Rufaa ya aliyekuwa DED Simanjiro yagonga mwamba

Babati. Mahakama Kuu Kanda ya Manyara imeridhia kifungo cha miaka 20 jela kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Gunzah, anayekutumikia kifungo hicho gerezani kwa kosa la rushwa na kutumia madaraka vibaya, baada ya kushindwa rufaa yake.

Uamuzi huo umetolewa leo, Ijumaa Februari 6, 2026, katika mahakama hiyo chini ya Jaji Devota Kamuzora. Kwa mujibu wa uamuzi huo, Gunzah ataendelea kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la rushwa na kutumia vibaya madaraka.

Awali, Gunzah aliyekuwa DED wa Simanjiro kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 alihukumiwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso, Septemba 18, 2026, kwa kosa la kwanza la rushwa na uhujumu uchumi.

Katika hukumu hiyo ya awali, Gunzah alitakiwa kufungwa miaka 20 jela kwa kosa la kwanza na miaka miwili kwa kosa la pili la kutumia madaraka vibaya, hivyo adhabu hizo zinakwenda sambamba.

Kuhusu uamuzi wa leo, Jaji Kamuzora ameeleza kuwa mahakama imeridhia Gunzah aendelee kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Katika ufafanuzi wake, Jaji huyo amesema Gunzah anaendelea kutumikia adhabu hiyo kwa kumpatia mfanyabiashara Elias Tipiliti nafasi ya kukusanya ushuru wa mnada wa mifugo katika mji mdogo wa Orkesumet bila kutangaza zabuni.

Jaji huyo ameeleza kuwa mahakama hiyo, baada ya kupitia upya hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, imeridhika na adhabu hiyo aliyohukumiwa Gunzah.

Amesema ushahidi umeonyesha pasipo shaka kuwa Gunzah alimpatia Tipiliti zabuni ya kukusanya ushuru bila kushindanishwa kati ya Februari 17 hadi 30, 2023, hivyo kuwepo mazingira ya rushwa.

Amesema katika rufaa hiyo iliyofanyika katika mahakama hiyo kuanzia Desemba 11, 2025 hadi Januari 29, 2026, Gunzah alishtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Amesema wamepitia hukumu hiyo na kifungu kilichosomwa pamoja na Aya ya 21, Jedwali la Kwanza, Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupanga, Sura ya 200, R.E. 2022, pamoja na kosa la kutotekeleza wajibu wa kisheria kinyume na Kifungu cha 123 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Amesema mahakama hiyo imeridhia Gunzah kutiwa hatiani na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la kwanza la matumizi mabaya ya madaraka.

Pia, mahakama hiyo imeridhia katika kosa la pili la kutotekeleza wajibu wa kisheria, mshtakiwa kutiwa hatiani na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Amesema Mahakama Kuu imeridhia makosa yote mawili na Gunzah kupata adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 22 gerezani, hivyo aendelee kutumikia adhabu hizo kwa pamoja sawa na kifungo cha miaka 20.