Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu amewataka Watanzania kuionea fahari lugha yao ya Kiswahili kama utambulisho wao kwani mataifa mengi duniani yanatumia lugha zao badala ya Kiingereza.
Zungu ametoa wito huo leo Februari 6, 2026 bungeni jijini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu, akifafanua mjadala ulioibuka mitandaoni baada ya Mbunge wa Ukonga (ACT Wazalendo), Bakari Shingo kushindwa kujieleza kwa Kiingereza wakati akiomba kura kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Jukwaa la Nchi za Maziwa Makuu.
Jana, mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma aliomba mwongozo wa Spika akihoji kwanini watu wasiojua Kiswahili wananyimwa fursa ya kuiwakilisha Tanzania kwenye majukwaa hayo na kwanini yeye (Shingo) aende licha ya kuwa hajui lugha hiyo.
Katika majibu yake, Spika Zungu alisema hilo ni suala la demokrasia kwa sababu wabunge wamempigia kura tofauti na utaratibu wa zamani ambapo wawakilishi walikuwa wanateuliwa. Amesema nafasi ya upinzani ilikuwa moja tu na mgombea alikuwa mmoja tu.
Hata hivyo, leo, Spika Zungu ameanza kwa kusema jana baada ya mwongozo wa Musukuma, kwenye mitandao ya kijamii zimetoka taarifa nyingi za kutumia lugha zisizo za kistaarabu kwa kuwakashifu na kuwasema vibaya wabunge.
“Nataka niwaambie wananchi, tuwe na ufahari na Kiswahili. Tujivunie. Katika bara zima la Afrika, ni Taifa moja tu la Tanzania ambalo tuna lugha moja ya taifa na wote tunazungumza lugha moja.
“Mnaotumia mitandao kukashifu au kudharau na kusema kuwa wenzetu majirani wasije wakasikia taarifa hizi, haipendezi na ni kujidhalilisha tu,” amesema Zungu huku wabunge wakishangilia kwa wakigonga meza.
Zungu ameongeza kuwa: “Shingo ni mbunge wa Dar es Salaam, na mimi namjua, hana shida na lugha ya Kiingereza. Binadamu hukutwa na shinikizo, kapanic, ndiyo mara yake ya kwanza, kuna maradhi mengine sisi hatujui tunatembea nayo. Kuna Post-stress somatic syndrome, unajikuta tu unashikwa na hofu.”
Amewahakikishia wananchi na wabunge kwamba uwakilishi kwenye nchi zingine hauzingatii lugha ya Kiingereza na kwa vile Kiswahili sasa kinatambulika kimataifa, kutakuwa na wakarimani, unasema Kiswahili, wanatafsiri kwa lugha nyingine.
“Na siyo kila mtu anajua Kiingereza, kuna mataifa ya Asia hayazungumzi Kiingereza, kuna Mataifa ya South America (Amerika Kusini) hayazungumzi Kiingereza, kuna Mataifa ya Afrika wanazungumza lugha za kwao badala ya Kiingereza…
“Kwa hiyo niwaombe sana, tuwe kila kitu tunaponda tu, huna mahali pa kwenda Zaidi ya Tanzania. Niwaombe sana watu wa mitandao, vitu kama hivi havipendezi, havileti heshima kwa Taifa,” amesema Zungu.