Kigogo afichua yanayoendelea Simba | Mwanaspoti

INGAWA Simba inamiliki pointi moja katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika, kigogo mmoja wa timu hiyo amesema wamejipanga kuonyesha ushindani mwanzo, mwisho bila kujali nafasi waliyopo sasa.

Kigogo huyo amesema kila kitu kipo sawa na wachezaji wamejengwa kisaikolojia kupambania thamani zao na heshima ya klabu ya Simba, kutambua ni mapito yanayoleta chachu ya kujipanga zaidi. 

“Kila kitu kinaendelea vizuri kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo, tunatambua itakuwa ngumu lakini kocha Steve Barker anaendelea kuwajenga wachezaji kimazoezi,” amesema kigogo huyo na kuongeza; 

PUMZ 04


“Ni kweli siyo kawaida ya Simba kuwa na matokeo kama haya katika michuano ya CAF, lakini kila kitu tunachukulia kwa upande wa kujipanga zaidi ili kufanya vizuri zaidi katika michuano mingine.”

Kigogo huyo amesema kuna wachezaji waliowaacha jijini Dar es Salaam wanaouguza majeraha ambao ni Abdulrazack Hamza, Wilson Nangu aliyeumia dhidi ya Esperance, Mohamed Bajaber (aliumia dhidi ya Mtibwa Sugar), Yakoub Suleiman (alipata majeraha akiwa na Taifa Stars ikijiandaa na mechi ya AFCON dhidi ya Nigeria).

PUMZ 05


“Wachezaji wanaofanya mazoezi chini ya uangalizi wa madaktari ni Nangu, Hamza na Bajaber, kuhusu Yakoub karejeshwa katika mazoezi ya timu lakini anasimamiwa na kocha wa viungo,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.

“Yakoub hajaambatana na timu kwani anatafuta ufiti, lakini tukirejea Dar es Salaam anakuwepo mazoezini, kwani majeraha yake hayakuwa makubwa.”

PUMZ 06


Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Amir Maftah amesema: “Haijalishi Simba ipo nafasi gani, wachezaji wapambane kuhakikisha wanapata ushindi kwa mechi zilizosalia ili kujenga heshima ya brandi ya klabu.” Mtazamo wake uliungwa mkono na kiungo wa zamani wa timu hiyo, Shabaan Kisiga ‘Marlone’. aliyesema: “Ni kweli nafasi iliyopo Simba ni maumivu kwa mashabiki, lakini katika mechi mbili zilizosalia wachezaji wapambane kwa hali na mali ili kushinda bila kujali zitaamua nini.”