Dar es Salaam. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini ikiwamo kujadiliana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP).
Yoweri Museveni anakuwa kiongozi wa kwanza wa kimataifa kufanya ziara yake Tanzania baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 ambao Rais Samia alitangazwa mshindi na kuapishwa kwa muhula wake wa pili.
Vilevile, ziara hiyo ya Museveni ni kwanza nje ya nchi tangu alipotangazwa mshindi katika uchaguzi wa Uganda uliofanyika Januari 15, 2026, akishinda muhula wake wa saba tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 6, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Museveni atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia na watajadili uhusiano baina ya mataifa yao.
“Mazungumzo yao yatajikita kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili, na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.
Pia, inaeleza miongoni mwa masuala yatakayozungumzwa katika mkutano wao ni suala la nishati, hususan mradi wa EACOP, unaotarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa nchi zote mbili na kanda kwa jumla.
Vilevile, viongozi hao wanatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mazungumzo yao.
Ziara hii inakuja wakati ambao nchi zote mbili zinaendelea kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara, usalama na miundombinu.
Kuhusu mradi wa EACOP, Tanzania na Uganda zilitiliana saini mkataba wa makubaliano (IGA) mwaka 2017, kutekeleza wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, Tanzania.
Baadaye Januari 2023, kampuni ya EACOP ilipata leseni kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. Leseni hiyo inaiwezesha kampuni hiyo kujenga bomba lenye urefu wa kilomita 1,443 na upana wa kipenyo cha inchi 24.
Hadi sasa, mradi huo unaendelea kujengwa katika mikoa minane na wilaya 25 zinazopitiwa na mradi huo. Tayari wananchi walishalipwa fidia zao na mradi huo ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa siyo tu kwa Tanzania na Uganda, bali Afrika Mashariki kwa jumla.
Akizungumzia ziara ya Museveni nchini, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema inaashiria uhusiano mzuri na thabiti wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
“Ziara za ngazi ya juu kama hii hulenga kuthibitisha tena imani ya kisiasa, heshima ya pande zote, na ushirikiano wa muda mrefu, hasa katika masuala ya amani na usalama wa kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na eneo la Maziwa Makuu,” amesema Shoo.
Amesema ziara hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi na kimkakati, hususan mradi wa EACOP ambao ni mradi mkubwa wa pamoja kati ya Uganda na Tanzania. Kidiplomasia, amesema inaonesha dhamira ya kuimarisha ujumuishaji wa kikanda na ushirikiano wa maendeleo ya muda mrefu.
“EACOP ni ishara ya utegemeano wa kina katika sekta ya nishati, miundombinu na uwekezaji, huku Tanzania ikithibitishwa kama mshirika muhimu wa kimkakati na nchi ya kupitisha mafuta ya Uganda,” amesema mwanazuoni huyo.
Mtaalamu wa uchumi, Florianus Karugaba amesema mbali na mradi wa EACOP unaotekelezwa na nchi hizo mbili, pia, zimekuwa zikishirikiana katika masuala ya biashara.
“Uhusiano wa nchi na nchi una mambo mengi ndani yake, kwa hiyo mbali ya mradi mkubwa wa EACOP, wamependa kujikagua katika uhusiano wao wa kidiplomasia. Vilevile, baada ya uchaguzi kuna matishio ya kiusalama huwa yanajitokeza kama wameingiliana.
“Kwa hiyo, huwa ni kitu cha kujikagua kwa sababu maendeleo ya miradi mingi mikubwa huwa inagusa vitu vingi katika kitu kimoja, ukizingatia Bunge la Ulaya lilikuwa linapinga mradi huu kwamba unaharibu mazingira, kwa hiyo wanajikagua kupitia hayo yote,” amesema.