WAZEE wa mapigo na mwendo, Mashujaa FC, wameanza mchakato wa kumchukua kocha Fikiri Elias ili kumrithi Salum Mayanga, baada ya uongozi kutoridhishwa na mwenendo wa timu.
Mashujaa kwa sasa ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 12, ambapo imeshinda tatu, sare nne na kupoteza tano, matokeo ambayo yamekuwa chanzo cha presha kubwa kwa benchi la ufundi, hali iliyowafanya viongozi kuanza kufanya tathmini ya kina juu ya hatma ya kocha Mayanga.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, uongozi wa klabu unamtazama Elias kutokana na uzoefu wake; kocha huyo aliwahi kuifundisha Coastal Union.
Chanzo hicho kilieleza kuwa mazungumzo ya awali kati ya pande hizo mbili yameanza na yanaendelea vizuri, na huenda baada ya mechi dhidi ya Prisons timu hiyo ikafanya uamuzi.
“Baada ya mwenendo kutoridhisha, viongozi wameona ni muhimu kufanya mabadiliko mapema. Fikiri anaifahamu ligi na anaweza kuisaidia timu kurejea kwenye ushindani,” kimesema chanzo hicho.
“Kwa hiyo baada ya mechi dhidi ya Prisons kutakuwa na uamuzi, upande wa kocha na timu kuona uwezekano wa kufanya kazi pamoja ili kuinusuru timu isifanye vibaya.”
Mayanga alijiunga na Mashujaa Machi 21, 2025 akitokea Mbeya City, akirithi mikoba ya Abdallah Mohamed ‘Baresi’, siku chache baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0 na Singida Black Stars Februari 26, 2025.