Baada ya kupoteza michezo miwili ya ugenini, leo Pamba Jiji imerudi nyumbani kwa kishindo baada ya kuichapa Coastal Union kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara umechezwa kuanzia saa 8 mchana, ambapo ushindi huo umeitoa Pamba katika nafasi ya tano hadi ya tatu kwenye msimamo.
Baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika bila bao, Pamba Jiji ilikuja juu kwa kasi kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji ambayo yamelipa na kuizawadia mabao matatu.
Katika mabadiliko hayo dadika ya 46 ilimtoa Yonta Camara na kuingia John Nakibinge na ile ya 69 ilimtoa Shaphan Siwa na kuingia Shassir Nahimana ambao wamebadilisha mchezo na kuleta kicheko kwa Wana TP Lindanda.
Dakika mbili tangu aingie uwanjani kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, Nahimana ameifungia Pamba Jiji bao la kwanza dakika ya 72 akimalizia mpira wa kona uliotemwa na kipa wa Coastal Union, Khatibu Mahamoud.
Dakika ya 76, Nahimana akatupia tena bao la pili akimalizia mpira uliopigwa na Zabona Mayombya na kuwababatiza mabeki wa Coastal Union.
Kabla ya filimbi ya mwisho kupulizwa, mshambuliaji raia wa Kenya, Mathew Tegis akaifungia bao la tatu Pamba Jiji kwa shuti la mbali baada ya kumchungulia kipa aliyekuwa amesogea kidogo mbele ya lango.
Kabla ya mchezo huo, Pamba Jiji ilicheza michezo minne bila ushindi tangu iliposhinda mabao 3-0 dhidi ya KMC katika uwanja huo Novemba 29, 2025 ambapo ilifungwa mabao 3-0 na JKT Tanzania, 1-1 na Mbeya City, ikachapwa 1-0 na Mtibwa Sugar na suluhu (0-0) dhidi ya Tanzania Prisons.
Kichapo cha leo ni mwendelezo wa matokeo mabaya kwa Coastal Union ambayo haijashinda tangu Novemba 26, 2025 ilipoifunga Mbeya City mabao 2-0.
Timu hiyo imetoka sare ya 1-1 na TRA United, 1-1 dhidi ya KMC, ikachapwa 1-0 na Namungo, 3-0 mbele ya Azam FC, ikapoteza 1-0 mbele ya Yanga na suluhu (0-0) dhidi ya Mashujaa FC.
Caastal Union inasalia katika nafasi ya 12 ikiwa na aama 11 baada ya michezo 13, ambapo imeshinda mbili, sare tano na kupoteza sita, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu 15.
Kocha Msaidizi wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema matokeo hayo yametokana na wachezaji wake kupoteza umakini katika eneo la ulinzi na ushambuliaji, kwa kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza kipindi cha kwanza.
Lazaro amesema mwendelezo huo mbaya wa matokeo umeleta hofu na presha kwenye kikosi, kwani yamewafanya wachezaji kutojiamini na kuingia mchezoni wakiwa na hofu ya kupoteza.
”Hatujacheza vibaya, lakini ndiyo presha imetumaliza na wametumia udhaifu wetu. Bado hatujakata tamaa, benchi la ufundi tuna kazi ya kwenda kubadilisha hali hii kuanzia kwenye Uwanja wa mazoezi,” amesema Lazaro.
Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema pamoja na mabadiliko ya kiufundi aliyoyafanya kipindi cha pili, lakini upepo pia umewasaidia kupata mabao matatu.
”Kipindi Cha kwanza tulikuwa tunacheza dhidi ya upepo ambao ulikuwa unakuja sana upande wetu, lakini kipindi cha pili tukawa na faida ya upepo kwenda upande wao na tukaongeza wachezaji wenye kasi,” amesema Baraza.
Pamba Jiji Kirumba yaichapa Coastal Union 3-0