Waziri Riziki awataadharisha wawekezaji kwenye sanaa Zanzibar

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Riziki Pembe, ametoa wito kwa wawekezaji kwenye sanaa Zanzibar kuzingatia mila na tamaduni.

Akiwa kwenye tamasha la Sauti za Busara, Februari 5,2026 Riziki amesema miundombinu ya Zanzibar ni rafiki kwa wawekezaji wa aina zote ikiwemo biashara, kisanaa ndiyo maana hata filamu ya The Royal Tour imefanyika pia ndani ya Zanzibar.

“Rais wetu wa Zanzibar amekuwa akiweka miundombinu rafiki, kwa ajili  ya uwekezaji wa kila namna tukija kwenye sanaa, mazingira yote yapo inategemea na seti ambayo wewe unataka kufanya na wapi. 

“Yeyote anayetaka kuja kuwekeza kwenye tamasha lolote lile fursa zote zipo. Na tunawakaribisha sana kwa sababu hakuna vizuizi, muhimu ufuate mila, silika na masharti kwa sababu kila sehemu kuna sheria zake na tamaduni zake. Huwezi kuja kufanya tamasha ukawa umetuvalia nusu uchi maana tutakutoa hapohapo wakati tamasha lako linaendelea. Wafuate taratibu zetu za kisanaa zipoje ili wasije kwenda kinyume,”amesema

Akizungumzia tamasha la Sauti za Busara amesema limetanua fursa nyingi kwani limekutanisha wafanyabiashara mbalimbali.

“Tamasha limeanza nikiri kwamba ni nzuri. Ilizoeleka linafanyika Ngome Kongwe, kwa mara ya kwanza limefanyika Mnazi Mmoja. Hata washiriki waliopo wanajitawanya wana nafasi nzuri hewa safi lakini limeleta mpaka wafanyabiashara.

“Ingawa na kule fursa zilikuwepo lakini huku imekuja kwa upana zaidi. Watu wamefurika kwa uharaka kwa sababu ni njiani. Washiriki wamejitokeza hii inaonesha Tanzania kuna amani sana inayosimamiwa na Dk Hussein Mwinyi  na Dk Samia Suluhu Hassan

“Mimi Waziri mwenye dhamana Zanzibar niendelee kuwaambia sisi serikali tutaendelea kushirikiana nao hawa. Lakini na wengine wote ambao watakuja kufanya matamasha yao Zanzibar kuwaambia milango ipo wazi na fursa zipo nyingi,”amesema