YANGA kesho Jumamosi itakuwa Uwanja wa Prince Moulay Abdellah uliopo Rabat nchini Morocco kucheza mechi ya tano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kundi B dhidi ya wenyeji wao, AS FAR Rabat.
Wakati hesabu zikiwa katika mechi hiyo, taarifa zimeibuka kwamba, kuna straika imempiga marufuku kucheza mechi yao ya mwisho kuhitimisha makundi dhidi ya JS Kabylie.
Aliyepigwa marufuku hayo ni Celestine Ecua ambaye anaichezea JS Kabylie kwa mkopo wa miezi sita akitokea Yanga aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu.
Ecua tangu atue JS Kabylie kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu uliofungwa Januari 2026 hapa nchini amefanikiwa kucheza mechi moja hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat na chama lake kupoteza ugenini kwa bao 1-0.
Taarifa kutoka Yanga zinasema kwamba, mkataba huo wa mkopo kwenda JS Kabylie, una kipengele maalum kinachomzuia kucheza dhidi ya klabu aliyotoka.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Ecua hataruhusiwa kushiriki mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, JS Kabylie ikiifuata Yanga, jambo ambalo limeipa nafuu klabu hiyo ya Jangwani katika harakati zake za kutinga robo fainali.
Hatua hiyo imekuja tofauti kabisa na mikataba ya mikopo ya wachezaji wengine wa Yanga, akiwemo Denis Nkane (TRA United) na Offen Chikola (Singida Black Stars), ambao walipewa ruhusa kucheza dhidi ya timu zao za sasa pale Yanga itakapokutana na klabu walizokuwa wamepelekwa kwa mkopo.
Vyanzo vya kuaminika ndani ya Yanga vinaeleza kuwa, uongozi wa klabu hiyo uliweka msimamo mkali kwenye mazungumzo ya mkopo wa Ecua ili asije akapata nafasi na kuwaumiza.
“Sakata la Ecua limeonesha mabadiliko ya kifikra kwa uongozi wa Yanga katika masuala ya mikataba ya mikopo, huku klabu hiyo ikionekana sasa kuwa makini zaidi katika kulinda maslahi yake ndani na nje ya uwanja,” amesema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Kanuni za CAF zinaeleza wazi kuwa, mchezaji wa mkopo anaruhusiwa kucheza dhidi ya timu aliyotoka iwapo hakuna kipengele maalum kinachomzuia na klabu yake, jambo lililoifanya Yanga kuweka zuio kisheria.
Kwa JS Kabylie, kutomchezesha Ecua kwenye mechi hiyo itakuwa pigo kubwa, ikizingatiwa kuwa kiungo huyo amesajiliwa ili kuipa nguvu timu hiyo katika michuano ya kimataifa ambayo timu hiyo inashiriki.
Kwa upande wa Yanga, hatua hiyo inaonekana kuwa faida ya kimkakati, hasa katika mechi ya mwisho ya makundi ambayo mara nyingi huamua hatma ya klabu kutinga robo fainali au kuaga mashindano.
Ecua alitua Yanga msimu huu akitokea ASEC Mimosas, amekaa kwa takribani miezi sita na kutolewa kwa mkopo.
Yanga ilifika Morocco juzi Jumatano na kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya FAR Rabat utakaochezwa kesho Jumamosi saa 4:00 Usiku.
Akizungumzia hali ya kikosi baada ya kufika Morocco, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema: “Hali ya hewa ya jana (juzi) ni ya baridi nyuzi joto 17 ikiwa pia ni msimu wa mvua ingawa hali ya hewa ni ya kubadilikabadilika, lakini kiufupi sio mbaya. Jambo jema ni kwamba katika kikosi ambacho kilisafiri kuja hapa wote wapo salama na afya njema.”
Hii ni kwa mara ya kwanza Yanga inatua katika Jiji la Rabat, lakini ni mara ya pili kwa timu hiyo kufika Morocco kucheza mechi za CAF ikifanya hivyo mara ya kwanza mwaka 1998 ambapo ilimenyana na Raja Casablanca kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, mechi ikipigwa Jiji la Casablanca na Yanga kupoteza kwa mabao 6-0, baada ya nyumbani kutoka sare ya 3-3.
Katika kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano sawa na AS FAR Rabat, huku Al Ahly ikiongoza na pointi nane, wakati JS Kabylie inaburuza mkia ikikusanya pointi mbili. Zote zimecheza mechi nne, bado mbili kukamilisha makundi.