Kaya masikini 11,276 Geita kunufaika na bima ya afya bure

Geita. Serikali mkoani Geita imezindua mpango wa kitaifa wa Bima ya Afya kwa Wote katika awamu ya kwanza ambapo kaya 11,276 zenye jumla ya watu 69,651, zinatarajia kuanza kunufaika na mpango huo kupitia kitita cha huduma muhimu kwa kaya zisizo na uwezo.

Kundi hilo katika awamu ya kwanza ni lile linalowahusu watu walio katika mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ambapo wanapatiwa bima za afya bure ili kuwarahisishia wananchi hao kumudu gharama za matibabu.

Uzinduzi huo kimkoa umefanyika leo Februari 6, 2026 katika kata ya Ludete, mji mdogo wa Katoro, ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Komba ametoa rai kwa maofisa maendeleo ya jamii na maofisa watendaji wa kata na vijiji, kutoa ushirikiano kwa watendaji kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika kuharakisha mchakato wa usajili kukamilika haraka.

Aidha, Komba amewatahadharisha wananchi kuwa mchakato wote wa usajili kwa kaya hizo unafanyika bila malipo, hivyo wasikubali kutoa fedha, pia, kwa watendaji wa idara ya afya, mkuu huyo wa wilaya ameonya watumishi watakaoshindwa kutoa huduma kwa wagonjwa na kuahidi kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale watakaobainika.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akimkabidhi Kadi ya Bima ya afya mtoto ambaye ni mnufaika kupitia awamu ya kwanza kwa watoto,wazee,Wenye ulemavu na wanaoishi mazingira magumu kiuchumi,kushoto ni Mwenyekiti Mamlaka ya mji mdogo Katoro Ramadhan Mapela na kulia ni Meneja wa NHIF Mkoa wa Geita Elius Odhiambo.



“Tujipange kikamilifu kuwapokea vema na kuwahudumia, tusingependa kusikia mtu anakuja na bima ya afya halafu anakosa matibabu, hayo siyo maelekezo ya Serikali na hatutosita kuchukua hatua,” amesema Komba.

Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa usajili huo wa awali, wataendelea na usajili kwa makundi mengine katika jamii, hivyo kuitaka jamii kuona umuhimu wa kujiunga badala ya kusubiri kutoa fedha taslimu pindi wanapougua au kuuguza.

“Nitoe rai, mchakato huu utakapokuwa umekamilika na kitita hiki kuhamia kwa watu wengine, kila Mwananchi aone umuhimu wa kujitengenezea uhakika wa matibabu ndani ya kaya yake kwa kulipia Sh100,000,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Geita, Elius Odhiambo ameeleza kuwa maofisa wa mfuko huo waliopo katika halmashauri zote za mkoa huo, kwa sasa wanaendelea kukamilisha utambuzi, usajili na kutoa vitambulisho kupitia kitita cha huduma muhimu kwa kaya zisizo na uwezo kupitia ushirikiano na viongozi wa serikali za mitaa ili kuwarahisishia wanakaya kuanza kunufaika na mpango huo, akieleza kuwa bima hizo zimelipiwa na Serikali.

“Kadi ambazo zinatolewa leo ni za matibabu kwa kaya zisizo na uwezo na haimanishi kuwa kaya hizi zitalipia pesa, hapana, fedha zao zimeshalipwa na Serikali, kumuona daktari, kupata vipimo na kupata matibabu,” amesema Odhiambo.

Aidha, Odhiambo amebainisha kuwa usajili unafanyika kidijitali na vifaa vinavyotumika vina uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yote bila kujali ukosefu wa umeme au mtandao katika eneo husika kwani teknolojia yake inaruhusu kufanya kazi bila ulazima wa mtandao.

Baadhi ya wananchi wakisajiliwa kwa mfumo wa kidijitali katika mfuko wa Taifa wa Bima ya afya NHIF awamu ya kwanza mkoani Geita kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu kiuchumi.



Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk Modest Buchard amesema ili nchi yoyote iwe imara lazima wananchi wake wawe na afya njma hivyo, tayari wamejipanga kutoa huduma kwa vituo 74 kuandaliwa ili kuwarahisishia wananchi kujisajili kwa haraka.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, wameishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele watu wanaoishi katika mazingira magumu, hatua itakayowasaidia kupata matibabu kwa haraka tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kupata bima ya afya.