Zungu aonesha ‘matobo’ serikalini, amtwisha jukumu Dk Mwigulu

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu ameibua hoja kuhusu changamoto katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, akitaja uwezo mdogo wa baadhi ya benki katika mitaji ya ukopeshaji kuwa kikwazo kikuu kinachosababisha mikopo hiyo kutowafikia walengwa wengi kwa wakati.

Zungu amesema baadhi ya benki zinazoshirikiana na halmashauri hazina uwezo wa kuhudumia vikundi vyote vinavyohitaji mikopo hiyo, hali inayowaumiza wananchi wa kipato cha chini, hususan wanawake na vijana wa vijijini.

Kauli hiyo ameitoa leo Ijumaa, Februari 6, 2026, bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa benki na taasisi za fedha nchini kubadili mtazamo wao na kuacha kuweka vikwazo visivyolingana na uhalisia wa maisha ya wananchi.

Amesema dhamira ya Serikali katika mikopo hiyo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi, si kuwakatisha tamaa.

Sakata la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa mgawanyo wa 4-4-2 limechukua mjadala mpana katika Mkutano wa Pili wa Bunge la 13. Katika mjadala huo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliwahi kutoa tamko bungeni kuhusu kupunguzwa kwa masharti ya mikopo hiyo, akieleza kuwa kigezo kikubwa kitakuwa ni Kitambulisho cha Taifa (Nida).

“Hatutaweza kuwasaidia wananchi kama tutaendelea kukaa na nadharia za uchumi bila kuzingatia uhalisia wa maisha yao. Tunapozungumzia mikopo, tunazungumzia mama lishe ambaye hana hata namba ya TIN lakini ana biashara halisi. Mabenki yawajibike, yajali maisha ya watu na yawe rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini,” amesema Spika Zungu kwa msisitizo.

Aidha, ameshauri Serikali kushirikiana kwa karibu na benki pamoja na watoa huduma za kifedha ili kuondoa masharti magumu yanayozuia wananchi wengi kunufaika na mikopo hiyo.

Ameonya kuwa endapo vikwazo hivyo vitaendelea, dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi shirikishi haitafikiwa ipasavyo.

Kauli ya Spika imetokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Neema Majule, aliyehoji iwapo Serikali ina mpango wa kuanzisha mfumo madhubuti wa kupima matokeo ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ili kubaini changamoto na mafanikio yake, hasa ikizingatiwa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.

Katika swali la nyongeza, Dk Majule amesema bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi wa vijijini mkoani Dodoma kuwa mikopo hiyo haiwafikii kwa wakati, masharti ni magumu na mchakato ni mrefu.

Amehoji ni lini Serikali itaweka mfumo wa “One Stop Centre” ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuwazuia wanawake na vijana kukata tamaa.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, amekiri kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wahitaji wa mikopo hiyo.

Amesema Serikali tayari imekutana na wawakilishi wa benki ili kujadili changamoto hizo na kuweka mikakati ya maboresho.

Profesa Shemdoe amesema benki zimekubali kufanya mabadiliko na kwamba kigezo kikubwa kitakachotumika katika utoaji wa mikopo hiyo kitakuwa ni Kitambulisho cha Taifa pamoja na uwepo wa biashara halisi.

“Mheshimiwa Spika, jambo lingine tuliloliona ni sharti la watu kuwa katika vikundi. Katika maeneo mengi, ikiwamo Kariakoo, watu hukutana sokoni na si rahisi kuwa pamoja kama kikundi kimoja. Hivyo, tumeamua kwenda katika mfumo wa kukopa mtu mmoja mmoja,” amesema Profesa Shemdoe.

Ameongeza kuwa Ofisi yake tayari imefanya tathmini moja tangu kuanza kwa mfumo mpya wa utoaji mikopo, huku tathmini nyingine zikiendelea kufanyika kulingana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji, hatua inayolenga kuboresha mifumo na kuongeza ufanisi wa mikopo hiyo.

Awali, Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwagilwa, alisema hadi Januari 2026 jumla ya vikundi 24,064 vimepata mikopo ya asilimia 10. Kati ya hivyo, vikundi vya wanawake ni 13,639, vijana 8,140 na watu wenye ulemavu 2,285.

Naibu Waziri amesema Serikali imejenga uwezo kwa wasimamizi 736 wa Halmashauri na 78 wa Mikoa kuhusu usimamizi wa Mfumo wa Wezeshi, huku maboresho ya mfumo huo yakiendelea kufanyiwa kazi.

Amesema Serikali pia ilifanya uamuzi wa kimkakati wa kuhusisha mabenki katika utoaji wa mikopo hiyo, ikiwemo CRDB na NMB, kwa lengo la kuondoa masharti magumu na kuwafikia wananchi waliokuwa hawakopesheki awali.

Hata hivyo, alitaja changamoto ya vikundi vingi kukutana mijini bila wanachama kufahamiana makazi yao, hali inayosababisha ugumu katika urejeshaji wa mikopo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Serikali imesaini mikataba na benki hizo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata mikopo, sambamba na kuwawezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kuwapatia pikipiki 90, hatua itakayowawezesha kuwafikia wananchi moja kwa moja na kutoa elimu kuhusu mikopo hiyo.

Akiwasilisha hoja ya kuhitimisha shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge hilo la 13, Waziri Mkuu, Dk Nchemba, amewataka Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wabunge na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanawafuata wananchi waliko na kuzungumza nao moja kwa moja ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

Dk Mwigulu amesema wananchi wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa haraka, jambo litakalowezekana iwapo viongozi watatenga muda wa kusikiliza kero zao katika maeneo yao.

“Viongozi tengeni muda wa kuwasikiliza wananchi. Nawaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafuata wananchi na kusikiliza changamoto zao, kila mmoja kwa nafasi yake,” amesisitiza Dk Mwigulu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu huyo amerudia msimamo wa Serikali kwa viongozi wanaochukua hatua dhidi ya watumishi wazembe, akisema Serikali itaendelea kuwalinda viongozi wanaotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na haitakuwa tayari kusimama upande wa wazembe.

Amesisitiza kuwa viongozi wanaochukua hatua stahiki dhidi ya uzembe wanapaswa kuwa na imani kuwa wako salama kwani Serikali inaendelea kuwaunga mkono.

Aidha, amewakumbusha wakulima kote nchini kutumia ipasavyo mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao yanayoendana na hali ya utabiri wa hewa, pamoja na kutunza mazao kwa ajili ya akiba ya baadaye.

Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 umehitimisha rasmi shughuli zake leo, huku Mkutano wa Tatu ambao ni Bunge la Bajeti ukitarajiwa kuanza Machi 31, 2026.

Kwa mujibu wa utaratibu, Wabunge wanatarajiwa kuanza vikao vya kikanuni kabla ya kuanza rasmi kwa mkutano huo.