KOCHA Mkuu wa TRA United, Etienne Ndayiragije, amesema maboresho yaliyofanywa na kikosi hicho katika dirisha dogo la usajili yamezingatia mahitaji, na ana matarajio makubwa na nyota wote waliojiunga na timu hiyo.
TRA imewasajili Mzamiru Yassin, Denis Nkane na Chamou Karaboue, wote kwa mkopo wa miezi sita pamoja na Valentine Nouma, Jamal Issah, Muhsin Malima na Mussa Halili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ndayiragije amesema usajili uliofanywa ni kwa mapendekezo yake baada ya kuona upungufu, hivyo anaamini wachezaji walioongezwa kikosini wataleta tija kwa kuipambania timu hiyo ifikie malengo.
“Huwezi kusajili wachezaji bila kuwa na mahitaji. Wamesajiliwa kwa sababu tulikuwa na uhitaji katika nafasi hizo, na naamini tumesajili kwa kuzingatia ubora. Watafanya kazi yao kwa kuhakikisha TRA United inafikia malengo,” amesema kocha huyo.
“Mpira ni mchezo wa wazi, kila mmoja atashuhudia tulichokifanya kikitimiza malengo ya timu. Namshukuru Mungu wachezaji wapo katika hali nzuri na wanaendelea na maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Mbeya City.”
Kocha huyo amesema baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, timu imerejea uwanjani kwa mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya wiki hii.
“Hautakuwa mchezo rahisi, hakuna timu iliyo kwa ajili ya kugawa pointi kwa mpinzani, hivyo tunatarajia ushindani mkubwa. Tumejiandaa kushindana, lengo ni kutokurudia makosa tuliyoyafanya kwenye mechi zilizopita,” amesema.