Dar es Salaam. Jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Bandari ya Dar es Salaam zinatarajiwa kuimarika, baada ya Serikali kutangaza mpango wa kuboresha Barabara ya Nelson Mandela inayounganisha eneo la bandari na Barabara ya Morogoro.
Barabara ya Morogoro ni lango kuu la usafirishaji kuelekea mikoa ya ndani ya nchi na mataifa jirani yasiyo na bandari, yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Zambia, Uganda, Malawi na Zimbabwe.
Wakala wa Barabara za Tanzania (Tanroads) umetangaza mpango wa kuboresha Barabara ya Mandela kuanzia Kivuko cha Kijazi hadi Daraja la Nyerere (Kigamboni), sambamba na kuimarisha njia za kuingia na kutoka Bandari ya Dar es Salaam.
Kupitia mradi huo, barabara hiyo itapanuliwa kuwa na njia nane; sita za magari ya kawaida, tatu kila upande, na njia mbili maalum za mabasi yaendayo haraka (BRT), moja kila upande.
Maofisa wanasema mradi huo utapunguza msongamano sugu ambao kwa muda mrefu umekuwa ukikwamisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda maeneo ya ndani ya nchi na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Msongamano wa magari umeendelea kusababisha gharama kubwa za kijamii, kiuchumi na kimazingira, zikiwemo kupotea kwa saa za kazi, kuongezeka kwa muda wa safari na kupungua kwa muda wa mapumziko kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Aidha, msongamano wa muda mrefu unaathiri juhudi za kimataifa za kupunguza uchafuzi wa mazingira, kwani magari yanapokaa barabarani bila kusogea hutoa hewa chafu zaidi, ikiwemo dioksidi kaboni.
Kwa mujibu wa ripoti ya Traffic Time Index (TTI) ya Machi 2025, safari ambayo kawaida ingetakiwa kuchukua dakika 30 jijini Dar es Salaam huweza kuchukua hadi dakika 70 wakati wa msongamano.
Kwa wastani, wasafiri hupoteza takribani saa 2.5 kila siku, sawa na karibu siku tatu kamili za kazi ndani ya wiki mbili.
Safari kati ya Kivuko cha Kijazi na Uhasibu, Temeke, inaweza kuchukua hadi saa mbili badala ya dakika 15 zinazohitajika katika hali ya kawaida bila msongamano.
Mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alionya kuwa msongamano wa magari ulikuwa unaigharimu nchi takribani Sh4 bilioni kwa siku, sawa na Sh1.44 trilioni kwa mwaka, kutokana na upotevu wa uzalishaji, matumizi makubwa ya mafuta na athari za kimazingira.
Akizungumza na The Citizen kwa mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Ephatar Mlavi, amesema taasisi hiyo inakamilisha taratibu za ndani na inatarajia kutangaza zabuni kwa wakandarasi kati ya mwishoni mwa Februari na Machi.
Mlavi amesema Barabara ya Mandela kuwa miongoni mwa mishipa muhimu zaidi ya usafiri jijini Dar es Salaam.
“Tunatarajia kusaini mkataba wa ujenzi wa Awamu ya Tano ya BRT na upanuzi wa Barabara ya Mandela hadi kuwa na njia tatu kila upande, sawa na ilivyo Barabara ya Morogoro,” amesema.
Amesema kipande cha Barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo Kijazi hadi Kimara kimekamilika kwa takribani asilimia 80, huku kazi zinazoendelea zikihusisha barabara za huduma, miundombinu ya watembea kwa miguu, mifumo ya maji ya mvua na uwekaji wa tabaka la mwisho la lami.
Taarifa ya Barabara ya Morogoro
Amesema upanuzi wa Barabara ya Morogoro hadi kuwa na njia nane, ikijumuisha BRT, unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu, huku uzinduzi rasmi ukipangwa kufanyika Septemba.
“Kwa sasa, msongamano wa magari kwenye Barabara ya Morogoro unatokana zaidi na uzembe wa madereva kuliko ukosefu wa uwezo wa barabara,” amesema Mlavi, akiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Amesema Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya kisasa, ambayo inapaswa kulindwa na watumiaji wote wa barabara.
Kwa mujibu wake, upanuzi wa kipande cha Ubungo hadi Kimara umepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari, ambao hapo awali ulizidi saa mbili wakati wa msongamano.
“Maboresho haya yamewanufaisha hasa madereva wa malori yanayosafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya ndani na nchi jirani zisizo na bandari, hivyo kurahisisha shughuli za kiuchumi,” amesema.
Awamu nyingine za BRT
Akizungumzia maendeleo ya miradi mingine ya BRT, Mlavi amesema Awamu ya Tatu imekamilika kwa takribani asilimia 90, huku Awamu ya Nne ikiwa imefikia asilimia 60.
Awamu ya Tatu ya BRT inapita katikati ya jiji, ikijumuisha Kariakoo na Posta hadi Gongo la Mboto, huku Awamu ya Nne ikiunganisha Tegeta na Posta pamoja na Ubungo hadi Mwenge.
Ameeleza Awamu ya Kwanza na ya Pili tayari zinafanya kazi, huku jitihada zikiendelea kuboresha ubora wa huduma na uhakika wa usafiri.
AFCON 2027
Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) la 36 mwaka 2027, pamoja na Kenya na Uganda, ambapo mamlaka za Tanzania zinahakikisha miundombinu ya usafiri inakuwa imara kabla ya mashindano hayo.
Maoni ya wadau
Dereva wa basi la mikoani, Musa Lipembe, amesema kupungua kwa msongamano kwenye Barabara za Mandela na Morogoro kutapunguza shinikizo kwenye njia mbadala.
“Njia hii mara nyingi hutawaliwa na malori makubwa, mengine yakipata hitilafu. Kwa kuwa na njia tatu, magari mengine yataweza kuyapita kwa usalama zaidi, hivyo kuokoa muda kwa mabasi na magari binafsi,” amesema.
Mfanyakazi wa sekta binafsi, aliyeomba kutotajwa jina, amesema upanuzi wa Barabara ya Mandela utabadilisha kabisa usafiri wa mijini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Ili kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050, Tanzania inahitaji usafirishaji wa haraka na wenye ufanisi wa bidhaa. Kuondoa vikwazo vinavyokwamisha usafiri ni jambo la msingi,” amesema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Joseph Priscus, amesema kukamilika kwa kazi za Barabara ya Morogoro kati ya Ubungo na Kimara, pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Mandela, kutapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za mafuta ambazo waendeshaji wa mabasi wamekuwa wakizipata kutokana na msongamano na uchakavu wa magari.
Ameongeza kuwa upanuzi hadi njia nane utaongeza pia muda wa matumizi ya barabara, kwani magari makubwa yanaposimama muda mrefu kwenye msongamano husababisha mashimo na majeraha kwenye lami.
“Hii ni hatua chanya itakayosaidia ukuaji wa uchumi,” amesema.
Priscus ameiomba Serikali kuipa kipaumbele Barabara ya Chalinze–Morogoro, ambayo kwa sasa ina njia mbili pekee na hukumbwa mara kwa mara na msongamano na ajali.
Kwa kuwa Barabara ya Morogoro ni mhimili muhimu wa usafirishaji kwa nchi tano jirani, uboreshaji wa eneo la Chalinze ni muhimu ili kuhakikisha mizigo inawasilishwa kwa wakati na biashara za kikanda zinaendelea kwa ufanisi.
Maofisa pia wanatarajia mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kuongezeka, kutokana na kuboreshwa kwa njia za kuingia na kutoka bandarini, jambo litakalopunguza ucheleweshaji wa usafirishaji na kuongeza ufanisi wa mizigo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Madogo na ya Kati Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabaan, amesema suluhisho la kudumu linahitaji Bandari Kavu ya Kwala kuanza kufanya kazi kikamilifu kulingana na maelekezo ya Rais.
Ameonya vikwazo vikubwa katika kipande cha Kibaha–Morogoro vimesababisha baadhi ya malori kukwama barabarani hadi siku 17.