Dar es Salaam. Wamachinga wanaofanya biashara katika mitaa ya kuingia Soko Kuu la Kariakoo wameondoa meza na mizigo yao kupisha maandalizi ya uzinduzi wa soko hilo unaotarajiwa kufanyika Jumapili, Februari 8, 2026.
Soko hilo limekuwa kwenye ukarabati kwa muda mrefu tangu lilipoteketea kwa moto mwaka 2021 na kuteketeza mali zote za wafanyabiashara waliokuwemo ndani ya soko ambapo Serikali ilitoa Sh28 bilioni ili kulijenga upya.
Katika kipindi chote hicho, wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao sokoni hapo walihamishwa katika masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex ili kupisha ujenzi.
Leo Februari 6, 2026, Mwananchi limetembelea eneo la Soko la Kariakoo na kushuhudia shughuli ya usafi ikiendelea huku mitaa miwili ya Mkunguni na Nyamwezi ikiwa tayari imeondolewa mabati yaliyokuwa yamezungushwa katika eneo la soko hilo.
Wafanyabiashara wakiangalia eneo walipokuwa wameweka meza zao za biashara kabla ya uzio wa mabati uliokuwa umezingushiwa katika Soko Kuu la Kariakoo kuondolewa Februari 5, 2026 kwa ajili yabuzinduzi wake
Hata hivyo, kwa upande wa mitaa ya Tandamti, Swahili na Sikukuu, mabati hayo bado hayajaondolewa, hali inayoonyesha kuwa maandalizi yanaendelea kwa awamu.
Pia, Mwananchi limeshuhudia wafanyabiashara waliokuwa wanapanga bidhaa zao katika mitaa ya kuingia soko kuu wakiwa pembeni kuangalia kinachoendelea.
Mbali na wafanyabiashara kukaa pembeni, wapo wapita njia nao walikuwa wanashangaa na kuulizia wenyeji kuhusu soko hilo na kupewa majibu ya “Uzinduzi umefika wenye soko lao wanarudi”.
Uzio wa mabati uliokuwa unatumiwa na wafanyabiashara wadogo maarufu machinga katika Soko Kuu la Kariakoo umeondolewa mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni kuelekea uzinduzi wa soko hilo unaotarajiwa kufanyika Februari 8,2026
Hata hivyo, haikuishia kuangalia, pia, kuongea mambo mbalimbali kuhusu kuondolewa kwao eneo hilo kwani hakuna aliyepata madhara yoyote kwa kuwa walitangaziwa tangu jana Februari 5, 2026 asubuhi kwamba wasifungue biashara kutakuwa na shughuli ya usafi wa eneo hilo.
Kutokana na tangazo hilo, wafanyabiashara hao waliondoa meza zao pamoja na kutolaza mizigo yao nje kama ilivyokuwa awali kwa kuwa shughuli za uondoaji mabati ilifanyika kuanzia siku hiyo mchana hadi usiku.
Maandalizi wa uzinduzi wa soko hilo yananaendelea kwani tayari maturubai yamewekwa katika eneo ambalo utafanyika mkutano wa uzinduzi katika Mtaa wa Mkunguni na usafi umefanyika katika maeneo ya jirani na soko hilo ikiwemo mitaro ya maji machafu imesafishwa pamoja na ule wa Mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni ambao ulilipotiwa na Mwananchi siku kadhaa zilizopita.
Agosti 25, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipohojiwa na Mwananchi sababu ya danada ya ufunguzi wa soko hilo, alijibu kwamba mkandarasi alikuwa hajamaliziwa sehemu ya fedha zake, lakini alilipwa wiki kadhaa na muda wowote angewakabidhi soko hilo.
Alisema baada ya kukamilika hilo soko lingefunguliwa Septemba 15, 2025 na alieleza wafanyabiashara walishaonesha maeneo yao wakiwamo wale waliopata maeneo ya kukodi kwa njia ya mnada mtandaoni.
Akizungumza na Mwananchi leo, Februari 6, 2026, Mwenyekiti wa Machinga Kariakoo na Makamu Mwenyekiti Taifa, Stephen Lusinde amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha usafi wa mazingira, usalama na mwonekano mzuri wa soko kabla ya uzinduzi huo unaotarajiwa kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema wafanyabiashara walitaarifiwa tangu jana asubuhi na kukumbushwa tena jioni ili wafunge biashara zao mapema na kuondoa mizigo yao wakati wa usiku.
“Tuliwaelekeza wafunge jioni na waondoe mizigo yao usiku. Wengi walitii na hakuna aliyelaza mzigo wake katika eneo hilo na kama wapo watatoa baadaye kwa sababu mitaa inatakiwa kuwa safi,” amesema Lusinde.
Uzio wa mabati uliokuwa unatumiwa na wafanyabiashara wadogo maarufu machinga katika Soko Kuu la Kariakoo umeondolewa mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni kuelekea uzinduzi wa soko hilo unaotarajiwa kufanyika Februari 8, 2026
Kwa mujibu wa Lusinde, mitaa iliyopisha kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi ni pamoja na Nyamwezi, Mkuguni, Tandamti, Msimbazi na Pemba kipande. Amesema kuwa maeneo yanayotakiwa kuwa wazi kwa muda.
Amesema hatua hiyo haimaanishi kuondolewa kwa machinga moja kwa moja, bali ni mpango wa muda kuelekea uzinduzi wa soko hilo.
“Baada ya uzinduzi, machinga watarudi kufanya biashara kwa utaratibu utakaopangwa. Endapo kutakuwa na mitaa itakayopaswa kubaki wazi kabisa, tutakaa na mamlaka husika kuwatafutia maeneo mbadala,” amesema.
Lusinde amesema machinga hao wana familia na hutegemea biashara hizo kwa maisha yao ya kila siku.
“Hizi biashara ndizo ofisi zao, hivyo lazima tushirikiane na mamlaka ili maisha yaendelee,” amesema.
Mfanyabiashara wa maturubai Mtaa wa Pemba, Khalid Twalib amesema walitangaziwa jana asubuhi waondoe meza zao kwa kuwa kutakuwa na uzinduzi wa soko hilo Jumapili na asilimia kubwa walifanya hivyo hususani waliokuwa wameweka kwenye uzio wa soko.
Wafanyabiashara wakiangalia eneo walipokuwa wameweka meza zao za biashara kabla ya uzio wa mabati uliokuwa umezingushiwa katika Soko Kuu la Kariakoo kuondolewa Februari 5, 2026 kwa ajili yabuzinduzi wake
“Tulitangaziwa jana na wafanyabiashara wa eneo la mabati, wote walitoa na hawakulaza mizigo yao eneo hilo kwa sababu walikuwa na taarifa na shughuli hii ya kuondoa mabati ilianza jana mchana,” amesema Twalib.
Amesema kwa sasa wanasubiri na wenzao wa Mtaa wa Pemba kama wataambiwa waondoe meza zao wapo tayari na hicho ndiyo chanzo cha kutofungua biashara zao tangu wamefika.