Arusha. Mahakama Kuu Zanzibar imemuachia huru Rehema Mwinyimkuu Mohamed, aliyeshtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa kilo nne, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote, kama inavyotakiwa kisheria katika mashauri ya jinai.
Ildaiwa Januari 31, 2022, saa 8:10 usiku, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, mshtakiwa aliingiza Zanzibar kifurushi cha plastiki cha njano, kikiwa na pakiti nyeusi yenye unga ambao baadaye ulithibitika kuwa ni heroin yenye uzito wa kilo nne.
Hukumu iliyomwachia huru mshtakiwa huyo imetolewa Februari 3, 2026, na Jaji George Kazi, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai, na nakala ya uamuzi huo imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Aidha, katika kesi hiyo mshtakiwa huyo aliwakilishwa na Wakili Suleiman Yusuf Ali, ambapo licha ya kutoroka, Mahakama iliendelea na kesi bila uwepo wake (mshtakiwa), chini ya kifungu cha 260(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Jaji amesema Mahakama iliona kuwa kulikuwa na dosari kubwa katika namna mshtakiwa alivyokamatwa, kupekuliwa, pamoja na jinsi kielelezo kilichodaiwa kuwa dawa za kulevya kilivyohifadhiwa hadi kufikishwa mahakamani.
Mahakama ilisisitiza kuwa, licha ya kesi hiyo kusikilizwa bila uwepo wa mshtakiwa kutokana na kutoroka kwake, wajibu wa upande wa mashtaka wa kuthibitisha kosa haukupungua, na Mahakama ilikuwa na jukumu la kuchunguza ushahidi kwa umakini mkubwa zaidi.
Jaji amesema Mahakama imebaini upekuzi wa mizigo ya mshtakiwa haukufanywa kwa kufuata matakwa ya sheria, hususan kwa kushindwa kuwashirikisha mashahidi huru wa kiraia wakati wa shughuli hiyo, ambayo kwa mujibu wa sheria inahitaji mashahidi huru wawili katika upekuzi unaohusisha makosa ya dawa za kulevya.
Mahakama ilieleza kuwa mashahidi waliodaiwa kushuhudia upekuzi huo walikuwa maofisa wa vyombo vya dola, jambo ambalo halikidhi matakwa ya sheria, ambapo hakukuwa na orodha ya vitu vilivyokamatwa wala uthibitisho wa maandishi uliotiwa saini na mshtakiwa kuonyesha kuwa kielelezo hicho kilipatikana kutoka kwake.
Sababu nyingine iliyotolewa na Mahakama ni kuwepo kwa utata mkubwa kuhusu mahali halisi upekuzi ulipofanyika, ambapo shahidi mmoja alidai upekuzi ulifanyika katika eneo la kukagua mizigo katika uwanja wa ndege, huku shahidi mwingine akieleza kuwa upekuzi ulifanyika katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege.
Jaji amesema tofauti hiyo haikuwa ndogo, bali iliathiri moja kwa moja uaminifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, pamoja na kubaini upungufu katika kuthibitisha mnyororo wa ulinzi wa kielelezo (chain of custody), kwani haikuthibitishwa kwa ushahidi wa maandishi kuwa kielelezo hicho kilibaki salama na bila kuingiliwa kuanzia kilipokamatwa hadi kilipochambuliwa na Mkemia wa Serikali.
Zaidi ya hayo, Mahakama ilieleza kuwa kulikuwa na utata kuhusu uzito halisi wa dawa za kulevya zilizodaiwa kukamatwa, ikizingatiwa kuwa haikuelezwa bayana kama kilo nne zilizotajwa zilihusisha dawa yenyewe pekee au pamoja na vifungashio vyake, jambo ambalo ni muhimu katika makosa ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Jamhuri, ilidaiwa kuwa Januari 31, 2022, mshtakiwa aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) akitokea Afrika Kusini kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Ofisa wa Polisi wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Koplo Rashid, alidai kumtilia shaka mshtakiwa kutokana na tabia yake ya kuonekana na wasiwasi alipokuwa akipanga foleni katika eneo la kuwasili.
Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya kumuita kando na kumhoji, alifanya upekuzi wa begi jekundu la mshtakiwa mbele ya Ofisa wa Usalama wa Uwanja wa Ndege na kubaini kifurushi kilichofungwa kwa sellotape ya njano, kilichodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
Baada ya hapo, mshtakiwa alikamatwa na begi hilo likahifadhiwa kama kielelezo na kuwekewa alama ya utambulisho, ambapo mashahidi wengine wa mashtaka walieleza kuwa kielelezo hicho kilichukuliwa na kupelekwa Maabara ya Mkemia wa Serikali kwa uchambuzi, na kuthibitishwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa kilo nne.
Aidha, katika kesi hiyo mshtakiwa huyo aliwakilishwa na Wakili Suleiman Yusuf Ali licha ya yeye kutoroka, ambapo Mahakama iliendelea na kesi bila mshtakiwa kuwepo, chini ya kifungu cha 260(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.