya ukusanyaji, uchakataji na elimu kwa jamii, taka za kielektroniki zitaendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka kwa afya ya binadamu na mustakabali wa mazingira.