LICHA ya Simba kukosa nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha mkuu wa kikosi hicho, Steve Barker amesema bado anaamini kuna wajibu mkubwa kwa wachezaji wake kupambana katika mechi zilizobaki ili kuilinda heshima ya klabu hiyo.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo dhidi ya Petro Atletico ya Angola, Barker amesema Simba haiwezi kuingia uwanjani bila dhamira ya ushindani kwa sababu imejenga jina kubwa barani Afrika.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amesema kuwa hadhi ya klabu ni kubwa kuliko matokeo ya mechi moja au msimamo wa kundi.
“Ni kweli tumepoteza nafasi ya kufuzu lakini Simba ni klabu kubwa, tunapaswa kucheza kwa ajili ya heshima ya nembo, klabu na mashabiki wetu,” amesema Barker.
Kocha huyo amesema kuwa mechi ya Petro Atletico ni muhimu kwa kikosi chake kwa sababu inatoa fursa ya wachezaji kuonesha tabia ya ushindani, nidhamu na kujituma, mambo ambayo ni msingi wa klabu kubwa kama Simba.
Simba ilianza vibaya hatua ya makundi baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Petro Atletico kwa bao 1-0 kabla ya kukumbana na vipigo vingine viwili mfululizo kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance Tunis, matokeo yaliyowaumiza wanasimba.
“Tuliumia sana hasa katika mechi iliyopita tulitegemea pengine tungebadili kitu. Ilikuwa mechi muhimu kwetu na tulitarajia matokeo mazuri lakini soka lina changamoto zake,” amesema kocha huyo.
Kwa mujibu wa Barker, matokeo hayo yameathiri kisaikolojia kikosi chake, lakini amesema bado anaona dalili za kupambana kwa wachezaji wake, jambo linalompa matumaini kuelekea michezo iliyobaki.
“Hata kama matokeo hayakuwa mazuri, nimeona wachezaji wakipambana. Hilo ndilo jambo muhimu kwangu kama kocha,” amesema.
Simba kwa sasa ina pointi moja pekee katika kundi D, hali inayomaanisha kuwa hata ikishinda mechi zake zote zilizobaki na kufikisha pointi saba, bado haitatosha kuivusha kwenda hatua ya robo fainali.
Hata hivyo, Barker amesema mechi zilizobaki hazipaswi kuonekana kama za kukamilisha ratiba, bali kama fursa ya kujenga heshima na kujiandaa kwa misimu ijayo ya mashindano ya kimataifa.
Kocha huyo pia aliwataka wachezaji wake wakongwe kama Shomary Kapombe kuchukua jukumu la kuwaongoza vijana, akisema uzoefu wao unahitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho timu inahitaji mshikamano na nidhamu.
Barker amesema matokeo mazuri dhidi ya Petro Atletico yatakuwa na maana kubwa kwa Simba, kwani yatarejesha imani ya mashabiki na kuipa timu morali katika michezo ijayo ya mashindano, ikiwemo Ligi Kuu.