Mbeya. Hospitali ya Aga Khan na Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya (MZRH) zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi huku jamii ikiombwa kutumia fursa ya bima ya afya kwa wote kujihakikishia matibabu.
Ushirikiano huo, pia, unalenga kuongeza tija katika kubadilishana ujuzi na kupanua wigo zaidi kwenye utoaji huduma bora, kuleta tafiti na kusaidia wagonjwa kupata matibabu katika vituo tofauti.
Akizungumza leo, Februari 6, 2026 wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema ushirikiano huo utasaidia Taifa kufikia malengo yake ya utalii tiba.
Amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ujuzi, uzoefu na upatikanaji wa ithibati kwa hospitali hiyo kutokana na Aga Khan kupiga hatua kwenye eneo hilo duniani.
“Hospitali yetu ilishapata ithibati upande wa maabara, hivyo Aga Khan watatusaidia kutujengea uwezo kupata ithibati kwa maeneo mengine ikiwamo wagonjwa wanavyoridhika na huduma zetu.
“Kuna maeneo mengine ya tafiti na wagonjwa wanaopata rufaa kutoka hospitali moja kwenda nyingine, lakini Taifa letu linasisitiza utalii tiba kwa wanaotoka nje, hivyo Pato la Taifa litaongezeka,” amesema.
Amesema suala la bima ya afya kwa wote litakuwa suluhisho kwa wananchi akiwaomba kulipa nafasi kubwa kwani tayari Serikali imeshaweka mpango huo kuhakikisha wanapata huduma hiyo.
“Wananchi waone umuhimu wa kukata bima ili kujihakikishia matibabu, unakuta mtu kakatia bima chombo chake cha moto ila yeye hana, lazima tujue sisi wenyewe ni wa muhimu,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh amesema ushirikiano huo utanufaisha pande zote katika maeneo mbalimbali ikiwamo utafiti, huduma za kliniki na kujengea uwezo watumishi.
Viongozi wakisaini makubaliano ya ushirikiano wa taasisi katika nyanja ya afya, tukio lililofanyika jijini Mbeya. leo Februari 6 katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya.
Amesema Mbeya ni mkoa ulioendelea na hospitali hiyo imekuwa inatoa huduma bora, hivyo kushirikiana na Aga Khan kutasaidia zaidi wananchi kupata huduma bora.
“Tunazo idara mbalimbali kwenye Taasisi ya Aga Khan ikiwamo mafunzo ya kitaaluma na fursa nyingine zaidi, huu ni mkakati wetu na tuko tayari kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Konteh.